2015-09-28 09:15:00

Ziara ya Papa Marekani:Awaasa Maaskofu kukemea anasa na utamaduni wa taka


Jumapili Baba Mtakatifu Francisko alikutana na Maaskofu wote waliokuwa wakihudhuria Mkutano wa Nane wa Dunia  wa Familia huko Philadelphia Marekani .

Hotuba ya Papa kwa Maaskofu hao,ilionyesha furaha yake ya kuwa pamoja nao katika muda huo  wa kushirikishana tafakari za Kichungaji kwa maisha ya familia, chimbuko la binadamu. Na pia iliwaasa Maaskofu kuwa macho na ongezeko la utamaduni wa taka, unaorarua familia na jamii leo hii.

Papa alikumbusha kwamba leo hii, tuko katika dunia ya ulaji na utupaji , tabia na mapenzi ya kujilimbikizia mali, inayo chukuliwa kama ndilo jambo muhimu la mtu kujivunia. Ubinafsi usiojali wengine, wala kuona umuhimu wa kujali hali za binadamu wengine.  Kama matokeo yakePapa anasema,  ,  jamii zimegeuzwa kuwa uwanja wa maonyesho ya ufahari  wa  tamaduni mbalimbali,  ulifungamanishwa na maonjo ya kulimbikiza mali na utupaji wa onvyo,  wakati familia zingine zikiwa hazina chochote cha kujikimu katika mahitaji msingi.

Papa aliendelea kuzitazama hali halisi za sasa , jinsi ambavyo kuna mabadiliko katika maduka na masoko. Aliangalishwa kwa jinsi leo hii kunatengenezwa maeneo makubwa ya maduka yanayoitwa “supermarket”, yaliyojazwa vitu kupindukia, akisema  dunia hii sasa inaweza kuitwa dunia ya utamaduni wa supermarket, wenye kuleta ushindani mkubwa katika uzalishaji wa mali na ushindani zaidi wa  nani ana vitu vingi vipya kuliko mwingine. Hali iliyoua moyo wa mshikamano na umoja na wengine, na kuvunja uaminifu katika mahusiano ya kijamii. Urafiki leo unajengwa zaidi katika misingi ya utajiri. Wenye navyo wanawatafuta wenzao walio navyo. Hivyo mambo yanayowaunganisha watu yanahusishwa zaidi na vitu alivyo navyo mtu. Ile misingi ya kujaliana kama binadamu au  jirani haipo tena, Ujirani unajengwa zaidi katika misingi ya anasa na ulafi.

 Papa ameonya, matokeo yake  ni kuwa na utamaduni wa taka, utamaduni wa kuchoka haraka na vitu na kuvitupa , hata kama bado vinaonekana kufaa kutumia vinatupwa  kwa nia za kuwahi kununua mitindo mipya inayojitokeza katika masoko.  Huu ni uharibifu mkubwa , kwa kuwa kiundani hujenga moyo wa kubaguana. Wale wasioweza kwenda na kasi hii ya utamaduni wa utupaji , hupata hisia za kuwa wanyonge na wapweke.  Upweke wenye kuwa na woga katika juhudi za kutimiza wajibu wao, kwa kuwa hujiona hawezi kufanya lolote katika jamii maana hawana kitu.

Baba Mtakatifu aliendelea kuhoji iwapo lawama zitupiwe vijana wanaokua katika aina hii ya jamii, au kuwalaumu kwa kuishi katika ulimwengu wa aina hii. Aidha Papa alihoji iwapo wachungaji wa kiroho, wahimize vijana kurudi kaika maisha ya ujima, kwa kuwa dunia sasa inasambaratika wala mwisho wake haujulikani utakuwaje? Papa alitoa hisia zake kwamba, hadhani kama ni sahihi kurudia maisha ya ujima. Lakini Maaskofu kama wachungaji wa kanisa ni lazima kufuata  nyayo za Mchungaji mwema, wanatakiwa kuandamana na watu na kuwainua na kutibu majeraha ya nyakati.  Kuzitazama hali halisi, kwa jicho makini, kwa ajili ya kutenda inavyopaswa , kazi za kichungaji zenye kuleta uongofu. Dunia ya leo inahitaji uongofu wa  moyo . Na hivyo inakuwa ni muhimu kwa kanisa leo hii kusonga mbele kwa ushupavu zaidi kuihubiri Injili kwa watu wote mahali popote nakatika matukio yote, bila kusita sita wa kuhofia kitu. Ni kuihubiri furaha ya Injili kwa watu wote bila ubaguzi.

 

Na hivyo aliwahimiza Maaskofu kuonyesha kushikamana na familia katika misingi ya kiinjili. Ni muhmu tena lazima kwa ajili ya kutengeneza mazingira ya jamii kujaliana, kuanza kufanya mabadiliko ndani ya familia. Kusadikisha watu kwamba, familia ni habari njema kwa maisha ya  dunia hii iliyomezwa na moyo wa ubinafsi na utamaduni wa taka.

Alikumbusha  katika maisha ya Kanisa,  familia hupewa kipaumbele cha kwanza kwa sababu,  familia ni mpango wa Mungu katika maajabu yake ya uumbaji. Na siku zote na mahali pote  duniani, Kanisa linapaswa kuifurahia zawadi hii ya Bwana kwa uwepo wa familia,  hata wakati wa majaribu na matatizo , hubaki aminifu katika ahadi yake na katika kuitunza imani.

Baba Mtakatifu aliendelea kuwaasa Maaskofu wenzake juu ya changamoto za Kichungaji zinazowakabili leo hii katika nyakati hizi za mabadiliko makubwa. Hivyo akasisitiza Kanisa kuwa na maamuzi thabiti katika kutambua zawadi hii kuu kutoka kwa Mungu. Papa alirudia kusema, familia ni misingi wa agano kati ya Kanisa na uumbaji wa Mungu . Bila familia , ina maana hata kanisa lisingekuwepo. Na hivyo Kanisa lisingeweza kuwa ishara na chombo kinachounganisha binadamu na Mungu na umoja wa kabila zote za  binadamu.

Papa aliendelea kuwataka Maaskofu wenzake kama wachungaji ,  kukusanya nguvu zao na kujenga upya shauku kwa ajili ya kuendeleza familia katika mahusiano yake ya milele, katika misingi ya utimilifu wa baraka za Mungu . Na kwamba, wanahitaji kuwekeza nguvu zao zote , si katika tu kufanya rejea kwenye matatizo ya kidunia yanayowazunguka , lakini katika uhalali wa uwepo wa familia ya Kikristo, kwa kutoa mwaliko wa dhati na ujasiri kwa vijana ,ili wachague maisha ya  ndoa na familia.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.