Karibuni nyote katika makala Dunia Mama ambamo tunaendelea kujielimisha na masuala mbalimbali yanayohusiana na maisha mchanganyiko, tukiwa ndani ya familia ambamo kwa kawaida tuna baba , mama, watoto na wazee na wagonjwa.
Katika wakati huu ambamo Mababa wa Kanisa, wameanza Mkutano wa Sinodi kwa ajili ya kutazama kwa makini Wito na Utume wa Familia ndani ya Kanisa na ulimwengu wa Kisasa, leo Kipindi Dunia Mama kinapenda kuanza na kundi la wazee, ambao ni mzizi mkuu wa familia. Wazee wetu tunaoishi nao ndani ya familia na nje ya familia zetu ambao tunakutana nao makanisani na mitaani. Alhamis iliyopita ambayo ilikuwa ni tarehe Moja Oktoba, dunia iliadhimisha siku ya Kimataifa ya Wazee. Ilikuwa ni Siku nzuri ya kupendeza kwa vijana kuwaenzi watu wenye umri mkubwa wazee waliohekimishwa na uzoefu wa maisha. Wanasayansi wanasema kuzeeka ni suala la maendeleo kimaisha na wanafalsafa wanasema uzee ni chemchemi ya hekima katika maisha ya familia , kijamii na katika mipango ya kiuchumi.
Kumbe basi tunapowazungumzia wazee, tunaoishi nao katika familia na nje ya familia zetu ,inapaswa kuwa kwa heshima zote, maana ni stahili yao. Tena tunawaheshimu kwa ufahamu kwamba, kuishi kwao miaka mingi kumewapa uzoefu wa kutosha kimaisha na wameona mengi pia na hivyo wanakuwa ni hazina kubwa kwa vizazi vipya.
Kwa kujali umuhimu wa kundi hili la vijana wa juzi , Umoja wa Mataifa uliitangaza tarehe moja Oktoba kuwa Siku ya Kimataifa ya Wazee. Kwa mwaka huu Siku ya Kimataifa ya wazee, iliadhimishwa chini ya kauli mbiu: Wazee , Nguvu Mpya ya Maendeleo. Huu ni wito makini, unaopaswa kufanyiwa kazi na lika la vijana , kuona maana yake ni nini hasa.
Mwenye Heri Papa Paulo VI , katika waraka wake wa Maendeleo ya Watu , akitaza wajibu wa familia alisema , hakuna binadamu anayeweza kusema anajitosheleza mwenyewe kimaisha, bali ameunganishwa na wengine katika mfumo wa kijamii, na hili linamhusu kila mwana familia wa lika zote. Kumbe hata yule mkongwe asiyejiweza uwepo wake ndani ya familia huleta ujotojoto wa mshikamano na kuwajibika na kiungo hiki asili kinachounganisha binadamu mmoja kwa mwingine.
Sayansi ya maisha ya watu inaonyesha kwamba kuna mabadiliko makubwa yanayoendelea duniani kote kuhusu maisha ya watu, kwamba dunia ya watu inaendelea kuzeeka zaidi ya kuwa kijana kwa maaana kwamba idadi ya watu wazee inakuwa kubwa kuliko vijana. Takwimu zimetolewa kwamba, duniani kote kuna jumla ya watu millioni 600 wana umri wa miaka zaidi ya 60, idadi inayotazamiwa kuwa mara mbili ifikapo mwaka 2025. Na kwamba hadi mwaka 2050 wazee watakuwa karibia billioni mbili, na wengi wao watakuwa katika nchi zenye viwanda vichache, ambako kwa wakati huu kuna idadi kubwa ya vijana na watoto. Kumbe kama ilivyonena Kaulimbiu ya adhimisho la Siku ya Kimataifa ya wazee kwa mwaka huu, Wazee , wanaendelea kuwa nguvu mpya ya Maendeleo.
Mpendwa , pengine hapa mtu angeuliza ni umri upi mtu anaweza tajwa katika kundi la wazee ? Wachambuzi wa maisha ya jamii wanasema mtu huingia katika kundi la wazee kuanzia umri wa miaka 65 hadi 74, baada ya umri huo mtu huingia katika kundi la kuitwa mkongwe.
Umoja wa Mataifa ukitafakari kwa kina mabadiliko haya ya maisha ya watu, unaonya kwamba , kwa kadri dunia inavyozidi kuzeeka kwa haraka, ndivyo mchango wa wazee unavyozidi kuhitajika kupitia kazi za urithishaji uzoefu na maarifa, licha ya kuwa msaada kwa familia zao na majukumu. Na hivyo unasisitiza haja ya kuongeza ushiriki wa wastaafu katika utendaji wa kazi mbalimbali, kwa malipo yanayostahili hata kama ni wana umri wa kustaafu.
Tayari mpaka sasa, hakuna anayeweza kukanusha kwa jinsi wazee wanavyotoa mchango
wao mkubwa kwa jamii. Kwa mfano, Afrika na mahali pengine, mamilioni ya watu wazima
wagonjwa, hasa maradhi yasiyoponyeka haraka kama UKIMWI au saratani , hutuzwa nyumbani
na wazazi wao. Na kinapotokea kifo, watoto yatima wanaoachwa na wazazi, mara nyingi
hubaki katika uangalizi wa bibi au babu. Takwimu zinaonyesha kwa sasa, kuna kundi
la watoto milioni 14 chini ya umri wa miaka 15 katika nchi za Afrika peke yake, walio
chini ya uangalizi wa babu na bibi zao. Lo ni raha iliyoje kulea wajukuu!
Taarifa mbalimbali zinaonyesha pia kwamba, si tu katika nchi zinazoendelea ambako
wazee wana jukumu kubwa katika maisha na maendeleo ni muhimu, lakini hata katika
nchi za Magharibi , zinazojiita zimeendelea. Mfano unatolewa nchini Hispania, wanao
fanya kazi kubwa ya kutunza watu binafsi tegemezi hasa wanaokabiliwa na maradhi
mbalimbali ,wagonjwa wa lika zote, zaidi hufanywa na wazee majumbani mwao na
hasa wanawake wazee.
Mpendwa , Ni matumaini ya kipindi Dunia katika wakati huu wa Sinodi ya Maaskofu juu ya utume wito na utume wa familia ndani ya kanisa na ulimwengu wa Kisasa, kwamba katika maamuzi yake paia watatoa tamko kwa ajili za kichungaji kwa watu wazee na utume wao katika kanisa. Moja ya nyaraka za Baraza la Kipapa kwa ajili ya Walei, inaeleza kwamba, Maendeleo ya kisayansi, hasa maendeleo katika uwanja wa tiba na dawa, umechangia kwa kiasi kubwa katika miongo ya hivi karibuni, kuongeza muda wa wastani wa maisha ya binadamu. Jina la kizazi cha tatu, limekuwa sehemu kubwa ya idadi ya watu duniani : watu wastaafu katika kazi ya ajira ya kazi, lakini, wanabaki kuwa rasilimali kubwa ndani ya familia , wakiwa na uwezo wa kutoa mchango kwa manufaa ya familia na umma.
Ni vyema kwamba , Mama Kanisa daima huonyesha kujali hali hii ya uwepo wa wazee, na sasa kutokana na taarifa hizi za idadi ya wazee kuwa kubwa kuliko watoto na vijana , Kanisa linapaswa tangu sasa kuandaa utaratibu wa kukabiliana na hali hiyo, mbayo grafu hii ya idadi ya watu inapaswa kuwa kinyume chake. Tumeona Ripoti ya mwaka ya Siku ya Kimataifa ya wazee iliyotolewa na WHO, kwamba idadi ya watu duniani iko katika kasi kuzeeka, kiasi kwamba, 2050, idadi ya watu duniani walio na umri wa zaidi ya miaka 60 itakuwa mara mbili kutoka asilimia 11% hadi 22%. Hili ni jambo la kutisha, hasa kwa kujiuliza nani atakuwa nguvu kazi ya jamii iwapo sote tunachechemea kwa uzee?
Watu vijana wanaweza tishika na hali hiyo, hasa kuwa na uchovu wa kuhudumia wazee. Baba Mtakatifu Francisco akiiona mbali kuzuka kwa tatizo la vijana kuchoka kuhudumia wazee , akihutubia maelfu ya watu, Jumapili ya tarehe 28 Septemba, ,mwaka jana , alikemea moyo wa kutaka kukatisha maisha ya wazee aidha kwa huduma mbovu za kutowajali akiita ni “eutanasia” ya kimyakimya kwa wazee ambayo hufanywa na baadhi ya watu iwe majumbani au katika taasisi. Papa alisema uwepo wa wazee majumbani, huziba pengo la upweke fulani katika mahusiano ya kifamilia. Papa Francisco alieleza na kutoa mfano wa jinsi Papa Mstaafu Benedikto XV1, ambaye mwaka huu ana miaka 88, uwepo wake ndani ya Vatican, ambako anaishi kama babu nyumbani kwake, kunaleta faraja na jotojoto la uhai wa maisha Vatican.
Tafakari za Baba Mtakatifu Francisco kwa wazee , zinatongoza katika kuona thamani ya uwepo wa watu wenye maisha marefu, kwamba huwa na mengi ya kusema katika maisha ya jamii. Na alitoa wito wa kuheshimu utu na haki zao msingi . Alihimiza uwajibikaji wa mtu binafsi, familia , vyama, serikali na mashirika ya kimataifa, katika kufanikisha afya na huduma bora kwa wazee. Na alionya Wazee wasibaguliwe au kuhesabika kama watu waliomaliza muda wao, watu wa kuwekwa pembeni kwanza katika huduma , lakini wao ni sehemu ya jamii hata katika mchakato wa mabadiliko ya maisha, kiuchumi na kiutamaduni.
Katika wakati huu ambamo sote tunaungana na Mababa wa Sinodi huku tukisubiri kwa hamu matokeo ya sinodi hii juu ya Wito na utume wa familia, tunaitwa pia kuwaombea wazee wetu, hasa wanaoshiriki katika mchakato huu wa Sinodi , hekima na uzoefu wao , uweze kusikilizwa na wajumbe wa sinodi. Aidha na tukumbuke wajibu wetu kama sehemu ya familia katika kuhudumiana daima, tukiwa na wepesi wa kuomba ruksa kabla ya kutenda jambo, kushukuru kwa kila jambo na kuomba samahani kwa mapungufu yetu hata kwa wazee wetu. Basi kwenu nyote kwa wakati huu nawaomba myaandike maneno haya mioyoni mwenu , Naomba, Asante na samahani kuwa ni silaha ya kudumisha umoja na mshikamano wa kila familia na jamii. Daima tukumbuke kusema kwa wazee wetu , Naomba , Asante na Nisamehe.
Makala haya huandaliwa nami TJMhella.
All the contents on this site are copyrighted ©. |