2015-10-13 15:01:00

Familia ya Mungu iweni mashuhuda wa kweli wa Injili ya Familia!


Askofu James Maria Wainaina wa Jimbo Katoliki Muran’ga, Kenya anamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuitisha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia, ambayo imeadhimishwa katika awamu kuu mbili: Sinodi maalum iliyofanyika kunako mwaka 2014 pamoja na Sinodi ambayo inaendelea kwa wakati huu mjini Vatican kwa kuongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa familia katika Kanisa na ulimwengu mamboleo”.

Askofu Wainaina katika mahojiano maalum na Radio Vatican kuhusiana na maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia anakaza kusema, maadhimisho haya imekuwa ni nafasi kwa Mama Kanisa kufafanua kwa kina na mapana maana, maisha na utume wa ndoa na familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo, kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Lakini haitoshi tu kwa waamini kufahamu, bali jambo la msingi ni kukazia ushuhuda unaotolewa katika maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu kwa kujikita katika kanuni maadili, utu wema, sala na tafakari ya Neno la Mungu, kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji inajikita katika Injili ya familia katika uhalisia wa maisha ya waamini.

Askofu James Maria Wainaina anakaza kusema, ushuhuda wa Injili ya familia, licha ya changamoto zake, ni kielelezo tosha kabisa cha nguvu ya Mungu inayotenda kazi kati ya Watu wa Mungu katika maisha ya kifamilia. Kumbe, hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, Familia ya Mungu inakuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya familia inayojikita katika ushuhuda kamili!

Askofu Wainaina anasema, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuona Kanisa likijisadaka kwa ajili ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Dhamana na utume huu unaendelezwa kwa namna ya pekee nchini Kenya katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu ya binadamu yanayogusa mahitaji msingi ya binadamu kiroho na kimwili. Kanisa limekuwa ni mdau wa pekee nchini Kenya katika mchakato wa huduma Familia ya Mungu nchini Kenya.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kufanya hija ya kichungaji nchini Kenya, Uganda na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 30 Novemba 2015, atakaporejea tena mjini Vatican kuendelea na utume na maisha yake. Familia ya Mungu katika nchi zitakazotembelewa na Baba Mtakatifu Francisko zinaendelea kukazia umuhimu wa kujindaa vyema ili kumpokea mgeni huyu mahususi ambaye anakwenda Barani Afrika ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, ili hatimaye, waweze kuwa ni madaraja ya watu kukutana na vyombo vya haki, amani na upatanisho wa kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.