2015-10-12 08:18:00

Tunzeni mazingira nyumba ya wote ili kupunguza majanga asilia!


Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko kwa masikitiko makubwa anasema amepokea taarifa za mauaji ya kinyama yaliyofanyika mjini Ankara, nchini Uturuki, Jumamosi tarehe 10 Oktoba 2015 wakati wananchi walipokuwa wanafanya maandamano ya amani. Kuna watu wengi wamepoteza maisha na wengine wengi kupata majeraha na vilema vya kudumu.

Huu ni uchungu mkubwa kwani mashambulizi haya yamefanywa kwa watu wasiokuwa na hatia. Baba Mtakatifu anawaombea wale wote waliopoteza maisha, huruma ya Mungu na waliopata majeraha waweze kupona haraka. Amewaalika waamini na watu wote waliokuwa wamekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kusali katika hali ya ukimya ili kuwaombea wote walioguswa na msiba huu mkubwa nchini Uturuki.

Baba Mtakatifu pia amekumbusha kwamba, Jumanne, tarehe 13 Oktoba 2015, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya kupunguza majanga asilia. Athari za uharibifu wa mazingira zinaendelea kuongezeka maradufu kutokana na binadamu kutojali utunzaji bora wa mazingira. Baba Mtakatifu anapenda kuungana na wote wanaojibidisha kulinda na  kutunza mazingira nyumba ya wote sanjari na kujenga utamaduni wa utunzaji wa mazingira ili kupunguza na kudhibiti majanga asilia. Iwe ni fursa ya kuunganisha ufahamu wa tafiti za kisayansi na mapokeo, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa wananchi maskini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.