2015-10-12 07:37:00

Tatizo la saruji Tanzania kupewa kisogo hivi karibuni!


Tanzania hivi karibuni itaanza kujitegemea kwa saruji, bila kulazimika kuagiza bidhaa nje, kufuatia kuzinduliwa kwa kiwanda kikubwa zaidi cha kuzalisha saruji kuliko kingine chochote katika Afrika Mashariki kilichojengwa katika eneo la Msijute, Mtwara Vijijini, Mkoa wa Mtwara ikiwa ni uwekezaji wa mabilioni ya fedha wa Kampuni ya Dangote Group ya Nigeria. Aidha, Kampuni hiyo imesema kuwa imechagua kuwekeza Tanzania katika ujenzi wa Kiwanda hicho na huduma za upakiaji na upakuaji mizigo katika eneo lenye ukubwa wa hekta 25 katika Kijiji cha Mgao, kilichoko karibu na kiwanda hicho, kwa gharama ya dola za Marekani milioni 600 kwa sababu ya sera nzuri za Serikali na mazingira mazuri na rafiki ya kufanyia biashara yaliyojengwa na Serikali ya Tanzania.

Kampuni hiyo pia imesema kuwa Kiwanda hicho ndicho kimejengwa kwa kasi zaidi na kwa muda mfupi zaidi miongoni mwa viwanda vyote vya saruji ambavyo vimejengwa na Kampuni hiyo katika Bara la Afrika. Ujenzi wa Kiwanda hicho umechukua miezi 30 tu, miaka miwili unusu, tokea ujenzi huo ulipoanza Mei 27, mwaka 2013, kufuatia mkataba uliotiwa saini kati ya Kampuni hiyo na Serikali ya Tanzania. Vile vile, Kampuni hiyo imetangaza kuwa imeamua kuwekeza zaidi katika Tanzania, na zamu hii, katika sekta ya kilimo ambako Dangote Group imeanza majadiliano na Serikali kwa ajili ya kuwekeza katika uzalishaji wa sukari.

Kiwanda hicho kilichozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete umefanywa Jumamosi, Oktoba 10, 2015 ni Kiwanda cha nne cha saruji kuzinduliwa na Kampuni ya Dangote Group katika Bara la Afrika katika miezi minne tu iliyopita na wala siyo cha mwisho kuzinduliwa na Kampuni hiyo mwaka huu. Akizungumza katika sherehe ya uzinduzi, Rais na Mtendaji Mkuu wa Dangote Group, Alhaj Aliko Dangote amesema kuwa kiwanda hicho ambacho kitazalisha saruji tani za ujazo milioni tatu kwa mwaka ni kiwanda kikubwa zaidi cha saruji katika Afrika Mashariki na kitakidhi mahitaji ya bidhaa hiyo nchini na kubakiza kiasi cha kutosha kwa ajili ya kuuza nje.

“Tutakapofikia kiwango cha juu kabisa cha uzalishaji wetu, Kiwanda hiki kitaiwezesha Tanzania kujitegemea kwa mahitaji ya saruji na kubakiza kiasi kikubwa tu kwa ajili ya kuuza katika masoko ya nje,” Alhaj Dangote amemwambia Rais Kikwete na mamia ya wananchi waliohudhuria sherehe ya uziduzi huo ambao walikuwa ni pamoja na wafanyabiashara 172 kutoka Nigeria ambao Alhaji Dangote aliwaalika katika sherehe hiyo. Miongoni mwa wageni hao pia walikuwepo kwenye sherehe hizo ni Mwakilishi wa Serikali ya Nigeria, Alhaj Mallam Nasir Ahmad el Rufai, Gavana wa Jimbo la Kaduna, Wajumbe wa Bodi ya Dangote Group na mabinti zake Dangote watatu ambao karibu wote wamepanda ndege zao binafsi jioni ya leo baada ya shughuli hiyo kurejea kwao Nigeria.

Kuhusu uamuzi wa Makampuni ya Dangote kuwekeza katika Tanzania, Alhaji Dangote amesema:“Tunamshukuru sana Rais Kikwete. Serikali yake ilitengeneza mazingira rafiki ya kutuwezesha kuwekeza. Jambo kubwa kwetu sisi wafanyabiashara ni kuwepo kwa mazingira rafiki ya uwekezaji. Kwa hakika, Tanzania ni moja ya nchi rafiki zaidi kwa ajili ya kuvutia uwekezaji katika Afrika. Mageuzi ambayo nchi hii imefanya katika sekta mbali mbali na kukua kwa uhakika kwa uchumi, ni mambo yaliyotuongoza kuichagua Tanzania kama nchi yetu ya kuwekeza.”

Ameongeza kuwa Dangote Group imeamua kuwekeza katika Kiwanda hicho katika Tanzania kwa sababu inataka kuchangia katika ujenzi wa miundombinu ya Tanzania, kupanua fursa za ajira na kushiriki katika maendeleo ya jumla. Kiwanda hicho kinatarajia kutoa ajira 1,500 za moja kwa moja na 9,000 zisizokuwa za moja kwa moja.  “Mwono wetu pia ni kuwekeza katika uchumi ambazo zina uwezo wa kurudisha gharama za uwekezaji huo kwa uhakika na kuwa ujenzi wa Kiwanda hicho utazidi kuimarisha uhusiano kati ya nchi rafiki za Tanzania na Nigeria.”

Kuhusu mipango yake ya kuiwezesha Afrika kujitegemea kwa uzalishaji wa saruji na kupunguza idadi ya fedha za kigeni zinazotumiwa na nchi za Afrika kuagiza saruji kutoka nje, Alhaj Dangote amesema: “Kiwanda hiki ni moja ya miradi yetu yenye mafanikio ambayo inaendelea kujengwa katika nchi 18 za Afrika kwa mujibu wa mkakati wetu wa uwekezaji katika Bara la Afrika.” Ameongeza:“Agosti mwaka huu, tumezindua viwanda viwili vipya katika Zambia na Cameroon. Na mwezi Juni, mwaka huu, tulifungua kiwanda chetu katika Ethiopia. Kabla ya mwisho wa mwaka huu, tutazindua viwanda vyetu vingine katika baadhi ya nchi nyingine za Afrika zikiwemo Senegal na Afrika Kusini. Tunaamini ipasavyo katika uwezo wa kiuchumi wa Afrika na maendeleo ya baadaye ya Bara la Afrika.”

Ameongeza Alhaj Dangote: “Vile vile mwezi Agosti mwaka huu mjini Lagos, tuliwekeana saini makubaliano ya kiasi cha dola za Marekani bilioni 4.34 na Kampuni ya Sinoma International Engineering kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vingine 10 vya saruji katika nchi nyingine za Afrika na katika nchi ya Nepal iliyoko Bara la Asia. Uwezo wa jumla wa kuzalisha tani za ujazo milioni 25 kwa mwaka. Miradi hii ikikamilika katika miaka michache ijayo, Dangote Group itakuwa na uwezo wa kuzalisha tani za ujazo milioni 81 kwa mwaka na hivyo kuifanya Kampuni yetu kuwa moja ya kampuni kubwa zaidi za uzalisha saruji duniani.”

Kampuni ya saruji ya Dangote Cement Plc ndiyo kampuni kubwa zaidi katika Nigeria na Afrika Magharibu nzima katika Soko la Hisa la Nigeria (NSE) tokea ilipoandikishwa kwenye Soko hilo Oktoba mwaka 2010. Kampuni hiyo inasudia kujisajili kwenye masoko ya hisa ya Johannesburg (Afrika Kusini) na London (Uingereza).

 

Na mwandishi maalum.








All the contents on this site are copyrighted ©.