2015-10-12 08:36:00

Mang'amuzi ya wito wa ndoa!


Kikao cha sita cha jumla cha Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, Jumamosi asubuhi, tarehe 10 Oktoba 2015, kiliendelea kutafakari na kushirikiana sehemu ya pili ya Hati ya kutendea kazi, Instrumentum Laboris kuhusu mang’amuzi ya wito wa ndoa, kwa kukazia kwa namna ya pekee, huruma ya Mungu kama dawa ya kuponya madonda ya utengano ndani ya familia sanjari na maandalizi ya kutosha kwa wanandoa na familia.

Kanisa linapaswa kuendeleza dhamana na utume wake wa kuwa Mama na mwalimu, huku likifungua malango ya huruma na upendo, kwa wote wanaotubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, tayari kuambata huruma ya Mungu. Shughuli za kichungaji zinazojikita katika huruma ya Mungu hazina budi kuwa karibu na familia kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya wokovu kwa wote. Huruma ni kazi ya wokovu na kielelezo cha hali ya juu kabisa cha haki ya Mungu inayomwilishwa kwa wadhambi wanaokumbatiwa na kuhurumiwa na Kristo Yesu, kama sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wake hapa duniani.

Mababa wa Sinodi wanakaza kusema, huruma ya Mungu kamwe haisigani na ukweli mfunuliwa, bali ni mambo mawili yanayokamilishana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu. Wanandoa watarajiwa watambue kwamba, Ndoa ni wito mtakatifu unaowahamasisha waamini kujenga familia inayojikita katika kifungo cha upendo kamili katika Sakramenti ya Ndoa, ambayo kimsingi ina mwelekeo wa kudumu. Waamini wanaweza kuishi Sakramenti hii wakiwa wameungana na kushibana na wenzi wao hadi pale mauti itakapowatenganisha kadiri ya mpango wa Mungu.

Hii si ndoto bali ni jambo linalowezekana kabisa na kwamba, kuna ushuhuda wa kutosha, kumbe, vijana hawana budi kufanya maamuzi mazito katika maisha yao, pamoja na kuendelea kutumainia neema na huruma ya Mungu katika safari ya maisha yao ya ndoa na familia. Parokia, Majimbo na Mabaraza ya Maaskofu yanapaswa kuwaandaa vituo maalum vya katekesi kwa ajili ya ndoa kwa kuwa na watu makini wanaoweza kutekeleza azma hii kwa weledi mkubwa, ili kuwafunda wanandoa watarajiwa barabara, kuliko mtindo wa sasa unaowaacha wanandoa wengi wakiwa bado hawajafundwa kikamilifu.

Mababa wa Sinodi wametambua umuhimu wa watoto katika maisha ya ndoa na familia. Watoto hawa wapewe malezi ya kutosha tayari kupambana na changamoto mbali mbali zinazoweza kujitokeza katika hija ya maisha yao kiroho na kimwili. Imani, matumaini na mapendo, uwe ni ushuhuda makini unaotolewa na wazazi pamoja na walezi kwa watoto wao. Kadiri ya mpango wa Mungu, mwanaume na mwanamke wameumbwa ili kuweza kukamilishana pamoja na kushiriki katika kazi ya uumbaji, ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu. Kumbe, ndoa za watu wa jinsia moja haziwezi kukubalika ndani ya Kanisa kwani ni kinyume kabisa cha mpango wa Mungu kwa binadamu na ni jambo linalokiuka utu na heshima ya binadamu.

Mababa wa Sinodi wanakaza kusema, jamii inayokosa dira na mwelekeo, matokeo yake ni kumong’onyoka kwa maadili na utu wema, hali inayojionesha pia kwa njia ya ukanimungu. Ekolojia ya binadamu inapania kuonesha uzuri wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanandoa wasaidiwe ili kuhakikisha kwanza wanayafahamu Mafundisho ya Kanisa kuhusu Ndoa na Familia, tayari kuyaishi na kuyatolea ushuhuda.

Wanandoa wajikite katika maisha ya Sala na Tafakari ya Neno la Mungu, ili kukabiliana na changamoto za maisha katika hali ya utulivu na amani. Ni dhamana na wajibu wa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anawafundisha waamini mafundisho tanzu ya Kanisa na Ukweli mfunuliwa, kwa kuwasaidia wanandoa kuwa karibu zaidi na Kristo Yesu. Familia zote zijengewe utamaduni wa kusikilizwa pasi na ubaguzi, ili ziweze kuona na kuonja, uwepo wa Kristo kati yao kwa njia ya wahudumu wa Injili. Wachungaji wawe na busara ili kuzisaidia familia katika hali ya upendo kama alivyofanya Baba mwenye huruma, kama anavyosimuliwa kwenye Injili ya Luka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.