2015-10-12 15:07:00

Vijana jengeni utamaduni wa haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa!


Waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema nchini Senegal hawana budi kujikita katika mchakato unaopania kujenga na kudumisha upendo, udugu, majadiliano na maridhiano kati ya waamini wa dini mbali mbali, ili amani, ustawi na maendeleo ya wengi yaweze kushika mkondo wake. Kwa namna ya pekee, vijana wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa kweli ni vyombo vya haki, amani na utulivu.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Askofu Andrè Guèye wa Jimbo Katoliki Thies, Senegal mara baada ya kukamilisha hija ya maisha ya kiroho kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Popenguine. Pamoja na Bikira Maria, wote kwa ajili ya Kanisa, Familia ya Mungu. Katika mahubiri yake, Askofu Guèye amepembua kwa kina na mapana hali halisi ya kisiasa, kijamii, kidini na kiuchumi inavyoendelea kuyumba kutokana na misigano ya kidini, jambo ambalo linahitaji kwa namna ya pekee kabisa ujenzi wa umoja, udugu na mshikamano wa kitaifa sanjari na kuendeleza majadiliano ya kidini, ili amani iweze kutawala miongoni mwa wananchi wa Senegal.

Ulimwengu mamboleo unakabiliwa na changamoto kubwa ya: vita, kinzani, dhuluma na nyanyaso zinazofanywa kwa misingi ya misimamo mikali ya kidini, jambo ambalo linahatarisha usalama, amani na mafungamano ya kijamii. Senegal inaweza kuw ani mfano bora wa kuigwa kwa kujikita katika majadiliano ya kidini yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kawaida, vijana wakipewa kipaumbele cha kwanza.

Askofu Guèye anawataka vijana kuwa makini na watu wanaotaka kupandikiza mbegu ya chokochoko, chuki na uhasama kati ya watu kwa kusema kwamba, hawa ni watu wanaopaswa kuogopwa kama “ugonjwa wa Ebola” kwani hawalitakii taifa mema. Watu watambue kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kumbe ni watoto wa Mungu, tofauti zao za kidini uwe ni utajiri kwa ajili ya kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Wananchi wote wa Senegal wanaunda familia moja ya Mungu inayowajibikiana na kusumbukiana wakati wa shida na raha. Askofu mkuu Benjamini Ndiaye wa Jimbo kuu la Dakar, Senegal anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini humo kuongeza bidii ya kutafuta amani, utulivu, maridhiano na maendeleo ya wananchi wote wa Senegal. Kila mtu aweze kupata fursa ya kuboresha maisha yake. Serikali itambue dhamana na wajibu wake wa kulinda na kudumisha amani, ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Senegal pamoja na kuendelea kuhamasisha upatanisho wa kitaifa, ili kuganga na kuponya madonda ya utengano yaliyojitokeza katika historia ya wananchi w Senegal.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.