2015-10-07 09:09:00

Papa Francisko anatarajiwa kutembelea Mexico 2016 ili kuwasha moto wa Injili!


Wakati huu Baba Mtakatifu Francisko anapojiandaa kufanya hija ya kichungaji Barani Afrika kwa kutembelea Kenya, Uganda na panapo majaliwa Jamhuri ya Watu wa kati ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican amethibitisha kwamba, panapo majaliwa, mwaka 2016, Baba Mtakatifu atatembelea nchini Mexico. Kwa muda mrefu Baba Mtakatifu ameonesha nia ya kutaka kutembelea Mexico na kwamba, nia hii kwa sasa inafanyiwa kazi, ili iweze kutekelezwa kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Padre Lombardi amethibitisha haya wakati alipokuwa anahojiwa na mwandishi wa habari kutoka Kituo cha Televisheni cha Noticiero Televisiva cha Mexico na kwamba, habari zaidi zinatarajiwa  kutolewa mwezi Novemba, 2015. Akizungumza na waandishi wa habari wakati akirejea kutoka Cuba na Marekani, Baba Mtakatifu alisema kwamba, mpango wake wa awali ulikuwa ni kutembelea Mexico na Marekani, lakini baada ya Marekani na Cuba kurejesha uhusiano wa kidiplomasia, ikawa ni fursa nzuri ya kwenda kuwaimarisha ndugu zake katika imani kwa kujika katika ujenzi wa madaraja yanayowaunganisha watu sanjari na kukoleza ari na moyo wa kimissionari.   Akitembelea Mexico, hapana shaka kwamba, Baba Mtakatifu atakwenda kutoa heshima zake za dhati kwa Bikira Maria wa Guadalupe! Vuteni subira mambo mazuri yanakuja! Wanasema Waswahili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.