2015-10-09 09:36:00

Msumbiji jikiteni katika misingi ya haki na amani kwa njia ya majadiliano!


Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania, amewaasa wabunge wa Bunge la Msumbiji kufanya mazungumzo ili kumaliza tofauti zao. Rais Kikwete ametoa ushauri huo tarehe 8 Oktoba wakati wa mazungumzo na Spika wa Bunge la Msumbiji Bibi Veronica Macamo ofisini kwake. "Fanyeni mazungumzo, haiwezekani mkarudia vita tena baada ya miaka 22 , hatutapenda mrudi kwenye uwanja wa vita, hivyo ni muhimu mkafanya mazungumzo" Rais amewaasa wabunge katika kikao chake na Spika. 

"Nyinyi wabunge lazima mtambue nafasi zenu na wajibu wenu wa kutokurudia vita tena, nyinyi ni wawakilishi wa watu na watu wanahitaji maendeleo sio vita" Rais Kikwete ameelezea. Rais Kikwete amewaasa wabunge wasikubali nchi yao kuingia katika vita na badala yake wakae pamoja na kuweka makubaliano ambayo yatakubalika kwa vyama vyote na hatimaye kuwaepushia wananchi wa Msumbiji kuingia kwenye vita kwa mara nyingine.

Kikao cha Rais na Spika Macao ambaye anatoka Chama Tawala cha Ukombozi wa Msumbiji, The Mozambique Liberation Front (FRELIMO) pia kimehudhuriwa na wabunge wa vyama vya Mozambique Democratic Movement (MDM) na Mozambican National Resistance (RENAMO)ambavyo vinaunda Bunge la Msumbiji. Rais Kikwete yupo nchini Msumbiji kwa ziara ya Kiserikali ya siku 2 kufuatia mualiko kutoka kwa Rais Filipe Jacinto Nyusi.

Mara baada ya kuwasili Maputo, Rais Kikwete amefanya mazungumzo na mwenyeji wake ambapo Rais Nyusi amemshukuru Rais Kikwete kwa msaada wake na kumueleza kuwa Msumbiji inathamini sana uhusiano baina ya nchi mbili hizi na kueleza nia yake ya kukuza uhusiano huu katika nyanja za kibiashara na katika kupambana na maovu mbalimbali baina ya nchi hizi.

Baadaye Rais Kikwete alipata heshima ya kupewa Ufunguo wa mji wa Maputo na kutangazwa Rais wa jiji hilo na Meya wa Maputo Ndugu David Simango. "Una haki zote za raia wa Maputo, una haki ya kuingia wakati wowote, nakutakia kujisikia upo nyumbani ambapo siku zote utapendwa na kukaribishwa." Amesema Meya Simango mara baada ya kumkabidhi Rais Kikwete Ufunguo huo. Ufunguo wa Mji wa Maputo ndiyo, heshima ya juu zaidi katika jiji la Maputo.

Rais pia ametembelea na kufanya mazungumzo kwenye ofisi za Chama Tawala cha FRELIMO na kuongea na wanachama wake, Alhamisi usiku, Rais Nyusi alimuandalia Rais Kikwete na Ujumbe wake chakula cha jioni kwa Heshima ya Rais Kikwete ambaye pia katika mazungumzo yao, Rais Kikwete ameaga na kueleza kuwa Tanzania inatarajia kupata kiongozi mwingine baada ya uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba ,2015 lakini mahusiano na sera za nchi kwa Taifa la Msumbiji utaendelea na hatimaye kuimarika zaidi.

Ijumaa asubuhi  Rais Kikwete anatarajia kuelekea mji wa Pemba, katika jimbo la Cabo Delgado ambapo anatarajia kufanya mkutano wa hadhara na baadae kukutana na Watanzania wanaoishi katika jimbo hilo kabla ya kuelekea Mkoani Mtwara kuendelea na shughuli za kitaifa.

Na mwandishi maalum.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.