2015-10-05 10:37:00

Mtikila aliyeitikisa Tanzania amefariki akiwa na ndoto nyingi za demokrasia!


Watanzania wanaomboleza kifo cha Mchungaji Christopher Mtikila, Mwenyekiti wa Chama cha DP, aliyefariki dunia kwa ajali ya gari Jumapili tarehe 4 Oktoba katika kijiji cha Msolwa, Chalinze, Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani akiwa anatoka Mkoani Njombe kuelekea Dar Es Salaam. Mchungaji Mtikila anakumbukwa na wengi kwa kusimama kidete kutetea demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania kunako miaka 1990. Mara kadhaa amefungua kesi dhidi ya Serikali ya Tanzania na kushinda, ingawa maamuzi yake pengine hayakutekelezwa kutoka na mazingira ya kisiasa ya wakati wake. Ni kiongozi wa kwanza kisiasa nchini Tanzania kudai uwepo wa mgombea huru wa Urais, kwani hii ni haki ya watanzania kikatiba. Alidai pia uwepo wa Tanganyika. Ni kiongozi aliyetiwa mbaroni mara kwa mara na vyombo vya ulinzi na usalama.

Wakati huo huo, Mjumbe  wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Mhe. Mizengo Pinda amesema yeye hana kinyongo na uteuzi wa Dk. John Pombe Magufuli kuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM kwa sababu anaamini kuwa Mungu alikwishamuandaa.  “Tulikuwa wengi kwenyhe kinyang’anyiro cha urais lakini Makamu wa Rais ametolewa, Waziri Mkuu aliyepo ametolewa, Mawaziri Wakuu wastaafu wametolewa, Majaji na mabalozi wametolewa, mawaziri wengine wametolewa; hivi ni kwa nini useme kwamba wewe tu ndiye unayefaa kuteuliwa? Ni kwamba Mungu alikwishamuandaa mmoja wetu,” alisema.

Ametoa kauli hiyo Jumamosi, Oktoba 3, 2015 wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa jimbo la Mpanda Vijijini kwenye mikutano minne ya hadhara iliyofanyika katika kata za Kasekese, Kapalamsenga, Karema na Ikola. “Magufuli ni muadilifu, ni mchapakazi, hana blah blah za kisiasa na hapendi rushwa. Ni mtu anayetaka kuona matokeo na mwenye kujali watu wanyonge. Nimefanya naye kazi kwa muda mrefu, ninamfahamu, ninaomba mumpe kura ya ndiyo ifikapo terehe 25 Oktoba,” alisema Mhe. Pinda wakati akimuombea kura Dk. Magufuli.

Akizungumzia mafanikio ya serikali ya awamu ya nne, Mhe. Pinda alisema Serikali ya CCM imefanya kazi nzuri kwa kufungua barabara za vijijini akitoa mfano wa barabara ya Mpanda hadi Karema ambayo alisema imeboreshwa tofauti na ilivyokuwa miaka 10 iliyopita. “Wakati huo ukitoka Mpanda kuja Karema ilimchukua mtu hadi siku tatu wakati ni umbali wa km. 150 tu… leo hii mtu anatoka Karema hadi Mpanda na kuunganisha mabasi ya Mwanza siku hiyo hiyo,” alisema.

Alisema katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015, Serikali ya awamu ya tano imepanga kujenga reli mpya ya viwango vya kimataifa (standard gauge) kutoka Kaliua kupitia Mpanda hadi Karema. Alisema anaamini reli hiyo itakuwa ni kiungo cha kuleta maendeleo ya haraka kwenye ukanda huo wa Magharibi.  Alisema Seikali itaendelea kuwaletea maendeleo wanandhi ikiwemo kubotesha huduma za maji, umeme na mawasiliano ya simu.

Aliwataka wakazi wa jimbo hilo watunze shahada za kupigia kura na wasikubali kurubuniwa na mtu yeyote iwe kwa fedha au kitu chochote. “Usikubali kumpa mtu shahada yaka hata kama ni motto wako. Ninawasihi mjitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura wala msisikilize vitisho vya mtu yeyote kwamba hakutakuwa na amani,” alisema. Mhe. Pinda alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini, Bw. Selemani Moshy Kakoso pamoja na madiwani wa kata zote nne. Akiwa Karema, Mhe. Pinda alipokea kadi za wanachama waliorejea CCM kutoka vyama vya CHADEMA NA ACT Wazalendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.