2015-09-23 09:17:00

Papa Francisko awasili Marekani


Jumanne,Baba Mtakatifu Francisco alikamilisha ziara yake kisiwani Cuba na kupanda ndege katika uwanja wa kimataifa wa Santiago akielekea Marekani Washington D.C , kwa ndege ya Altalia , safari iliyomchukua muda wa saa sita akiwa angani.Hii ni mara ya kwanza katika Maisha yake Papa Francisko kwenda Marekani. 

Akipita katika anga za nchi,  kwa njia ya telegramu alipeleka salaam zake za matashi mema kwa wakuu wa nchi akianzia Rais Raul Castro Ruz, akisema “wakati naondoka katika taifa pendwa la Cuba, napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwako wewe na watu wote wa Cuba kwa mapokezi mazuri mliyonipatia. Nami nawaombea Baraka za Mwenyezi Mungu, kwenu nyote na ninawahakikishia maombi yangu kwa ajili ya amani na ustawi wenu nyote”.  

Aidha Papa akipita katika anga la nchi ya Bahamas, alipeleka salaam zake kwa Mheshimiwa Rais  Marguerite Pindling, Gavana na Mkuu wa Jumuiya ya  Visiwa vya Bahamas , akisema, “Kwa mara ingine ninapopita katika taifa lako, napenda kurudia kutoa matashi mema kwako wewe na kwa wananchi wa nchi hii , nikiwaombea Baraka za Mwenyezi Mungu  kwa Bahama yote”.

Baba Mtakatifu alitua katika uwanja wa ndege wa Kijeshi wa Andrews wa Mjini Washington D.C majira ya saa kumi kwa saa za Marekani , ambako alipokelewa na  Rais Obama akiwa ameandamana na familia yake, mkewe na watoto, wakiwepo pia viongozi wengine wa Kiserikali na Kanisa. Wachambuzi wanasema, hi ilikuwa ni mara ya kwanza katika urais wake,  Obama kumpokea uwanjani Rais wa Nchi anayetembelea Marekani. Kwa kawaida hukutana na  wageni muhimu wanaomtembelea katika jengo la  Ikulu. Na pia hii ilikuwa ni mara ya kwanza nje ya , itifaki iliyozoeleka, kwa Makamu wa Rais kuwa  familia yake uwanjani kukaribisha mgeni.

Na pia ni tukio la kukumbukwa kwamba, Rais George W. Bush na Laura Bush pia walisafiri hadi uwanjani hapo kwa ajili ya kusalimiana na Papa  Francisko, wakikumbuka pia  tukio la Mstaafu Papa Benedict XVI alipotembelea nchini Marekani mwaka 2008.

Hii ni mara ya pili kwa Papa Francisko, kukutana na Rais Obama ambaye kwa mara ya  kwanza, walikutana Vatican Machi 2014.

Katika muda wa siku sita za kuwa Marekani, Papa Francisko kati ya matukio makuu, itakuwa ni pamoja na  kutembelea Ikulu ya Marekani- kuongoza Ibada ya Misa na ikiwemo ile kumtaja katika daraja la Watakatifu Mwenye Heri Padre  Junipero Serra na Ibada za masifu ya jioni ,  kukutana na Kutembelea Congress ya Marekani mjini Washington D.C , Kutembelea Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa  na Ground Zero New York na kushiriki katika Mkutano wa Dunia wa Familia huko Philadelphia. Papa atakamilisha ziara hii Marekani  siku ya Jumapili  27  Septemba 2015  








All the contents on this site are copyrighted ©.