2015-10-08 09:02:00

Majadiliano katika makundi madogo madogo ni kielelezo cha umoja katika utofauti


Askofu Bruno Forte, Katibu mahususi wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia  katika mahojiano maalum na Radio Vatican anakaza kusema, maadhimisho ya Sinodi kwa mwaka huu 2015 yanatoa nafasi ya pekee kwa Mababa wa Sinodi kutafakari na kujadiliana katika makundi madogo madogo kielelezo cha mshikamano wa Kikanisa. Hapa ni mahali ambapo Mababa wa Sinodi wanapata nafasi ya kufanya upembuzi yakinifu kwa kufafanua mawazo kadhaa yanayotolewa kwenye maadhimisho haya.

Haya ni makundi ambayo yamegawanyika katika lugha kuu tano zinazotumiwa na Mababa wa Sinodi na hivyo wanaunda makundi ya kazi ambayo kwa mwaka 2015 ni kumi na matatu. Lengo ni kuwawezesha Mababa wa Sinodi kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi. Mambo yanayojadiliwa katika makundi haya madogo madogo ni yale yaliyobainishwa kwenye hati ya kutendea kazi, tayari Mababa wa Sinodi kutembea kwa pamoja, kama neno Sinodi linavyo maanisha. Mababa wa Sinodi wanashirikiana  na wataalam na mabingwa katika nyanja mbali mbali ili kupata ufafanuzi wa kina.

Makundi madogo madogo ni kielelezo cha demokrasia anasema Askofu Bruno Forte, kwani hapa kuna mratibu na katibu anayeandika muhtasari wa mawazo makuu yaliyojitokeza miongoni mwa Mababa wa Sinodi  na hatimaye, kufikishwa mbele ya mkutano unaowajumuisha Mababa wote wa Sinodi. Kimsingi, kutafanyika mikutano kumi na minane ya Mababa wa Sinodi kielelezo cha mshikamano wa Kanisa unaodhihirishwa na Maaskofu. Kila mtu anaweza kuchangia kadiri Roho wa Mungu anavyomjalia.

Utaratibu wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa mwaka huu, umetoa nafasi kubwa zaidi kwa Mababa wa Sinodi kutafakari na kujadiliana katika makundi madogo madogo yanayojulikana kama “Circoli minori”. Askofu Bruno Forte anawasihi Mababa wa Sinodi kujadiliana kwa kina katika uhuru, ukweli na uwazi, ili kuchangia katika uwajibikaji mpana katika masuala ya imani na kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa. Maadhimisho ya Sinodi ya familia yamewashirikisha kwa namna ya pekee kabisa Makanisa mahalia, kwa kusali, kutafakari sanjari na kujibu maswali dodoso yaliyotolewa na Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu.

Hiki ni kielelezo makini cha umoja na mshikamano ndani ya Kanisa unaojionesha pia hata katika utofauti, lengo ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu. Itakumbukwa kwamba, maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu ni matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.