2015-10-05 13:40:00

Watanzania dumisheni haki na amani ili kufanikisha uchaguzi mkuu 2015


Watanzania wanapoendelea na kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaoratajiwa kufanyika hapo tarehe 25 Oktoba 2015 wametakiwa kujenga na kudumisha amani, utulivu na maridhiano, ili kutoa nafasi kwa wagombea nafasi mbali mbali za uongozi kuweza kunadi sera na vipaumbele vyao. Changamoto hii imetolewa hivi karibuni na mkuu wa mkoa wa Dodoma Chiku Galawa katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake hivi karibuni na mwakilishi kutoka Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dodoma wakati wa kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu na kumbu kumbu ya takribani miaka 50 ya uwepo wa Wamissionari hao nchini Tanzania.

Mkuu wa mkoa wa Dodoma kwa namna ya pekee amewapongeza Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania kuwa kweli ni wadau wakuu wa maendeleo kwa mikoa ya Kanda ya kati. Huko wamekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa wagonjwa na maskini; elimu kwa watoto na vijana, huduma ya maji pamoja na kukoleza mchakato wa maendeleo endelevu ya watanzania: kiroho na kimwili. Sherehe hizi zilihudhuriwa na umati mkubwa wa Familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Dodoma, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.