2015-10-09 14:26:00

Papa Francisko anaungana na Mababa wa Sinodi kuombea amani duniani!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia yanayoendelea hapa mjini Vatican, Ijumaa  tarehe 9 Oktoba 2015 amewaomba Mababa wa Sinodi kuungana pamoja naye kwa ajili ya kuombea amani huko Mashariki ya Kati ya katika baadhi ya Nchi za Kiafrika ambazo bado mtutu wa bunduki unarindima na hivyo kusababisha majanga makubwa kwa familia ya binadamu.

Baba Mtakatifu ameonesha mshikamano wake wa dhati na maaskofu wanaotoka katika maeneo yaliyoathirika kwa vita na kinzani za kijamii. Baba Mtakatifu anaiomba tena, Jumuiya ya Kimataifa kuongeza juhudi za kidiplomasia ili amani ya kweli iweze kupatikana na watu waweze kusonga mbele katika maisha yao. Mashariki ya kati kwa sasa inaendelea kuwaka moto na kwamba, mauaji ya watu wasiokuwa na hatia yamekuwa ni sehemu ya habari zinazochukua uzito wa juu katika vyombo vya mawasiliano ya kijamii.

Baba Mtakatifu amewaomba Mababa wa Sinodi, mkusanyiko mkubwa ambao anashiriki kwa kusikiliza kwa makini mchango unaotolewa na Mababa wa Sinodi. Akizungumza na Mababa hawa wakati wa sala ya Kanisa, Baba Mtakatifu amewaomba Mababa wa Sinodi kuendelea kusali kwa ajili ya upatikanaji wa haki, amani na upatanisho wa kweli huko Mashariki ya Kati, yaani: Syria, Iraq na Yerusalem na Yordani. Kuna watu wasiokuwa na hatia wanaoendelea kupoteza maisha yao kutokana na vita na vitendo vya kigaidi hali inayosababisha pia mateso na mahangaiko makubwa na kwamba, matumaini ya wananchi wengi yanajikita katika suluhu ya amani kwa njia ya majadiliano.

Mababa wa Sinodi wanaotoka sehemu mbali mbali za dunia ni kielelezo cha Kanisa la Kiulimwengu, linaloongozwa na kusimamiwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, juhudi na majadiliano yanayojikita katika misingi ya haki, amani na ukweli na kufumbatwa katika diplomasia zitaweza kuzimisha moto wa mapambano. Ni jukumu na wajibu wa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuwajibika barabara katika maamuzi yao, ili kweli amani iweze kupatikana.

Baba Mtakatifu anaungana na Mababa wa Sinodi kuiomba Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi badala ya kujikita katika mafao ya nchi binafsi; haki ya kimataifa na diplomasia viwe ni nyenzo msingi katika kutafuta suluhu ya amani kwenye maeneo yanayoteseka kutokana na vita pamoja na kinzani za kijamii. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Bara la Afrika linakabiliwa na changamoto na majanga makubwa anamwomba Bikira Maria, Malkia wa amani kuwambea watoto wake wanaoteseka kutokana na vita.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.