2015-10-06 14:46:00

Makanisa mahalia yamechangia katika maandalizi ya Sinodi ya Familia


Kardinali Andrè Vingt-Trois, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Paris, Ufaransa ambaye pia ni Rais mwakilishi katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia katika hotuba yake, Jumatatu, tarehe 5 Oktoba 2015 amegusia umuhimu wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia katika awamu kuu mbili, ili kulipatia Kanisa nafasi ya kupembua kwa kina na mapana utume wa familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo. Awamu ya kwanza imekuwa na mafanikio makubwa na Maaskofu wenyewe ni mashuhuda wa tukio hili.

Makanisa mahalia katika kipindi cha mwaka mzima, yamejitahidi kutafakari na hatimaye, kuchangia kwa kujibu maswali dodoso yaliyotolewa na hatimaye, kuchapishwa kwa hati ya kutendea kazi kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi, hati inayojulikana kwa lugha ya Kilatini kama “Instrumentum Laboris”. Amegusia pia Waraka binafsi wa Baba Mtakatifu Francisko “Mitis Iudex Dominus Iesus”, inayobainisha mchakato na njia zinazopaswa kufuatwa ili kuhakiki kuhusu ukweli wa Sakramenti ya ndoa kati ya waamini wanaokabiliana na mgogoro wa maisha ya ndoa na familia.

Nyaraka hizi mbili ni muhimu sana kwa Mababa wa Sinodi katika kutafakari na hatimaye, kuchangia mawazo yao katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia inayoendelea hapa mjini Vatican. Hapa inapaswa kukumbukwa kwamba, Mababa wa Sinodi wataendelea kuzingatia Mapokeo ya Kanisa kuhusu Sakramenti ya Ndoa, Mafundisho kuhusu udumifu wa ndoa pamoja na kushirikishana uzoefu na mang’amuzi yao ya shughuli za kichungaji. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kuibua mbinu mkakati utakaowawezesha waamini kutangaza Injili ya Familia inayojikita katika huruma ya Mungu inayoambata ukweli mfunuliwa na changamoto ya kutubu na kuongoka, tayari kukimbilia msamaha wa dhambi unaotolewa na Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.