2015-10-08 07:50:00

Sinodi ya Familia: Lengo ni kutafuta na kuambata ukweli!


Mababa wa Sinodi ya maaskofu kwa ajili ya familia inayoongozwa na kauli mbiu wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo wanaendelea na vikao vyao katika makundi madogo madogo yanayoonesha umoja unaofumbatwa katika lugha na utofauti unaotokana na mahali,  mang’amuzi na uzoefu wa Mababa wa Sinodi. Wote wanafanya kazi kwa pamoja kama familia ya Mungu inayowajibika. Hii ni fursa kwa Mababa wa Sinodi kuvuka mipaka ya tofauti zao, tayari kuzama katika kutafuta ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya binadamu katika ujumla wake. Kanisa Katoliki linakazia pamoja na mambo mengine, umoja na mshikamano wa dhati licha ya tofauti mbali mbali zinazoweza kujitokeza ndani ya Kanisa.

Kimsingi, huu ndio ushuhuda uliotolewa na Askofu mkuu Laurent Ulrich wa Jimbo Katoliki Lille, Ufaransa, Jumatano, tarehe 7 Oktoba 2015, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mambo msingi yanayoendelea kujadiliwa na Mababa wa Sinodi. Tukio hili limeratibiwa na Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican.

Kwa upande wake Askofu mkuu Pineiro Garcia Calderòn wa Jimbo kuu la Salvador, nchini El Salvador anakaza kusema, Kanisa halina budi kuwasindikiza wanafamilia. Ni jukumu na wajibu wa familia zenyewe kuonesha ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa kujenga na kuimarisha: umoja, udugu na mshikamano. Wawe imara kupinga sheria za utoaji mimba, tayari kukumbatia Injili ya Familia inayojikita katika Injili ya Uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Sheria za utoaji mimba na kifo laini ni kashfa na nyanyaso kubwa kwa tunu msingi za maisha ya kifamilia. Wanandoa wasimame kidete kushuhudia na kutangaza Injili ya Familia, Injili ya Uhai, Injili ya Matumaini na Mapendo. Wanandoa waliojeruhiwa wasindikizwe kwa faraja inayoambata huruma ya Mungu.

Askofu mkuu Charles Joseph Chaput wa Jimbo kuu la Philadelhia, Marekani ambaye hivi karibuni alikuwa ni mwenyeji wa maadhimisho ya Siku ya nane ya Familia Kimataifa iliyofanyika nchini Marekani na kuhudhuriwa na Baba Mtakatifu Francisko, amegusia utakatifu wa maisha ya familia ulioshuhudiwa na kuoneshwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya kimataifa ya familia huko Philadelphia. Ni tukio ambalo limetoa changamoto ya kurejesha tena matumaini katika maisha ya kifamilia pamoja na kukazia mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu Sakramenti ya Ndoa. Kanisa liwasaidie wanafamilia ili kamwe wasijisikie kwamba, wamesahaulika katika maisha na utume wa Kanisa.

Askofu mkuu Chaput anawataka Mababa wa Sinodi kuwa na mwelekeo mpana zaidi kwa kuangalia ustawi na maendeleo ya familia ya mwanadamu badala ya kumezwa na magumu pamoja na changamoto zinazojitokeza katika baadhi ya nchi. Kumbe, Mababa wa Sinodi kwa wakati huu katika majadiliano ya vikundi wanaangalia changamoto za Kanisa zima, kwa kujikita katika majadiliano kati ya Kanisa la kiulimwengu na Makanisa mahalia kama inavyobainishwa katika Hati ya kutendea kazi: Instrumentum Laboris. Si haki kwamba, Mabaraza ya Maaskofu Katoliki yakajiamria yenyewe kuhusu Mafundisho tanzu ya Kanisa. Mababa wa Sinodi wapo si kwa ajili ya kutafuta ushindi bali kutafuta na kuendelea kushuhudia ukweli mfunuliwa kadiri ya mapenzi ya Kristo Yesu kwa Kanisa lake.

Askofu mkuu Chaput anawataka pia Mababa wa Sinodi kuwa makini la lugha inayotumika ili wasiwe ni kikwazo na hivyo kusababisha majeraha kwa baadhi ya waamini. Kanisa linataka kuionjesha Familia ya Mungu upendo na mshikamano, kwa kuzihudumia familia: kiroho na kimwili.

Padre Lombardi akijibu maswali kutoka kwa baadhi ya waandishi wa habari kuhusiana na mawazo ya baadhi ya Mababa wa Sinodi yanayopatikana kwenye mitandao anasema kwamba, wako huru kushirikisha waamini wao mchango wao, lakini kwa kuzingatia pia kanuni, sheria na maadili ya maadhimisho ya Sinodi. Hadi sasa kuna makundi madogo madogo 13 yaliyogawanyika kadiri ya lugha wanazotumia Mababa wa Sinodi. Makundi manne ni kwa ajili ya wale “wanaochonga Kimombo”: matatu lugha ya Kifaransa na Kiitalia; mawili kwa ajili ya Kihispania na kundi moja kwa wale wanaozungumza Kijerumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.