2015-10-13 09:17:00

Iweni chonjo na wazushi! Sinodi ni chombo cha ushauri kwa Papa!


Hati ya mwisho kutoka katika Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia itakuwepo kama kawaida, lakini ni dhamana na wajibu wa Baba Mtakatifu Francisko kutoa maamuzi kuhusu machapisho haya, kama yatakuwa ni mara tu baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, au itakuchukua muda ili kutoa nafasi kwa Mababa wa Sinodi kufanya tafakari tena kabla ya kuchapishwa au hati hii inaweza kuwa ni sehemu ya Waraka wa kitume utakaochapishwa na Baba Mtakatifu mara baada ya maadhimisho ya Sinodi.

Ufafanuzi huu umetolewa na Padre Federico Lombardi Msemaji mkuu wa Vatican, Jumatatu, tarehe 12 Oktoba 2015 wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari, ili kutoa kwa muhtasari yale yanayojiri katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu hapa mjini Vatican.

Alikizungumzia kuhusu barua inayosadikiwa kwamba, imeandikwa na Makardinali kumi na watatu kwenda kwa Baba Mtakatifu Francisko, Padre Lombardi amewataka waandishi wa habari kuwa makini na vyanzo vyao vya habari pamoja na kuhakiki habari inayotolewa, vinginevyo wanaweza kuonekana kuwa ni wazushi. Kwa vile barua hii haijachapishwa na kuwekwa hadharani, binafsi hana jambo la kuzungumzia, ila baadhi ya Makardinali aliowauliza kuhusiana na uwepo wa barua hii, wamekana kuhusika.

Padre Lombardi anakaza kusema, Mababa wa Sinodi wanaendelea na tafakari zao kwa kuonesha kwamba, Kanisa liko karibu sana na wanandoa wanaoendelea kuogelea katika mtikisiko wa imani na kwamba, vyama vya utume wa familia vinapaswa kuimarishwa zaidi ili kuwasaidia wanandoa katika hija ya maisha yao. Wanandoa watarajiwa wapewe mafundisho makini na endelevu, tayari kusimama kidete kulinda na kutangaza Injili ya Familia.

Kanisa linapaswa kuwa makini na mchakato wa kutengua ndoa tata na kwamba, wanandoa waliotalakiana na hatimaye kuamua kuoa au kuolewa wanaotaka kupokea Ekaristi takatifu, hawana budi kufanya hija ya toba na wongofu wa ndani. Utume kwa vijana, utamadunisho, vipigo vya majumbani, ndoa mseto na changamoto zake hususan katika nchi ambazo zina idadi kubwa ya waamini wa dini ya Kiislam; dhambi na mdhambi.

Kuna umuhimu wa pekee kabisa Kanisa kuambata Mafundisho tanzu ya Kanisa katika shughuli na mikakati ya kichungaji. Lugha makini kwa Mababa wa Sinodi na kwamba, wajumbe wengi wa Sinodi wanataka kushuhudia Kanisa linalojikita katika huduma kwa wanandoa na familia.; mambo ambayo yameendelea kukaziwa zaidi na Mababa wa Sinodi. Padre Federico Lombardi katika mazungumzo yake na waandishi wa habari amesaidiwa na Padre Bernd Hagenkord, mrataibu wa habari za Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia katika lugha ya Kijerumaini, ambaye pia ameonesha umakini wa Mababa wa Sinodi katika kuchambua na kupembua maisha na utume wa wanandoa na familia katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.