2015-10-10 08:50:00

Maadhimisho ya Sinodi ya Familia yanapania mafao, ustawi na maendeleo ya familia


Patriaki Ignace Youssif  Younan wa III wa Kanisa la Wakatoliki wa Syria, ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kutowasahau na kuwatelekeza wananchi wa Syria, kwani madhara ya vita ni makubwa sana kwa maisha ya familia nyingi huko Mashariki ya kati. Kuna baadhi ya wananchi wanalazimika kuzikimbia familia na makazi yao, huko Syria na Iraq ili kusalimisha maisha yao. Imekuwa ni vigumu sana kuweza kuwashawishi vijana wa kizazi kipya kubaki nchini mwao kutokana na hali halisi wanayokabiliana nayo kila siku ya maisha yao. Ni vigumu kwa Wakristo kuendelea kubaki katika maeneo ambamo ni chimbuko la Ukristo. Hadi sasa kuna maelfu ya wananchi ambao wanashikiliwa na vikundi vya kigaidi na madhara yake ni makubwa katika maisha ya wananchi huko Mashariki ya Kati.

Patriaki Ignace Youssif Younan wa III anawasihi viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa hususan kutoka Ulaya na Marekani kutowasahau kwani hadi sasa wanajisikia kana kwamba, wamesalitiwa na viongozi ha ona kwamba, wanaendelea kutoa kilio cha wanyonge huko Mashariki ya Kati, ili viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa waweze kufanya maamuzi machungu ili hatimaye, kupata amani na utulivu wa kudumu, kikolezo makini cha maendeleo ya watu kiroho na kimwili. Patriaki Younan ameyasema haya wakati baadhi ya Mababa wa Sinodi walipokuwa wanazungumza na waandishi wa habari, tukio ambalo limeratibiwa na Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican, baada ya kukamilisha tafakari na majadiliano ya makundi madogo madogo .

Kwa upande wake, Askofu mkuu Charles Palmer-Buckle wa Jimbo kuu la Accra, Ghana anasema, ujumbe wa Mababa wa Sinodi kutoka Barani Afrika, hauna nia wala mpango wa kukwamisha maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia. Bara la Afrika lina mtazo mpana kuhusu dhana ya familia. Ni dhamana na wajibu wa Mababa wa Sinodi kuona kwamba, familia zinaendelea kujikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu, kama chemichemi ya furaha na amani ya familia yenyewe.

Ikumbukwe kwamba, maisha na utume wa Kanisa kwa siku za usoni, uko mikononi mwa familia na kwa namna ya pekee Barani Afrika ambako, Kanisa linaendelea kukua na kukomaa kwa kasi ya ajabu. Mababa wa Sinodi kutoka Afrika wanakaza kusema kwamba, wito na utume wa familia unaojadiliwa na kupembuliwa na Mababa wa Sinodi si tu kwa ajili ya Kanisa Barani Ulaya, bali ni kwa Kanisa la kiulimwengu.

Kardinali Edoardo Menichelli, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Ancona-Osimo akichangia mada wakati wa mazungumzo na waandishi wa habari anakaza kusema, majadiliano ya Mababa wa Sinodi katika makundi madogo madogo ni fursa inayowashirikisha wengi katika kuchangia mawazo. Mababa wa Sinodi wamegusia hata uwezekano wa kuwa na Mashemasi wanawake ndani ya Kanisa. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linaendelea kuonesha upendo na kujali familia, ili kweli ziweze kuwa mstari wa mbele katika kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia inayoambata Injili ya uhai.

Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anaendelea kukazia umuhimu wa Mababa wa Sinodi kushirikiana kwa kuaminiana na kuthaminiana, ili kuziwezesha familia kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Ikumbukwe kwamba, Sinodi ni mahali pa kushirikishana na kubadilishana mawazo; ni mahali pa kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Kanisa na wala si jukwaa la kinzani. Majadiliano wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu yanafanyika katika hali ya amani, utulivu na maelewano, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo. Huu ndio wajibu wa Jumuiya ya Kikristo na wala si vinginevyo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.