2015-10-09 09:15:00

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 28 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa!


Ni Dominika nyingine mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, kipindi tafakari Neno la Mungu, tunaposhirikishana upendo usio na mwisho. Neno la Mungu Dominika ya 28 ya mwaka B wa Kanisa latualika kuchagua Hekima ya kimungu, njia ya kurithi uzima wa milele. Katika somo la kwanza toka kitabu cha Hekima tunamwona mfalme Suleimani akiitukuza hekima ya kumjua Mungu ambayo ni mwangaza na njia kamilifu kwa ajili ya kufika mbinguni. Mfalme Suleimani anaona Hekima, kitu cha thamani kubwa na hivi haiwezi kulinganishwa na kitu chochote kiwacho hapa ulimwenguni. Ndiyo kusema, Hekima hiyo ni zawadi ya kumjua Mungu itolewayo na Mungu mwenyewe pasipo madai ya awaye yote.

Hekima ni zawadi, ni tunu bora toka kwa Mungu kwa ajili ya zama zetu hizi na hivi tunapaswa kuipokea na kuichagua kwa unyenyekevu pasipo mashaka. Tunaalikwa kusadiki kina mafumbo yote matakatifu na kwa njia hiyo tutaweza kuuingia mlango wa heri wa Hekima, mlango wa mbinguni. Katika kuchagua Hekima ya kumjua Mungu lazima kila mmoja wetu azame kwa undani kabisa katika Neno la Mungu ambalo ni nguzo mojawapo ya imani yetu. Kwa njia ya Neno la Mungu tutaweza kujua yaliyomo ndani ya imani yetu na kuyaweka katika matendo. Tunasikia katika somo la pili Dominika hii kuwa Neno la Mungu ni kali kuliko upanga wowote ule!

Ni kali kwa sababu ni hai na lina uwezo wa kupenya katika mioyo ya watu. Kumbe mwaliko ni kulisoma ama kulisikia na kulisikiliza na kisha kutafakari. Ndiyo kusema tunaalikwa kila siku walau kujisomea Neno la Mungu na kwa namna hiyo tutakuwa katika mlango wa kukua kihekima na katika tumaini la kweli kwa Mungu. Neno la Mungu lililo msingi wa imani yetu lazima lizame mioyoni na lilete mabadiliko na hivi kuzaa matunda.

Mpendwa msikilizaji, Mwinjili Marko anatupa namna ambavyo tunatakiwa kubadilishwa na Neno la Mungu, ndiyo kusema kuwa tayari kuacha mambo ya zamani ambayo hayaambatani na mapendo ya jirani, kuacha kujifungamanisha na mali na ubinafsi na badala yake tuambatane na ushirika wa kimungu yaani kutumia vipaji na mali zetu kwa sifa na utukufu kwa Mungu na kwa mafaa ya wengine. Anatuasa kuwa makini katika kushika amri za Mungu, yaani si katika kuziorodhesha na pengine kuzikariri bali kuzitumia kama njia na mlango wa mapendo ya Mungu kwa mwanadamu na hivi toka pale kupiga hatua katika kutimiza mapenzi yake. Lazima mmoja wetu afikiri na kujiuliza je mali na vipaji nilivyonavyo vyanipa nafasi ya kumpenda Mungu na kumtumikia na kisha vitaweza kunifikisha mbinguni?

Mpendwa, yafaa kuwa kama mfalme Suleimani ambaye katika kitabu cha kwanza cha Wafalme 3: 4-15 yuko Gibeoni akitolea sadaka na huko anaomba Hekima ya Mungu ili imsaidie kutenda haki na hukumu ya kweli katika kazi yake ya kutawala taifa la Mungu. Ndivyo wewe Kasisi, mchungaji, Baba na Mama katika familia unavyopaswa kusali na kuomba mbele ya Mungu. Yote haya tuyafanye kwa Imani matumaini na mapendo na heri yake ni ya milele.

Ninakualikeni katika wasaa na wakati huu Dominika ijayo tunaposafiri pamoja katika kuendeleza utume wa Neno la Mungu. Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako toka Padre Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.