2015-10-09 07:09:00

Hii ni Sinodi ya Familia ya Mungu!


Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia wanaoendelea na tafakari zao hapa mjini Vatican, Alhamisi tarehe 8 Oktoba 2015 wamehitimisha tafakari zilizokuwa zinafanywa kwenye makundi madogo madogo “Circoli minori”, kielelezo cha umoja, mshikamano na utofauti unoambata utajiri wa maisha na utume wa Kanisa la kiulimwengu. Ijumaa asubuhi, Mababa wa Sinodi wamesikiliza kwa kina na mapana sehemu ya kwanza ya hati ya kutendea kazi “Instrumentum Laboris”.

Ni sehemu inayojadili kwa mapana changamoto ambazo familia ya binadamu inakabiliana nazo katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko daima anawataka Mababa wa Sinodi kujengeana imani na matumaini kati yao na kamwe wasiwe ni watu wa kukata tamaa kutokana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika maisha na utume wa ndoa na familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo.

Mababa wengi wa Sinodi wanakiri kwamba, maadhimisho ya Sinodi kwa mwaka huu, yanaonesha kwa namna ya pekee imani, matumaini na mapendo ya watu wa Mungu kwa Kanisa. Kimsingi hii ni Sinodi ya Watu wa Mungu anakaza kusema Kardinali Edoardo Menichelli, mratibu wa moja ya vikundi vya lugha ya Kiitalia. Maadhimisho haya ni matunda ya safari ya Familia ya Mungu katika kipindi cha miaka miwili, hali ambayo imetoa fursa kwa Mama Kanisa kupembua kwa kina na mapana yale yaliyojadiliwa, tayari kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya familia ya binadamu mintarafu mpango wa Mungu kwa binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.