2015-09-24 08:43:00

Siku ya kwanza ya ziara ya Papa nchini Marekani


Jumatano , 23 .09.2015, ilikuwa ni siku ya kwanza ya  Baba Mtakatifu Francisco, katika ziara yake ya  Kitume nchini Marekani. Na  aliianza siku katika Mji Mkuu wa Marekani, Washington D.C kwa kutembelea Ikulu ya Marekani ambako kulifanyika hafla rasmi ya kumpokea mapema siku ya Jumatano kama ilivyoandaliwa na Mwenyeji wake Rais Barack Obama na wasaidizi wake, katika viwanja vya Ikulu. Mahali hapo pia kulikuwa pia na kundi kubwa la wageni waalikwa akiwemo Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki la Marekani USCCB Kardinali Donald Wuerl, Askofu Mkuu wa Washington D.C  na Maaskofu Wasaidizi wa Jimbo Kuu la Washington D.C. Papa alipokewa kwa heshima ya gwaride la Kijeshi na nyimbo za kitaifa , ikifutiwa na hotuba kutoka kwa Rais Barack Obama na baadaye Papa Kuhutubia. Baada ya tukio hili , Baba Mtakatifu Francisko , majira ya Alasiri alkutana na Maaskofu Katoliki wa Marekani katika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Mathayo na kufunga ratiba ya siku kwa kuongoza Ibada ya Misa katika Madhabahu ya Kitaifa ya Washington D.C. yaliyoko katika Chuo Kikuu Katoliki cha Marekani , kwa nia ya kumtaja Mwenye Heri Junipero Serra katika daraja la Watakatifu. 

Katika hafla ya Mapokezi, Baba Mtakatifu alitoa shukurani zake za dhati kwa mapokezi mazuri aliyopata kutoka kwa Rais Baraka Obama kwa niaba ya Wamarekani wote , na kwamba kama mtoto wa familia ya wahamiaji , pia aliona fahari ya kuwa mgeni katika taifa hilo ambalo kwa kiasi kikubwa limejengwa na familia za wahamiaji .Na alionyesha matumaini yake kwamba, katika siku hizi za kukutana na kuwa na mazungumzo, ataweza kusikiliza na kushirikishana  matumaini ya ndoto za Wamarekani wengi.

Aidha allitaja heshima aliyopewa ya kuhutubia Baraza la Congress,na kuwa na matumaini makubwa kwamba, kama ndugu wa nchi hii, maneno yake yataweza  kuwatia moyo wale wote walioitwa kuongoza mustakabali wa kisiasa wa taifa la Marekani, katika  uaminifu wa kanuni za mwanzilishi wake. Na pia akaitaja safari yake ya Philadelphia kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano wa Familia ya Dunia wa Nane, unaolenga kuonyesha ukuu na umuhimu wa kusaidia taasisi ya ndoa na familia, kama jambo muhimu katika historia ya ustaarabu  wa wakati wetu.

Baba Mtakatifu alieleza kutaja jinsi Wakatoliki nchini Marekani ,wanavyokuwa na shauku ya kujenga jamii ambayo kweli inathamini kuvumiliana na umoja kwa ajili ya kulinda haki za watu binafsi na jamii, na  katika kukataa kila aina ya uovu wa ubaguzi. Na kama ilivyo kwa watu wengine wenye mapenzi mema, pia ndio vivyo hivyo, wanavyojali juhudi  na uwepo wa jitihada za kujenga jamii ya haki kwa busara na heshima, katika misingi ya  haki ya uhuru wa kidini. Uhuru  ambao unaendelea kuwa moja ya nguzo muhimu kwa taifa la  Marekani. Na kama ambavyo Maaskofu wa Marekani wamekuwa daima wakikumbusha  juu ya umuhimu wa  kuwa macho katika lengo la kudumisha haki na uraia mwema,kuhifadhi na kulinda uhuru dhidi ya vitisho vyote.

Aidha hotuba ya Papa iligusia suala ya kutunza mazingira hasa katika  kuzingatia hatua zinazo pendekezwa katika kupunguza uchafuzi wa hewa. Papa amehimiza utendaji wa binadamu wa pamoja kwa ajili ya kuitunza dunia katika asili yake kama alivyoeleza katika waraka wake wa "(Sifa kwako  kwa utunzanji wa dunia ya wote.  Kama Wakristo aliongeza, kwa  hakika huu unakuwa ni  wajibu kwa ajili ya manufaa ya wote.

Hotuba ya Papa ilikamilika na mwaliko kwa wanaume na wanawake wote wenye mapenzi mema wa taifa la Marekani kutoa  msaada katika Juhudi za jumuiya ya kimataifa zinazolenga kulinda mazingira ya dunia yetu na kuwa kichocheo cha mifano muhimu ya  umoja katika  maendeleo, ili kwamba watu wote wa kila mahali wajue maana ya baraka ya amani na ustawi, kama mapenzi ya Mungu kwa watoto wake wote.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.