2015-10-07 07:28:00

Jukwaa la Wakristo Tanzania: Haki na uhuru ni msingi wa amani ya kweli!


Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) limetoa tamko linalotoa dira kuelekea Uchaguzi Mkuu huku masuala ya Haki, Uhuru na Amani yakitajwa kuwa ni msingi katika kuijenga Tanzania mpya. Tamko hilo limetolewa hivi karibuni mara baada ya kikao cha wajumbe wa Jukwaa hilo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa AMECEA, uliopo Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Jijini Dar es Salaam, huku mapendekezo na tahadhari katika kueleka Uchaguzi Mkuu nchini na baada ya uchaguzi huo vikitolewa.

Tamko hilo limejadili mambo ya msingi ambayo Taifa linapaswa kuyapa kipaumbele hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu na hata baada ya uchaguzi huo, huku masuala ya haki, uhuru na amani yakitajwa kuwa kiini cha kuijenga Tanzania mpya kwa kuzingatia kuwa pasipo haki na uhuru wa kweli amani haiwezi kupatikana. Aidha tamko hilo limebainisha kuwa, ukiukwaji wa haki hupelekea kuwanyima watu uhuru wao hali inayoweza kusababisha machafuko hasa pale wananchi wanapolazimika kudai haki yao kwa nguvu.

Pia tahadhari imetolewa kwa vyombo vya ulinzi na usalama hususan Jeshi la Polisi kutimiza majukumu yake bila upendeleo, ili kuepusha matumizi ya nguvu yanayopelekea uvunjifu wa amani kwa wananchi. Pia tamko limekemea vitisho, umwagaji wa damu na upendeleo wa vyombo vya dola unaoweza kuhatarisha amani katika kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Nayo Tume ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC) imetakiwa isimamie haki bila kuegemea upande wowote wa vyama vya siasa ili kuepusha malalamiko ya mara kwa mara yanayojitokeza wakati wa chaguzi mbalimbali na kupelekea uvunjifu wa utulivu, amani na kutotoa haki kwa pande zote zinazoshiriki uchaguzi.

Jukwaa hilo limeitaka Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) lisimamie vyombo vya habari hasa vinavyokiuka kanuni na maadili ya uandishi na kuchochea vurugu huku vyombo vya habari vikitakiwa kuwa makini katika kutoa habari katika Uchaguzi Mkuu na hasa kutotumika katika kupandikiza chuki na uhasama kwa wananchi. Jukwaa limewataka wananchi kuitumia vizuri haki yao ya kupiga kura kwa kushiriki kikamilifu katika zoezi la kupiga kura, kutokubali kununuliwa na wanasiasa, kutouza kadi zao za kupigia kura huku likiwasihi wawe makini katika kufuatilia wagombea katika kampeni zao ili waweze kubaini na kujiridhisha na kiongozi anayewafaa.

Na Pascal Mwanache,

Dar Es Salaam.

TAMKO LA VIONGOZI WA DINI KUHUSU UHURU, HAKI NA AMANI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU LEO TAREHE 17.09.2015

Sisi, viongozi wa dini pamoja na taasisi zinazosimamia mchakato wa uchaguzi (NEC,TAKUKURU, Polisi pamoja na Msajili wa vyama vya siasa)  tuliokutana leo tarehe 17/9/2015, tumepata nafasi ya kujadili kwa kina suala la uhuru,haki na amani kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika 25/10/2015 na wajibu wa kila mdau kuhakikisha kuwa uhuru,haki na amani vinalindwa kipindi hiki.Suala la uhuru haki na amani ni wajibu wetu sisi viongozi wa dini na watanzania wote kwa ujumla na halina mjadala.Kila mmoja achukuwe nafasi yake kulinda uhuru,haki na amani na kuweka uzalendo kwanza kuliko kutanguliza maslahi binafsi ya vyama vya siasa.

Viongozi wa dini wamepata nafasi ya kujadili na vyombo hivi masuala ya msingi kama kuhakikisha kuwa maadili ya uchaguzi yanazingatiwa kwa wote, muda wa kutangaza matokeo ya kura unazingatiwa , haki ya wananchi kupata matokeo haraka ili kuepuka fujo wakati wa kusubiri na kutangazwa kwa matokeo. Jeshi la polisi kutokutumia nguvu kupita kiasi, wajibu wa Msajili kuhakikisha vyama vyote vinapata fursa sawa na pia tumejadili suala la kutumia nyumba za ibada kama sehemu ya jukwaa la siasa.

Viongozi wa dini tumekubaliana kwa pamoja kuepuka kutumia nyumba za ibada kuonyesha ushabiki wa aina yoyote kwa chama chochote cha siasa.

Baada ya kujadili kwa kina masuala hayo viongozi wa dini wanatoa wito ufuatao;

1. Vyombo vya habari vifanye kazi kwa ueledi bila upendeleo na pia kuhakikisha kuwa inatoa taarifa ya kutosha kuelimisha umma.

2. Tunaishauri NEC kwenye chaguzi zijazo  iweke utaratibu maalum wa kuruhusu wanafunzi wa vyuo vikuu waliojiandikisha pamoja na watu wote waliojiandikisha/watakaojiandikisha waweze kupiga kura.

3. Tunaishauri  NEC    kwenye chaguzi zijazo  siku ya kupiga kura isiwe siku ya ibada.

4. NEC iendelee kutoa elimu ya uraia  kuhusu haki ya raia kupiga kura na haki yao ya  kukaa mita mia moja kusubiri matokeo yatangazwe kwa utulivu kama ambavyo NEC imehakikishia viongozi wa dini kuwa kila kituo itabandika matokeo yote (Urais,Ubunge na Udiwani)

5.  Pamoja na kutimiza wajibu wake wa msingi wa kulinda raia na mali zao Jeshi la polisi wakati huu wa uchaguzi  liendelee kutimiza wajibu wake wa kusimamia amani na taratibu kwa haki bila upendeleo.

6. Wagombea,wafuasi   na wanaowanadi,  wanaaswa waache mara moja lugha za matusi,vitisho,kejeli na kukashifiana vinavyoweza kuchochea fujo na kuleta uvunjifu wa amani wajikite kunadi sera za vyama vyao.

7.Tunawahimiza wananchi kuwa makini katika kufuatilia kampeni na sera mbalimbali za wagombea, kuzipima kwa hali ya juu sera hizo, kutokuuza kadi zao za kupigia kura, kutokununuliwa na kujitokeza kwa wingi kutumia uhuru na haki yao ya kuchagua viongozi wanao wataka kwa hiari na  amani.

 8. Viongozi wa dini wanawahimiza Watanzania wote kuendelea kuombea nchi hii kuendelea kuwa  taifa lililojengwa   katika misingi ya uhuru , haki na amani.

9. Viongozi wa dini tutabaki kuwa manabii na wahubiri wa uhuru,haki na amani wakati huu , wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi

Sisi viongozi wa dini Tunawashukuru Inspekta generali wa polisi, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Msajili wa Vyama vya siasa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kwa ufafanuzi makini na wa kina juu ya nafasi na utayari wao wa kushirikiana na viongozi wa dini kuhakikisha uhuru, haki na amani vinaendelea nchini.Maelezo yao na mafafanuzi  yao tumeyasikia  na tutaendeleza kwa kuwa  hiki ni kikao cha mwanzo na tutaendelea kuwa na vikao vingine pamoja nao kuelekea uchaguzi mkuu ili kufuatilia utekelezaji na kuendeleza makubaliano yetu katika kuhakikisha uhuru,haki na amani.








All the contents on this site are copyrighted ©.