2015-10-11 15:33:00

Sinodi juu ya Familia: Huruma haina maana ya kupuuza mafundisho ya Kanisa


Mwishoni mwa wiki ya kwanza ya Mkutano wa Kawaida wa Sinodi ya Maaskofu juu ya familia iliyoanza rasmi Jumatatu 4 Oktoba 2015 mjini Vatican, Jumamosi baada ya kukamilisha kazi za mikutano,ikiwa ni siku ya sita,  Padre Thomas Rosica CSB, Afisa Mwambata wa  Vyombo vya habari vya Jimbo la Papa, aliungana na  Padre Federico Lombardi SJ, Mkuu wa Idara ya Habari Vatican, kutoa muhtasari wa majadiliano ya Sinodi kwa waandishi wa habari.

Padre Lombardi, akilenga katika kazi za sinodi kwa siku mbili za mwisho yaani Ijumaa na Jumamosi aliwaambia wanahabari kwamba,  masuala kadhaa yameshughulikiwa kupitia majadiliano ya vikundi vidogovidogo vya  Mababa wa sinodi, huku wakiendelea na kutoa michango yao juu ya sehemu ya pili ya rasimu ya kufanyia kazi shughuli zao (Instrumentum Laboris).  Na mara walipokamilisha sehimu hiyo ya pili, walianza pia kusikiliza michango ya wajumbe kwa ajili ya sehemu ya tatu  ya rasimu.

Padre Lombardi aliendelea kutaja, katika kipindi hiki, jumla ya michango 75 imetolewa katika vikao vya pamoja kutoka Mababa wa Sinodi wakiwakilisha maeneo ya Ulaya, Afrika, Mashariki ya Kati, na Amerika ya Kusini. Na kulikuwa pia na michango michache kutoka eneo la Amerika ya Kaskazini.

Na kati ya mandhari zilizoibuka katika michango hiyo ni pamoja na hali ya kiroho ya maisha ya familia, wajibu wa kimisionari kwa familia katika kutunza na  kuendeleza ndoa bora, uwajibikaji katika majukumu na harakati mbalimbali za familia katika Kanisa, na kwa jinsi gani Kanisa linaweza kubaki karibu na kutoa msaada kwa familia zinazokabiliwa na matatizo katika yote kiroho na kihali pia.

Pia kulikuwa na michango kadhaa juu ya  uhusiano na uwiano kati ya haki na msaada. Na kwamba katika mada hii kulikuwa na  maoni tofauti tofauti juu ya suala hili miongoni mwa Mababa. Mmoja wa Baba alisema kuwa huruma haimaanishi kutelekeza mafundisho ya Kanisa.

Katika Mkutano huu wa wanahabari,  Mgeni rasmi alikuwa Mwenye Heri Baselios Cleemis Thottunkal, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki India, ambaye pia ni Mkuu wa Kanisa Katoliki katika eneo ya  Syro- Malankara.  Naye aliwaambia wanahabari kwamba, huruma maana yake ni kukubali kubadiliko ya kiroho pande zote mbili. Injili inataka hilo kutendeka kama sharti kwamba,  Ufalme wa Mungu umekaribia,ongokeni, alisema.

Aidha Mababa wa Sinodi walionyesha kujali hali ya familia za wanajeshi, ambao kwa mara nyingi hufanya kazi zao za kijeshi mbali na nyumbani kwao mbali na familia zao tena inaweza kuwa  kwa kipindi kirefu. Hawa wanaume na wanawake, kama inavyotakiwa kwa  familia zao, pia wao wanajeshi wana haja ya kupata huduma maalum kichungaji.

Pia Mababa wa Sinodi, wameonyesha kukubali kwamba, kutokana na hali tofauti na mazingira tofauti, haiwezekani kuwa na mlingano wa familia au kama "familia ya kawaida". Wajumbe wengi walizungumzia jinsi isivyokuwa rahisi kwa waliopokea sakramenti ya ndoa kutangua ndoa, maana huo ni  utambulisho muhimu wa ndoa ya Kikristo.

Michango mingi ya Mababa wengi wa Sinodi, ilizungumzia kwa kina, umuhimu wa kuwa na maandalizi thabiti kwa wachumba wanaotaka kufunga ndoa kanisa. Wametaja kuwa, ni muhimu sana  kwa wachumba kupata majiundo na malezi ya kutosha  kabla ya ndoa, ili wapate ufahamu kamili wa kile wanachotaka kukifanya, kwamba mara wakisha kula kiapo altareni hakuna tena namna ya kutangua maamuzi yao. Mababa wa Sinodi waliona tatizo hasa kwa wanaotaka kutangua ndoa, ni ukosefu wa umakini wa kutambua wanachokifanya tangu mwanzo wa uchumba. Mjumbe mmoja alisema kuwa, Maaskofu wenyewe wanapaswa kukubali  kosa lao  kwamba, wameshindwa kutoa malezi ya kutosha kwa  waumini wa kawaida katika suala hili. Na mchango mwingine ulishauri kwamba, wachumba kama ilivyo katika malezi ya au maisha ya kitawa ni lazima wapitie kipindi cha "Unovisi” kabla ya kuingia katika sakramenti ya ndoa. Kulikuwa na fikira kwamba,  vipeo vinavyoonekana katika miito ya Upadre na Utawa, pia ni mgogoro huohuo unaoonekana katika maisha ya ndoa na  familia.

Pia Wanahabari waliuliza maswali mbalimbali kuhusu mchakato wa Sinodi, kufuatia pendekezo lililotolewa kwamba, kwa siku zijazo , inafaa mchakato ufanyike kwanza katika katika ngazi ya bara, na kisha  maoni ya bara yafikishwe katika Mkutano Mkuu wa Sinodi ya kawaida kwa uchambuzi wa mwisho. Hii ina maana kwamba masuala yatakuwa yamejadiliwa kwa umakini zaidi na kuandaliwa vyema, kulingana na mazingira ya bara,  kabla ya kufikishwa katika Mkutano wa Sinodi ya jumla ya Kanisa la Ulimwengu .  Mwenye Heri  Kardinali Thottunkal alijibu hoja hiyo,kwa kuonyesha kukubaliana na hoja akisema, ni kweli inafaa hoja kuanza kujadiliwa katika mazingira ya ndani ya nchi na bara, kabla ya kuletwa katika Mkutano wa Sinodi kama huu. Na kwake yeye,  hakuna utata katika mfumo wa  mbinu hii na wazo  kwamba, mchakato kama huo unaweza kuwa na  matunda bora zaidi kwa ajili ya kanisa zima.

Padre Federico Lombardi , alifafanua kwamba, Rasimu ya kufanyia kazi (Instrumentum Laboris)  inaweza kubadilishwa iwapo maoni ya wajumbe wengi katika makundi madogomadogo ya vikao vya Sinodi , wengi  watapendekeza mabadiliko. Pendekezo kisha, litafikishwa katika Kamati ya Sinodi. Na aliwakumbusha wanahabari kwamba, michango inayotolewa na wajumbe katika vikao si mapendekezo  kwa Sinodi; lakini ni sehemu ya "mazungumzo" tu ya Mkutano wa Sinodi. 

Aidha Padre Federico Lombardi alisema , athari za uhamiaji, ni hoja iliyokuwa ikijirudia mara kwa mara katika majadiliano ya Sinodi katika wiki ya kwanza. Kardinali Thottunkal alisema kuwa yeye anakubaliana na wazo la Papa Francisco, linalo himiza watu wote kuwapokea wahamiaji katika misingi ya Msamaria mwema. Lakini hata hivyo akasema, alipenda kuongeza maoni yake binafsi katika hilo, akionyesha  imani yake kwamba,  jumuiya ya kimataifa na viongozi wa nchi na serikali, wanapaswa kufanikisha kila linalowezekana kwa watu kubaki katika nchi zao . Na kwamba ni lazima kufanya kila jitihada za kuhakikisha watu wanabaki nchini mwao,  alisema.

Mababa wa Sinodi, baada ya mapumziko ya Jumapili, wataanza tena  kazi zao siku ya Jumatatu asubuhi. 








All the contents on this site are copyrighted ©.