2015-10-05 08:20:00

Msifanye majaribio kwa nadhiri zenu za kitawa! Mtakiona che mtema kuni!


Kardinali Polycarp Pengo Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam amewaasa watawa nchini Tanzania kusimama kidete na kuziishi nadhiri zao kikamilifu bila kusita ili kupitia utume wao ulimwengu upate kutakatifuzwa na Mwenyezi Mungu kupewa sifa na utukufu. Kardinali Pengo ametoa nasaha hizo hivi karibuni katika sherehe za kuweka nadhiri za kwanza kwa Masista wa Shirika Watawa wa Mama yetu wa Wakarmeli zilizofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Vincent wa Paulo-Vikindu, Jimbo kuu la Dar es Salaam ambapo amehimiza umuhimu wa watawa kujikita katika azma ya kuyatakatifuza malimwengu hasa nyakati hizi ambapo mwanadamu anapoteza hofu ya Mungu.

“Ninyi mmetambua kuwa Mungu mnayetaka kumtumikia siyo wa Hekaluni pekee, bali kwa kuutumikia ulimwengu mzima. Hakuna kusita sita wala kukawia, tekelezeni kama Mungu alivyoagiza. Ikiwa mtu aliyewekwa wakfu anaanza kusita au kuhoji kama wito alionao ni wa Mungu au wa mwanadamu, utume wake huwa wa kusita sita pia.

Tunalolijua kuwa ni la Mungu hatuna haja kulichunguza na kutia mashaka kana kwamba hatukujua kuwa yupo Kristo na upo ulimwengu. Kama mmekaa na kufundishwa Katekisimu toka mkiwa kwa wazazi wenu na hata katika Shirika basi mtambue kuwa hakuna haja ya kusita sita. Unaanzaje kusita juu ya nadhiri zako” amehoji Kardinali Pengo.

Aidha Kardinali Pengo amewataka watawa hao na wengine wote kutogeuka nyuma katika wito wao na kamwe kutojiachia mbele ya ulimwengu. Amewaasa watumie karama walizonazo katika kuufanya ulimwengu kuwa sehemu salama na yenye matumaini hasa kupitia sala na matendo yao yenye kutakatifuza ulimwengu. “Usafi wenu udhihirike katika matendo yenu. Heshima yenu kwa Kanisa iwe pia kwa ulimwengu mzima, hamna ruhusa ya kujiachia mbele ya ulimwengu. Hatutegemei kuja kunyang’anyanamali na ninyi au kukutana katika anasa mbalimbali za dunia hii bali tunategemea sala kutoka kwenu kwa niaba ya ulimwengu” amebainisha Kardinali Pengo.

Pamoja na mwito huo kwa watawa, Kardinali Pengo amewataka waamini kusali kwa ajili ya kuwaombea watawa ili utume wao uendelee na kuleta tija kwa maisha ya ulimwengu huu wenye kila namna ya fujo. “Tunakusanyika kuwaombea ili nadhiri mnazoweka leo mziishi kikamilifu. Tunaamini kuwa mnajitoa kikamilifu katika Kristo na hatutegemei kitu kingine kitokee. Mmetoa maisha yenu kwa ajili ya Kanisa na ulimwengu wote. Si kila mtu anaweza kujitoa kikamilifu kama ninyi. Hivyo nawaalika waamini tusali kwa ajili siyo tu ya hawa wanaoweka nadhiri, ila watu wote waliowekwa wakfu ili utume wao uendelee kunufaisha ulimwengu” ameeleza.

Pia Kardinali Pengo ameelezea umuhimu wa watawa katika ulimwengu wa leo kuwa dunia inahitaji watu kama hao wanaosimama mbele ya Mungu kwa niaba ya watu wa ulimwengu huu ambao mara nyingi wanajisahau na kujikuta wakishughulika na mambo ya dunia bila kuhangaikia juu ya ufalme wa mbinguni.

Akitoa shukrani, mmoja wa watawa hao walioweka nadhiri Sr. Irene ameeleza kuwa mchango wa wazazi, walezi na waamini ni muhimu katika kuitikia miito mbalimbali. “Tunamshukuru Mungu kwa neema zake anazotujalia na kutufanya hivi tulivyo. Tunayo furaha kuwashukuru ninyi nyote kwa sala zilizotufikisha leo. Tunakushuru Baba Mwadhama kwa upendo wako na ujumbe uliotupatia hasa ule unaotutaka kubaki waaminifu. Aidha wazazi mmetusaidia kuitikia wito na hasa kwa kuturuhusu kuingia katika wito huu. Nanyi waamini tunawashukuru kwa kuungana nasi, tunaendelea kuomba sala zenu” ameeleza.

Ibada ya Misa Takatifu iliyoenda sambamba na uwekaji wa nadhiri hizo imeongozwa na Kardinali Pengo huku tukio hilo likishuhudiwa na watawa kutoka mashirika mbalimbali, mapadri, waamini na wageni kutoka sehemu mbalimbali. Watawa walioweka nadhiri zao za kwanza ni Sista Julitha Shirima, Sista Irene Kavishe, Sista Bibiana Luhanga na Sista Julitha Tarimo.

Na Pascal Mwanache. Dar es Salaam.








All the contents on this site are copyrighted ©.