2015-10-08 15:24:00

Tanzania inayo mengi ya kujivunia katika kipindi cha miaka 50 iliyopita!


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Mhe. Mizengo Pinda amewaonya Watanzania wanaobeza juhudi za kuleta maendeleo zilizofanywa na Serikali tangu wakati wa uhuru. Ametoa kauli hiyo Jumatano, Oktoba 7, 2015 wakati akizungumza na wakazi wa Usevya na vijiji vya jirani kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Usevya, wilaya ya Mlele, mkoa wa Katavi.

Alisema ukubwa wa nchi ya Rwanda ni kilometa za mraba 27,000 wakati ukubwa wa Tanzania ni km za mraba 945,000 ambayo ni kubwa mara 35 zaidi ya Rwanda. “Ukubwa wa Rwanda ni sawa na wilaya moja tu ya Mlele ambayo ina ukubwa wa kilometa zaidi ya 29,000. Hivi tuna wilaya ngapi hapa nchini ambazo ni kubwa kuliko Rwanda?, alihoji. “Acheni tabia ya kulinganisha vinchi vidogo na Tanzania… kazi ya kuleta maendeleo siyo ndogo. Tunamhitaji Dk. Magufuli ili aweze kuleta maendeleo kwa kasi hapa nchini kwa sababu yeye ni mchapakazi na kila mmoja wetu anatambua hilo, hataki mchezo na kazi na hata wapinzani wanalitambua hilo,” alisema.

Alisema ameshangaa kusikia watu wakijitapa kuwa watendesha nchi kwa kasi ya ajabu na kwamba ndani ya siku 100 watamaliza shida zote na kuondoa umaskini miongoni mwa Watanzania. “Kazi ya kuongoza nchi inataka umakini, uzoefu na watu waliobobea kwenye uongozi. Hii si kazi ya majaribio hata kidogo… eleweni kuwa changamoto ni sehemu ya maendeleo. Tuaminini CCM na tupeni nafasi tufanye kazi kwa kumpa kura zote Dk. Magufuli, mbunge wa CCM na madiwani wa CCM,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Katavi, Dk. Ibrahim Msengi amewataka wakazi wa mkoa huo wasiwe na hofu na wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura. “Wote watakaoleta vurugu na kuwazuia wenzao wasipige kura tutawadhibiti sababu tuna nia ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Wakati huo huo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Mhe. Mizengo Pinda amepokea kadi tisa kati ya 205 zilizorejeshwa na wanachama wa CHADEMA katika kata ya Mamba, wilaya ya Mlele kwenye jimbo la uchaguzi la Kavuu na kuwapongeza wanachama hawa kwa maamuzi yao ya busara. Ametoa kauli hiyo Jumatano, Oktoba 7, 2015) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa jimbo la Kavuu kwenye mikutano mitatu ya hadhara iliyofanyika katika kata za Mamba, Mwamapuli na Usevya.

Mhe. Pinda alikuwa mbunge kwenye jimbo hilo ambalo limegawanywa na kupata majimbo matatu ya Nsimbo, Katavi na Kavuu. Wakati huo lilikuwa likijulikana kama Jimbo moja la Katavi. Alisema katika kipindi hiki cha kampeni, uongozi wa wilaya umepokea wanachama 126 kutoka kata ya Chamalendi, 15 kutoka Kasansa ambao wanane kati yao ni wenyeviti wa vitongoji, tisa kutoka Mamba na 62 kutoka Majimoto. Wanahama hao wametoka vyama vya CHADEMA na ADT WAZALENDO.

Alisema anastaafu akiwa na amani moyoni mwake kutokana na juhudi ambazo Serikali ya awamu ya nne imezifanya kwenye mkoa wa Katavi. “Niliamua kuacha kugombea ubunge kwa sababu ninatambua kuwa kuna watu wengine wenye uwezo wa kuongoza,” alisema. “Ninaondoka nikiwa nimefarijika kwa sababu Serikali imetupatia mkoa mpya wa Katavi, tumepata wilaya tatu, halmashauri tatno na majimbo matano ya uchaguzi. Hii itawapa fursa ya kupanga mipango yenu kupitia madiwani wenu tofauti na zamani tulipokuwa tukisubiri kila kitu kitoke Rukwa,” alisema.

Akizungumzia mafanikio ya serikali ya awamu ya nne, Mhe. Pinda alisema Serikali ya CCM imekamilisha suala la mawasiliano ya simu na sasa hivi inakamilisha suala la umeme ambao alisema hivi punde utaanza kupatikana kwenye bonde la Rukwa. “Mwanzoni tulitaka umeme utoke Chala hadi huku bondeni lakini kitaalamu ikabainika kwamba kadri unavyosafirishwa ndivyo unavyozidi kupungua nguvu. Kwa hiyo. Wataalamu wameamua kuchukua umeme kutoka Muze kuja Kasansa hadi Majimoto,” alisema huku akishangiliwa.

Alitumia fursa hiyo kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe Magufuli pamoja na mgombea ubunge wa jimbo la Kavuu, Dk. Pudensiana Kikwembe. Pia aliwanadi wagombea udiwani wa kata tisa za jimbo hilo wakiwemo madiwani wa kata za Mamba, Majimoto, Mwamapuli, Ikuba, Mbede, na Kibaoni ambao walihudhuria mikutano hiyo.

Na Irene K. Bwire.








All the contents on this site are copyrighted ©.