2015-09-22 10:13:00

Papa ziarani Cuba : Ibada ya Misa mjini Holguin: neema ya Yesu hugeuza historia


Jumatatu majira ya Asubuhi, 21 Septemba, ambamo Mama Kanisa humkumbuka Mtume Mateo Mwinjilishaji, Baba Mtakatifu akiwa ziarani Cuba, aliongoza Ibada ya Misa katika Uwanja wa Mapinduzi wa mjini Holguin .

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Papa Francisco kuutembelea mji huo wa tatu kwa ukubwa nchini Cuba , ambao una historia ya mgunduzi Christopher Columbus , kutua nanga kwa mara ya kwanza mwaka 1492.

 Uwepo wa Papa Francisco katika mji huu,  ulivutia maelfu ya watu kushiriki katika Ibada ya Misa  aliyoiongoza yeye Papa katika uwanja wa mji huo. Kati ya umati wa watu waliohudhuria Ibada hii alikuwepo pia Rais Raul Castro wa Cuba.

Taarifa inasema, ilikuwa ni siku ya Kipekee kwa Papa Francisco, kutokana na jotojoto la makaribisho mazuri aliyoyapata  na hasa nyimbo nzuri  zenye mchanganyiko wa mahadhi ya Ulaya na Afrika. 

Kauli mbiu ya Papa  katika  homilia yake ililenga katika kuongolewa kwa Mtakatifu Mathayo  Mwinjilishaji ambaye awali kabla ya kukutana na Yesu , alikuwa mtoza ushuru , mtu aliyechukiwa na watu kama fisadi na msaliti. Lakini maisha yake , yalibadilishwa na Yesu. Yesu alipokutana naye Mateo alimtazama na kumpenda  mtoza ushuru huyu, na kumwambia  “Nifuate".

Papa ametazama kwa makini tukio hili na kusema macho ya Yesu yaliweza kumweka Huru Mathayo Na ndivyo inavyoweza kuwa hata kwetu. Papa alieleza na kushuhudia kwamba, ndivyo ilivyokuwa kwake yeye  Bergoglio alipokuwa kijana, Yesu alimtazama kwa macho ya huruma na kumwambia ; nifuate.   Papa  kwa kirefu alizungumzia  juu ya huruma ya Mungu yenye uwezo wa  kubadilisha historia". Yesu anamwangalia Mathayo, Mrumi  mtoza ushuru, mwenye kuonekana kwa watu wake kama fisadi na msaliti, na kumwambia nifuate.

Kumbe mtazamo wa  macho ya huruma ya Yesu; yaliufungua moyo wa Mathayo, na kuibadili tabia yake,  akamponya, akampa matumaini na maisha mapya, kama ilivyokuwa kwa Zakayo, Bartimayo, Mariamu Magdalene, Petro, na pia kwa kila mmoja wetu. Ingawa sisi hatuthubutu kuinua macho yake kwa Bwana, Yeye daima hututazama kwa macho yake ya huruma na kuona yaliyomo ndani mwetu na kutupa mwaliko wa kumfuata. Yesu anaita “Nifuate”

Yesu huwatafuta hata  wale ambao kwa wengine wanaonekana hawana stahili ya kuwa karibu na Mungu. Papa aliendelea kueleza na kuwatia moyo wote waliokuwa wakimsikiliza kwamba, Upendo wa Yesu unaendelea kuwepo kwa ajili yetu sote.  Macho yake Yesu, hutangulia kujua hata  mahitaji yetu. Yana uwezo wa kuona mbali,  mahali tunapo elemewa na dhambi  au mfadhaiko wa aibu. Na huona hata aina ya kundi la kijamii linalotuhusu.
 

Papa aliendelea kufundisha kwamba, baada ya kupokea huruma ya Mungu , na kukubali kumfuata Kristo , kinachofuatia ni kutimiza kazi zake za kitume .Kwa kuwa pamoja na Yesu , tunaachana na mzingo wa mambo ya kidunia na , fedha na starehe zake.  Jambo la kwanza inakuwa ni kutumikiana mmoja kwa mwingine. Ni kuitikia wito wa Yesu “nifuate”, kuinuka na kujitolea hata nafsi zetu katika huduma , kama ilivyokuwa kwa Mathayo,  wito wa Yesu ulimwenzesha Mathayo kuiona  furaha ya kweli katika kutumikia. Hivyo macho ya Yesu, yanaona shughuli za kimisionari ambazo ni  huduma na kujitolea. Upendo huu wa Yesu huponya mioyo yetu , na kutuhimiza kutazama zaidi tunachopaswa kutenda kwa ajili ya wengine, na si kujiondoa katika utendaji wa shughuli  hata katika masuala ya kijamii na hasa katika uwanja wa Kisiasa.

Baba Mtakatifu alieleza na kuwahoji waliokuwa wakimsikiliza iwapo wanaamini kwamba, mtoza ushuru anaweza badilika na kuwa mtumishi wote?  Na iwapo inawezekana  msaliti kuwa rafiki?  Na kama inawezekana  mwana wa seremala, kuwa  Mwana wa Mungu?  Alisema , iwapo wanasadiki katika hayo, basi pia wanaamini kwamba  Macho ya Yesu , yanayowatazama yana uwezo wa kugeuza  moyo yao. Mungu ni Baba anayetaka kutoa  ukombozi kwa wote wale wanaomkubali.  Na  Macho ya Yesu hutuongoza sisi kuishiriki huruma yake , ambayo hutolewa bure si tu kwa wagonjwa, wafungwa na wazee, lakini pia katika kila hitaji la  familia na mtu binafsi.

Papa Francisco alikamilisha homilia yake kwa kugeukia juhudi na  sadaka za Kanisa la Cuba, ambalo linafanya kazi ya kumleta kila mtu, hata walio mbali zaidi,  katika neno na uwepo wa Kristo. Papa alilitazama tatizo la uhaba wa dhamira, uhaba wa makanisa na makuhani, na mahali pa kukusanyika watu, ili watu wengi zaidi waweze kushiriki katika Ibada,  sala, kusikiliza Neno, katekesi na tafakari za maisha ya jamii. Papa aliitaja mikusanyiko hiyo kuwa ni ishara ndogo ya uwepo wa Mungu katika miji. 








All the contents on this site are copyrighted ©.