2015-08-24 15:51:00

Kanisa Ethiopia laiomba Tume ya Umoja wa Afrika kumwalika Papa Ethiopia


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Makada Yohannes, Afisa mawasiliano na mahusiano ya umma katika Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia, Kanisa Katoliki nchini Ethiopia, limeiomba Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) kumwalika  Baba Mtakatifu Francisko, atembelee Umoja wa Afrika.  Kardinali Berhaneyesus  Sourapiel, Askofu Mkuu wa Addis Ababa, na Mwenyekiti wa AMECEA, alipendekeza hilo wakati wa majadiliano ya ujumbe wa Kanisa ulipokutana na Mwenyekiti wa Tume ya AUC , Dk Dlamini Zuma Nkozasana.

Kardinali Berhaneyesus na ujumbe wake walikutana na Dk Zuma kujadili masuala yanayolenga kuimarisha uhusiano kati ya  Kanisa na Tume ya Umoja wa Afrika na  nchi. Ujumbe wa viongozi wa Kanisa Katoliki, ulikiwa pamoja na Dk Berhane Gebray ambaye ni Mwenyekiti kwa kamati ya maandalizi ya Mkutano wa 19 wa  AMECEA, mkutano utakaofanyika nchini Ethiopia mwaka 2018. Katika majadiliano yao walitoa pia mapendekezo ya jinsi AUC inavyo weza kushirikiana na Kanisa Katoliki katika maandalizi ya mkutano huo.

Kwa upande wake Dk Zuma alisema kuwa itakuwa ni heshima kubwa kumkaribisha Papa Francisko. Lakini ni lazima kufanya kazi kwa pamoja, Kanisa Katoliki nchini Ethiopia na Serikali ya Ethiopia, na  AUC  kushirikishwa  katika vikao na maandalizi yake. Ilikubaliwa kuwa kikundi cha kufuatilia hilo kitaundwa. Katika majadiliano yao pia ilikubalika kuteuliwa kwa Kasisi wa Kudumu kwa ajili ya kazi za kichungaji kwa wafanyakazi katika Ofisi za Makao Makuu ya Umoja wa Afrika. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Kardinali Berhaneyesus kuitembelea Tume ya Umoja wa Afrika , tangu alipochaguliwa kuwa Kardinali. Makeda Yonannes wa CBCE ameripoti .  

 








All the contents on this site are copyrighted ©.