2015-10-10 14:23:00

Kanisa linasikiliza: Mang'amuzi ya wito wa kifamilia! Umoja, udumifu na uwazi!


Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia mara baada ya kumaliza kutoa muhtasari wa tafakari, mawazo na maoni kutoka katika makundi madogo madogo, wameanza kuangalia sehemu ya pili ya Hati ya kutendea kazi inayojikita juu ya mang’amuzi ya wito wa kifamilia. Mambo makuu yaliyojitokeza katika sehemu hii ni: umoja, kutovunjika na uwazi kwa Injili ya uhai kuwa ni mambo msingi katika maisha ya ndoa na familia. Haya ni mambo ambayo Mababa wa Sinodi wanasema yanapaswa kufafanuliwa kwa kina na mapana ili kuwasaidia waamini kutambua, kuthamini na kushuhudia Injili ya Familia. Mama Kanisa anakumbushwa kwamba, utume wake msingi ni kuwasaidia waamini kumwilisha imani katika uhalisia wa maisha yao.

Mababa wa Sinodi katika tafakari na majadiliano yao, wamegusia kwa kiasi kikubwa muungano uliopo kati ya familia na mchakato wa Uinjilishaji mpya unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ikumbukwe kwamba, kimsingi familia ni kiini cha maisha ya kimissionari na kwamba, watoto ni muhimu sana katika azma ya Uinjilishaji kwani wanaweza pia kusaidia kuamsha imani ya wazazi wao na hivyo kuambata Injili, changamoto kwa wazazi na walezi kuhakikisha kwamba, wanarithisha imani na tunu msingi za maisha ya kiutu kwa watoto wao.

Wazazi wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda wa utakatifu wa maisha unaopata chimbuko lake katika maisha ya kifamilia. Ikumbukwe kwamba, familia ni madhabahu muafaka ya utakatifu wa maisha; chemchemi ya matumaini na kiini cha Uinjilishaji, mahali ambapo cheche za mageuzi ya kijamii zinaweza kupata chimbuko lake, ikiwa kama fadhila ya imani itapewa kipaumbele cha kwanza. Mababa wa Sinodi wamewakumbuka kwa namna ya pekee wanafamilia ambao wanaogelea katika dimbwi kubwa la majanga na madonda. Kanisa linapaswa kuwaangalia wote hawa kwa moyo wa upendo na huruma; kwa uvumilivu katika ukweli, uwazi na ujasiri wa kichungaji. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, pengine hakuna mwanandoa mwenye uelewa wote na wa haki kuhusu Sakramenti ya Ndoa.

Sinodi imekazia umuhimu wa sala katika familia, lakini zaidi ushiriki katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, hasa Ibada ya Misa Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho, ili kuziwezesha familia kuwa kweli ni Kanisa dogo la nyumbani. Mababa wa Sinodi wamewakumbuka na kuwaombea wanafamilia wanaokabiliwa na majanga katika maisha yao kama vile wale wanaoishi katika maeneo ya vita, kinzani na migogoro ya kijamii, maafa asilia na majanga mengine ya maisha yanayowashinikiza kuhama na kukimbia kutoka katika familia na nchi zao.

Mababa wa Sinodi, wakiwa wameungana na Baba Mtakatifu Francisko, wameendelea kukazia umuhimu wa kuunda na kujenga familia kumzunguka Kristo Yesu. Wazazi na walezi watambue dhamana na wajibu wao kwamba, wanashiriki katika kazi ya uumbaji, kumbe wanao wajibu na utume wa kutekeleza mintarafu miongozo inayotolewa na Mama Kanisa. Familia zinachangamotishwa kujenga mahusiano ya karibu zaidi na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Yesu Kristo, kwa kuwa na majiundo makini na endelevu kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa, Amri za Mungu na Maisha ya Sala. Mama Kanisa awasaidie na kuwasindikiza wanandoa wapya katika hija ya maisha yao, ili kupunguza kinzani, kero na mipasuko inayojitokeza katika miaka ya kwanza kwanza ya maisha ya ndoa na familia. Mashuhuda wa ndoa, wawe pia mstari wa mbele kuwasaidia wanandoa watarajiwa kwa njia ya ushuhuda na mifano bora ya kuigwa.

Umoja, kutovunjika na uwazi kwa Injili ya uhai na malezi ni mambo msingi yasiyokuwa na mjadala na kwamba, Kanisa linatumwa kutangaza ukweli huu ambao kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Sakramenti ya Ndoa ni chemchemi ya baraka na muungano thabiti kati ya bwana na bibi, mwaliko kwa wanandoa kuishi kadiri tunu msingi za Kiinjili. Hii ni nguvu mpya wanayopewa wanandoa na kwamba, wanapaswa kuipokea kwa moyo wa shukrani na upendo mkuu, ili kuonesha: ukuu na utakatifu wa maisha ya ndoa. Dhana hii ni kati ya mambo yanayowaogofya waamini kufanya maamuzi magumu katika maisha kwa kuachana na uchumba sugu au ndoa za majaribio.

Wazazi na walezi wanakumbushwa kwamba, wao ni makatekista wa kwanza wanaopaswa kurithisha imani kwa watoto wao, changamoto kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anatekeleza dhamana na wajibu wake, ili wazazi waweze kufanikisha wito na azma hii katika maisha. Familia za Kikristo zijenge mazingira na ari ya kimissionari, kwa kutambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, chemchemi ya imani, matumaini na mapendo na kwamba, wao ni kielelezo cha mahusiano ya Familia ya Mungu. Mababa wa Sinodi wanataka vijana kufanya maamuzi magumu kwa kuambata wito wa ndoa, kwa kuwa waaminifu; tayari kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Familia kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Utume wa familia upewe kipaumbele cha pekee unaombata ushuhuda wa Kanisa, kwa kuwasaidia wanandoa wanaotembea katika shida na magumu ya maisha, kwani kamwe Mwenyezi Mungu hawezi kuwaacha pweke!

Kimsingi Mababa wa Sinodi wanaendelea kukazia: Ushuhuda wa Injili ya Familia, upendo, haki na huruma; upole na ujasiri; Kanisa likiwa mstari wa mbele kutekeleza dhamana na wajibu wake. Kanisa ni familia kubwa ambayo haipaswi kuwanyooshea watoto wake kidole, bali liwe mstari wa mbele kuzima kiu ya wale wanaomtafuta Mwenyezi Mungu kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani, ili kuwaonjesha: upendo, ukweli, msamaha na huruma ya Mungu inayoponya madhaifu na mapungufu ya kibinadamu. Ni neema na baraka inayohitaji toba na wongofu wa ndani.

Mababa wa Sinodi wanakazia pia umuhimu wa kuwafunda watoto katika misingi ya majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kuwajengea dhamiri nyofu zinazojikita katika tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kijami na kitamaduni, tayari kuondokana na hofu na mashaka yasiyokuwa na msingi. Familia ijenge utamaduni wa kusikilizana, kujadiliana na kushirikishana katika masuala mbali mbali, lakini zaidi katika Neno la Mungu, ili kuasha na kukuza imani, mapendo, matumaini na mshikamano wa dhati; tayari kukabiliana na changamoto za maisha!

Mababa wa Sinodi wanawahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika maisha ya hadhara na katika jukwaa la siasa ili kuchangia mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya chachu ya Injili na Mafundisho Jamii ya Kanisa; kwa kuzingatia kanuni auni, mafao ya wengi, haki, amani na mapendo. Viongozi wa Serikali na Kisiasa wasiwe ni chanzo cha kuvunjika kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, bali wawe ni walinzi na watetezi wa kazi ya uumbaji. Mababa wa Sinodi wanaliomba Kanisa kuwa na utume maalum kwa familia za askari ambao daima wanajikuta wako mstari wa mbele. Mara nyingi familia kama hizi zinajikuta zikitumbukia katika hali ya kukata tamaa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.