2015-10-06 08:41:00

Onesheni upendo, umoja na huduma ili kukabiliana na changamoto kwa familia


Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia yanaendelea kwa kasi mjini Vatican kwa kuongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa Familia katika Kanisa na Ulimwengu mamboleo”. Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha Mababa wa Sinodi kwamba, Sinodi ni mchakato wa Kanisa kutembea kwa pamoja kwa kusoma alama za nyakati, huku wakisikiliza kwa makini sauti ya Roho Mtakatifu. Ni fursa ya kuonesha umoja na mshikamano wa Kikanisa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na Familia ya binadamu katika ujumla wake.

Ni mchakato unaojikita katika mikakati ya shughuli za kichungaji, mafundisho sadikifu ya Kanisa, hekima na ukweli. Amana ya imani ni kisima cha maisha mapya na wala si hifadhi ya makumbusho ya kale. Maadhimisho ya Sinodi yanatekelezwa kwa kuzingatia mahitaji ya Familia ya Mungu, changamoto inayohitaji ujasiri wa kitume, unyenyekevu wa Kiinjili na utekelezaji unaojikita katika imani. Mwenyezi Mungu anaendelea kuzungumza na waja wake katika ukimya, changamoto kwa Mababa wa Sinodi kusikiliza sauti ya Mungu katika mikutano yao; ili kweli Kanisa liendelee kuwa aminifu kwa Kristo. Sinodi ni mchakato wa hija ya imani, furaha na matumaini kwa familia ya binadamu.

Wakati huo huo, Kardinali Berhaneyesus Soraphiel, Mwenyekiti wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA ambaye pia ni mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki, CUEA, katika maadhimisho ya mahafali ya 32 tangu CUEA ianzishwe, amezitaka Familia Barani Afrika kuhakikisha kwamba, zinajikita na kufumbata upendo, umoja na huduma makini, ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika taasisi ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo.

Kardinali Souraphiel anakaza kusema, utajiri si nyenzo msingi ya kuzifanya familia kuwa na furaha ya kweli, bali ni fadhila ya upendo, umoja na mshikamano ni mambo msingi na chachu ya furaha ya kweli ndani ya familia. Kardinali Souraphiel anahudhuria maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia yaliyofunguliwa rasmi, Jumapili iliyopita kwa Ibada ya Misa takatifu na Jumatatu, tarehe 5 Oktoba, 2015, Mababa wa Sinodi wakaanza vikao vyao rasmi.

Wazazi na walezi wanapaswa kuonesha hali ya upole, unyenyekevu, umoja na amani ndani ya familia, nyenzo msingi katika kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kuiandama familia ya binadamu katika ulimwengu mamboleo. Kwa namna ya pekee, kwa niaba ya AMECEA, Kardinali Souraphiel anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuitisha maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ambayo kwa sasa yameingia awamu ya pili, ili kujadili na kupembua kwa kina na mapana: “wito na utume wa Familia ndani ya Kanisa na Ulimwengu mamboleo”.

Kardinali Souraphiel anaitaka Familia ya Mungu kuhakikisha kwamba, inajikita katika utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji “ Laudato Si” “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Katika mahafali haya wanafunzi 1, 591 wamehitumu masomo yao katika viwango mbali mbali. Mgeni rasmi alikuwa ni Mama Angelina Wapakabulo, Balozi wa Uganda nchini Kenya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.