2015-10-12 16:07:00

Ikulu ni mahali patakatifu, lazima aende huko mtu safi na mwenye moyo mweupe!


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Mizengo Pinda amesema CCM itashinda kiti cha Urais bila wasiwasikwa sababu ina mgombea mzuri ambaye hawezi kulinganishwa na wagombea kutoka vyama vingine. “Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli ana mvuto kwa jamii, mtazamo wake wa wapi anataka kuipeleka Tanzania unaeleweka na uko wazi, katika utumishi wake ana rekodi nzuri, hapendi watu wavivu sababu yeye ni mchapakazi,” alisema.

Ametoa kauli hiyo Jumapili, Oktoba 11, 2015 wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa jimbo la Sumbawanga Mjini kwenye mikutano miwili ya hadhara iliyofanyika katika kijiji cha Mawenzusi, kata ya Molo na Uwanja wa Stendi ya Chanji uliopo Sumbawanga Mjini.  “Mgombea wetu ni safi sana na hata hao wapinzani wanajua lakini kazi yao ni kuonyesha kuwa Serikali ya awamu ya nne haijafanya kitu na kutoa ahadi za uongo kuwa katika siku 100 za mwanzo wataigeuza nchi iwe kama mbingu. Inawezekana hiyo?” alihoji na kujibiwa na wananchi kuwa haiwezekani. Alisema CCM kupitia Ilani yake imetekeleza mambo mengi lakini akakiri kwamba kazi ya kuleta maendeleo ina changamoto nyingi lakini hazina budi kupitiwa hatua kwa hatua ili kukabiliana nazo. Alitumia fursa hiyo kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe Magufuli pamoja na mgombea ubunge wa jimbo hilo, Bw. Khalfan Aeshi Hilaly. Pia aliwanadi wagombea udiwani wa kata 19 za jimbo hilo wakiwemo madiwani wa viti maalum ambao walihudhuria mikutano hiyo.


Katika hatua nyingine, Mbunge wa zamani wa Jimbo la Kwela, Dkt. Chrissant Mzindakaya ametangaza rasmi kuwa amemsamehe Bw. Khalfan Aeshi Hilaly ambaye anagombea ubunge jimbo la Sumbawanga Mjini na kuahidi kufanya naye kazi kuleta maendeleo kwa wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga na vitongoji vyake. “Tarehe 21 Agosti mwaka huu nilifanya ibada ya kuadhimisha miaka 75 ya kuzaliwa kwangu. Nilimwita Bwana Aeshi na kutangaza rasmi kwamba nimemsamehe na yamekwisha, hakuna haja ya baraza kwani kinachotoa msamaha ni roho ya mtu binafsi,” alisema. “Nilitamka Zaburi ya 133 ambayo inasema: Tazama, jinsi ilivyo vema ndugu wakae pamoja na kwa umoja…. Na hapa namwombea kura kwenu wana-Sumbawanga na wala msamaha wangu kwa Aeshi usiwe ajenda ya kisiasa. Mbona Sumaye na Mbowe wanamuombea kura Edward Lowassa wakati wao walikuwa wanamnanga kila siku?” alisema huku akishangiliwa.

Mei 25, 2014 kwenye ibada ya kumuweka wakfu Askofu Mteule Conrad Nguvumali wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Rukwa iliyofanyika kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga, Dkt. Mzindakaya alikataa kumsamehe hadharani Bw. Aeshi Hilaly baada ya kupewa fursa ya kushikana mikono jukwaani na kusameheana. Mzee Mzindakaya alikataa kufanya hivyo akisema yeye ni mkristu lakini hakuwa ameandaliwa kiroho kwa ajili ya tukio hilo. “Hapa ni shughuli ya Kanisa na si mkutano wa Chama. Lazima niwe mkweli leo sijajiandaa kwa jambo hili… Mimi ni mtu mzima, nafsi ya msamaha inahitaji maandalizi, nahitaji maandalizi ya kiroho,” alisema.

Dkt Mzindakaya ambaye alikumbatiana jukwaani na Bw. Aeshi na kusema atashirikiana naye kwa lolote kwa sababu ni kijana wake, alitumia fursa hiyo pia kumuombea kura Dk. Magufuli kwa sababu ni mtu safi na ni mchapakazi mwenye nia ya kuibadilisha Tanzania kiuchumi kupitia sekta ya viwanda. “Miaka 10 ijayo Tanzania itakuwa inaongoza kwa wingi wa viwanda. Wiki ijayo Rais Kikwete anaweka jiwe la msingi kwenye kiwanda cha chuma... hiki kitakuwa kiwanda cha nne kwa ukubwa barani Afrika,” alisema. Aliwataka Watanzania wawapime wanaowania urais kwa vitendo kwani baadhi yao miezi kadhaa iliyopita walikuwa wakimsifu Rais Kikwete na Serikali yake lakini sasa hivi wanamkebehi. “Rais ni mteule wa Mungu na Ikulu ni mahali patakatifu. Lazima tupeleke mtu aliye safi, aliyetakata na mwenye mikono safi, na huyo si mwingine bali ni Dkt. Magufuli,” alisema.








All the contents on this site are copyrighted ©.