2015-09-26 12:43:00

Tafakari ya neno la Mungu Domenika ya XXVI ya Mwaka B, 27Septemba 2015


Mpendwa mwana wa Mungu,  katika kipindi tafakari Neno la Bwana, leo tunatafakari Dominika ya 26 ya mwaka B wa Kanisa. Neno la Mungu latutaka kutambua kuwa Roho wa Mungu ni zawadi kwa ajili ya wote ilimradi mmoja anaitumia zawadi hiyo kadri ya mpango wa Mungu.

Katika somo la kwanza kutoka kitabu cha Hesabu, tunaona jinsi Mungu alivyowashukia wale ndugu 70 na wakatabiri kama ambavyo Musa alikuwa akishukiwa na Mungu. Si hao tu bali kulikuwa na watu wengine wawili ambao wao katika harakati za kwenda hemani ambapo daima Musa alikuwa akikutana na Mungu wao walibaki kambini pia nao wakashukiwa na roho wa Mungu na wakaanza kutabiri. Tendo hili liliwaudhi watu wengine ambao waliona daima lazima Mungu agawe roho wake pale kwenye hema tu na si kwingine! Mpendwa jambo la wivu ni la zamani sana kama ambavyo tunaona kwa tukio hili. Je leo jambo hili lipo? Kabisa na ni kweli kwamba katika zama zetu kuna baadhi yetu ambao huona kama Roho Mtakatifu ni kwa ajili yao tu! Yapo makundi katika Kanisa katoliki ambayo hujisikia kabisa kwamba yanaweza kumkumbatia Roho Mtakatifu na kumteka kwa ajili yao tu! Labda pia kwenye makanisa mengine! Mpendwa hili ni kosa la kiteolojia na pengine linapaswa kukemewa mara moja na viongozi wetu wa Kanisa kwa sababu limekuwa ni jambo linalohangaisha na kuleta usumbufu kwa jumuiya ya Kanisa.

Somo la pili, linatualika kutazama vema juu ya suala la kuwanyonya maskini na hasa katika suala zima la malipo baada ya kazi. Mt. Yakobo anasema madhulumu kwa walio maskini huleta kilio ambacho humfikia Mungu mara moja kama kilio cha damu ya Abeli kilivyomfikia Mungu haraka. Anawakumbusha matajiri kutumia utajiri wao kwa haki na zaidi kuimarisha maisha ya ustawi uliojaa uwiano sahihi. Mpendwa mwana wa Mungu, kama tunataka kweli kushika vema Injili ya Kristu yatupasa kufikiria vema namna ya kushikama na utajiri ili kisiwe kikwazo bali chombo kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu.

Katika somo la Injili tunapata msaada wa kuweza kuelewa somo la kwanza ambapo tulisikia juu ya wivu kwa kuwa watu wawili ambao hawakuwa wameandamana na wale 70 pamoja na Musa nao walipata uwezo wa kutabiri. Ndiyo kusema mtu mmoja anatoa pepo kwa jina la Bwana lakini hayuko katika kundi la Mitume, na matokeo yake Yohane anamwambia Bwana kwamba walipomwona mtu huyu akitenda walimkataza asifanye shughuli hiyo ya kutoa pepo! Bwana anawajibu Mitume akisema hakuna ambaye atakuwa kinyume nami na kisha ataweza kutoa pepo kwa jina langu, kwa jinsi hiyo basi huyo yu upande wetu. Jambo la msingi ni kwamba mkuu wa shughuli nzima ya kitume ni Yesu Kristu na si Mitume kumbe yeye hugawa apendavyo karama zake. Roho Mtakatifu ni zawadi kwa wote hata wale ambao wako nje ya Kanisa linaloonekana, na hivi wanaotumia nguvu ya Kristu wanalisaidia Kanisa kusonga mbele katika shughuli ya wokovu.

Mpendwa sehemu ya pili ya Injili inazungumza na kutuasa juu ya ukarimu ambao Mt. Yakobo daima anasisitiza. Anawatayarishia heri wale wote watakaowakirimu Mitume wakiwa katika utume wa utangazaji wa Injili ya Bwana. Mpendwa , kazi ya kitume inaendelea na hivi wanaheri wale wote ambao wanaifanya kazi hiyo njema isonge mbele. Namna za kuifanya kazi ya kitume iende mbele ziko nyingi na mojawapo ikiwa kwa njia ya sala, kwa michango ya fedha na vitu, kuwahifadhi watumishi wa Kanisa mara kunapokuwa na hitaji kama vile nyumba, mfano parokia mpya inapofunguliwa.

Mpendwa, bado kuna hatua nyingine ya kutekeleza utume wa Kristu, nayo ni kuhakikisha huwi kikwazo au chanzo cha makwazo kwa jumuiya ya waamini, maana Bwana anasema atakayemkwaza mmojawapo wa wadogo hawa ni afadhali afungiwe jiwe na kutupwa katika kilindi cha maji marefu. Anazidi kusema kama kiungo kimojawapo cha mwili kinaleta chukizo basi ni vema kukiondoa na kubaki kilema kuliko kubaki mzima na ukapoteza uzima wa milele. Huu ni mwaliko wa kudumu kuhusu kazi ya kimisionari, na zaidi kazi ya wokovu inayodai utulivu na uvumilivu wa hali ya juu, kuweza kutafakari alama za nyakati tukiongozwa na Roho Mtakatifu.

Ninafurahi zaidi nikikutakia neema za Yesu mfufuka anayetukirimia Roho Mtakatifu kwa ajili ya wokovu wa watu na sifa kwa Mungu Baba. Tumsifu Yesu Kristu. Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya Cpps

 








All the contents on this site are copyrighted ©.