2015-10-09 15:34:00

Siku ya Afya ya Akili Duniani 2015: Tambua dalili za magonjwa ya akili


Katika maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Duniani, Wizara ya afya na ustawi wa jamii nchini Tanzania imetoa tamko kuhusu maadhimisho haya kwa kubainisha dalili za magonjwa ya akili zinazotokana na: kihisia, kimwili na kiakili pamoja na kubainisha baadhi ya magonjwa ya akili na sababu zake. Mwaliko unatolewa kwa wananchi wote kuhakikisha kwamba, wanapata huduma mapema wanapoona dalili za magonjwa ya akili, ili waweze kuhudumiwa mapema zaidi. Unaweza kujitajirisha zaidi kwa kujisomea tamko hili, kwa faida yako mwenyewe na jamii inayokuzunguka.

Ndugu Wananchi,

Siku ya Afya ya Akili Duniani, huadhimishwa duniani kote kila mwaka tarehe 10 ya Mwezi Oktoba. Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Duniani mwaka 2015 ni “Utu katika Afya ya Akili (Dignity in Mental Health)”. Kaulimbiu hii ambavyo imetolewa na Shirikisho la Afya ya Akili Duniani (World Federation of Mental Health) inalenga kuhamasisha jamii juu ya matatizo mbalimbali ya afya ya akili yanayoikabili jamii hususan kutokuthaminiwa kwa utu wao. Hii ni kutokana na ukweli kwamba maelfu ya wagonjwa wa akili Duniani kote wanakosa haki zao kama binadamu. Pia wagonjwa wa akili si kwamba wanatengwa,wanabaguliwa na kunyanyapaliwa tu, bali pia ni waathirika wakubwa wa unyanyasaji wa kihisia (emotional abuse) pamoja na unyanyasaji wa kimwili (physical abuse) katika jamii na katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Lengo kuu la kauli mbiu ya mwaka huu ni kutoa elimu kwa jamii ili waelewe kuwa wagonjwa wa akili wanaweza kuishi maisha yao na kuthaminiwa utu wao kwa kuzingatia sheria za haki za binadamu (Human Right Orientation Policy and Law). Hivyo basi, Tanzania kama ilivyo nchi zingine duniani kote itaadhimisha siku hii ambapo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii (WAUJ) kwa kushirikiana na Chama cha Wataalamu wa Afya ya Akili Tanzania (MEHATA) itaadhimisha siku hii kwa kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kuzingatia utu wa mgonjwa wa akili pale anapokwenda kupata huduma za matibabu katika vituo vya kutolea huduma.

Ndugu Wananachi,

Tunapozungumzia afya tunamaanisha hali ya ustawi wa mwanadamu kimwili, kiakili na kijamii. Mtu mwenye afya njema ya akili anaaminika kutengemaa katika namna anavyofikiri, anavyohisi, na anavyotambua mambo, ambayo kwa pamoja hujionyesha katika matendo yake ya kila siku.

Magonjwa ya akili ni magonjwa ambayo yanaathiri uwezo wa mtu kufikiri, kuhisi, kutambua na kutenda, na hivyo kuwa na tabia au mwenendo uliotofauti au usioendana na jamii husika kiimani, kimila, desturi, na nyanja nyingine za kijamii. Tabia hizo zinatokana na ugonjwa wa akili kuathiri ufanisi na shughuli za mtu husika (mgonjwa) au huathiri jamii nzima inayomzunguka endapo mgonjwa huyo hatopatiwa matibabu stahiki na kwa wakati muafaka. Hapa nchini kwetu wagonjwa wengi wa akili hawafiki katika vituo vya kutolea huduma za afya na badala yake kuishia kwenye tiba za jadi au kutelekezwa na kunyanyapaliwa.

Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania ina idadi ya watu takriban milioni 45 na kutokana na taarifa ya afya ya akili kwa mwaka 2014/15 inaonyesha kuwa idadi ya watu 817,532 wanaugua magonjwa mbalimbali ya akili nchini, hii ni karibu asilimia 2 ya watanzania wote. Pia idadi hii ni ongezeko la wagonjwa 367,532 ukilinganisha na takwimu za mwaka 2013/14 walikuwa ni 450,000. Kati ya wagonjwa wote wa akili kwa mwaka 2014/15 wanawake ni ni 332,000 na wanaume ni 485,532. Mkoa wa Dar-Es-Salaam unaongoza kwa kuwa n awagonjwa wengi nchini ukifuatiwa n amkoa wa Dodoma na mkoa wa mwisho ni Lindi. Idadi hiyo ya wagonjwa ni wale walioweza kuhudhuria katika vituo vya kutolea huduma ya afya hapa nchini.

Ndugu Wananchi,

Magonjwa ya akili yapo ya aina nyingi na mengi huwa hayatambuliki kwa urahisi kwa jamii na hata kwa watoa huduma wa afya na hivyo wagonjwa wengi huchelewa kupata matibabu stahiki. Aidha wagonjwa wa akili wamekuwa wakibaguliwa na kunyanyaswa na jamii kutokana na imani potofu katika jamii yetu kuhusiana na sababu zinazo sababisha magonjwa ya akili pamoja na kutofahamu kuhusu matibabu ya magonjwa ya akili.

Dalili zinazoashiria magonjwa ya akili ni nyingi sana, baadhi tu ni ambazo zimegawanyika katika makundi matatu ni kama ifuatavyo:

i) Kihisia

· Kukosa furaha na kuhuzunika sana

· Kuwa na furaha sana kupita kiasi

· Wasiwasi na/ au woga kupita kiasi

· Kupunguza kuongea au kutokuongea kabisa au kuongea sana kupita kiasi

· Hasira za haraka haraka hata kufikia kupiga wengine

· Kuwa na msongo wa mawazo

· Kujitenga na watu na kupenda kukaa mwenyewe muda mwingi au kupenda kuwa na watu sana kuliko kawaida

· Kutokuwa na ari ya kufanya kazi au kufanya kazi nyingi kwa wakati mmoja bila ya kuzikamilisha

· Kutokuonyesha hisia yoyote usoni mwake (mf. furaha au huzuni nk)

· Kutokujijali usafi na muonekano wake

· Kuhisi maisha hayana thamani na kuona bora kufa kuliko kuishi na hatimaye kufikia uamuzi wa kujiua na hata kuua wengine.

ii) Kimwili

· Mwili kukosa nguvu au kuhisi mwili una nguvu sana kupita kiasi

· Kukosa usingizi au kulala usingizi sana kupita kiasi

· Kukosa hamu ya kula au kuwa na hamu sana ya kula

· Kutokutulia (kuhamanika) au kutulia sehemu moja muda mrefu bila ya kujisogeza

· Maumivu sehemu mbalimbali za mwili kama vile kichwa, mabega, mgongo, na viungo mbalimbali ambavyo akienda hospitali vipimo havionyeshi tatizo lolote la kimwili.

iii) Kiakili

· Kukosa umakini wa shughuli zake za kila siku

· Kusahau kwa haraka au kupoteza kumbukumbu

· Kukosa uwezo wa kupambanua mambo kwa mitazamo tofauti

· Kusikia sauti ambazo hazipo na kuona vitu ambavyo havipo

· Imani ya ajabu ambazo haziendani na mila, imani au desturi za jamii yake ; kama vile yeye ni mtu maarufu, au anaamini kuwa yeye ni Nabii

au anaamini kupokea taarifa kutoka kwenye redio au mitandao ya simu

· Pia anaamini ana nguvu ya ziada kutoka nje ya mwili yake inayomsababishia kutenda au kuwaza mambo anayoyawaza

· Anaamini mawazo yake yanapunguzwa au kuongezwa na watu wasiojulikana, vyombo vya habari kama vile Radio na TV kuwa vinazungumzia yeye, au vinaongea mawazo yake yeye

· Mawazo yake hayana mtiririko unaoeleweka.

Ndugu Wananchi,

Baadhi ya aina za magonjwa ya akili ni kama vile magonjwa ya kuchanganyikiwa (Psychoses), magonjwa yanayohusiana na matumizi mabaya ya pombe na uraibu wa madawa ya kulevya magonjwa yanayohusiana na matumizi ya pombe, uraibu wa madawa ya kulevya (addiction of alchohol and drugs), aidha Magonjwa ya wasiwasi au hofu/woga (anxiety/Phobia), magonjwa yanayoathiri hisia (mood disorders) ambayo hupelekea watu kujiua pamoja na matatizo ya jinsia (sexual dysfuctions). Magonjwa haya mara nyingi yanapoanza yanaonekana ni hali ya kawaida tu na huenda pasiwepo na jitihada yoyote ya kupata msaada wa kitabibu hadi hali itakapokuwa mbaya au kuzidiwa. Pia watoto nao huwa wanaugua magonjwa ya akili ambayo kama yasipotambuliwa na kupatiwa matibabu mapema huathiri ukuaji wao pamoja na uwezo wao wa kupata elimu.

Ndugu Wananchi,

Vipo visababishi vingi ambavyo husababbisha matatizo ya afya ya akili, sababu hizi ni za kijamii na kisaikolojia kam avile umaskini uliokithiri, kutengwa na jamii, kuwa tegemezi, upweke na upotevu wa vitu mbalimbali (mfano kufiwa na mtu wa karibu, kupoteza mbali, kupoteza kazi au kupata mlemavu), mafarakano katika jamii pamoja na matatizo ya mahusiano, kikosa huduma muhimu, unyanyapao , unyanyasaji naubaguzi wa aina mbalimbali.

Aidha kuna sababu nyingine za kibaiolojia kama vile motto kupata shida wakati wa kuzaliwa na kusababisha mgandamizo wa ubongo, uchungu wa muda mrefu na motto kukosa hewa ya ojsijeni, maradhi kwamama mjamzito ambayo hushambulia mfumo wa fahamu wa mtoto aliye tumboni na pia kama wazazi wana vinasaba vya ugonjwa wa akili mtoto/watoto pia wanaweza kurithi.

Serikali imeendelea na utekelezaji wa Sera ya Afya ya Mwaka 2007 ambayo inalenga kutoa huduma bila malipo kwa wagonjwa wa akili, aidha sera ya mwongozo wa huduma za Afya ya Akili inasisitiza utoaji wa huduma ya Afya ya Akili bila ya malipo. Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeendelea kutambua uwepo wa maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Duniani kama sehemu ya uhamasishaji wa jamii kuhusu magonjwa ya akili, kama ilivyo kwenye nchi zingine duniani.

Ndugu Wananchi,

Wagonjwa wa akili wanahitaji uangalizi na matunzo maalum ya kitaalam; pamoja na ukweli huo, huduma ya afya ya akili hazipatikani kwa urahisi katika vituo vya afya na zahanati nchini. Ili kuboresha huduma hizo na haswa katika kutoa huduma za matibabu kwa kuzingatia utu wa wagonjwa wa akili, serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imehakikisha kwamba:-

(i) Watumishi wa afya wanapewa mafunzo maalum ya namna ya kuwahudumia wagonjwa wa akili, hii ikiwa ni p amoja ma kuheshimu utu wa wagonjwa, kuwaelimisha wagonjwa pamoja na ndugu zaokuhusu magonjwa ya akili na matibabu yake pamoja na kuwashirikisha katika maamuzi ya matibabu na kupata ridhaa kutoka kwao.

(ii) Serikali itahakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba mbalimbali vinavyotumika katika matibabu ya magonjwa mbalimbali ya akili hii ikiwa ni pamoja upatikanaji wamashine ya ECT (Electroconvulsive Therapy) katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

(iii) Serikali inaendelea kufanya jitihada za kuwasomesha wataalam wa afya na magonjwa ya akili nchini ili kuweza kupata wataalamu wengi watakaoweza kutoa huduma bora mijini na vijijini. Lengo ikiwa ni kuhakikisha kwamba angalau kila hospitali ya mkoa iwe na daktari bingwa wa afya na magonjwa ya akili.

(iv) Kuweka utaratibu wa kufuatilia afya za wagonjwa wa akili katika jamii (outreach services).

(v) Aidha serikali itaendelea kuimarisha vituo vyake vya afya ya msingi na utengamao wa akili nchini kote. (Primary health care and Rehabilitation centers).

(vi) Kufanya tafiti mbalimbali zinazosaidia kuboresha huduma za kuzuia na kudhibiti magonjwa ya akili katika jamii kwa watoto, vijana na watu wazima.

Ndugu Wananchi,

Natoa wito kuwa ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa anatoa msaada wa kutosha kwa wagonjwa wa akili, ikiwa ni pamoja na kupunguza unyanyasaji na ubaguzi. Kwa kuwamagonjwa mengi ya akili yanaweza yasionyeshe dalili yoyote bayana, ni vema kila mmoja wenu akapata fursa ya kutembelea kituo cha afya mara kwa mara ili kutambua hali yake ya afya ya akili. Endapo utatambuliwa kuwa una ugonjwa wowote wa tumia huduma za afya kulingana na ushauri utakaopewa na wataalam wa afya ya akili. Kwa wale ambao wameshajitambua kuwa na matatizo ya afya ya Akili lakini hawatumii huduma za afya ipasavyo, nawaasa watumie huduma za afya zilizopo kwa manufaa ya afya zao na kuepusha athari zinazotokana na magonjwa ya akili endapo atachelewa kupata matibabu au kama hatapata matibabu kabisa.

MICHAEL O. JOHN

KAIMU KATIBU MKUU

09/10/2015








All the contents on this site are copyrighted ©.