(Vatican Radio) Kardinali Pietro Parolin, na Waziri Mkuu Rui Maria de Araujo, Ijumaa (14 Agosti) waliweka saini katika hati ya makubaliano ya kushirikiana katika masuala ya uhusiano wa kisheria kati ya Jimbo Takatifu na Jamhuri ya Timor ya Mashariki. Akizungumza katika hotuba baada ya kusaini mkataba huo, Kardinali Parolin, aliitaja hati waliyoweka saini kuwa ni ishara kubwa ya matunda ya mahusiano mazuri kati ya Kanisa Katoliki na Serikali ya Timor ya Mashariki. Uwekaji wa sahihi huu umekuwa ni moja ya matukio makubwa katika maadhimisho ya kupita miaka mia tano, tangu Neno la Injili lilipohubiriwa kwa mara kwanza Timor ya Mashariki. Kardinali Parolin aliteuliwa na Papa Francisco kumwakilisha katika maadhimisho haya.
Utiaji wa sahihi katika hati ya makubaliano ya ushirikiano na mshikamano wa kisheria,
ulihudhuriwa pia na Rais Taur Matan Ruak, wa Jamhuri ya Timor ya Mashariki; Vicente
Guterres, Rais wa Bunge la Taifa; na Rais wa Mahakama ya Rufaa , Guilhermino da Silva,
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje Hernani Coelho, pamoja na kundi la wabunge na maofisa
wa ngazi ya juu serikali, wanadiplomasia, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Maaskofu
wa Timor ya Mashariki.
Kardinali Parolin akitoa neno baada ya utiaji wa saini, alishukuru kwa kupata upendeleo
huo wa kuweka saini katika hati hiyo muhimu ya Mkataba kati ya Jimbo Takatifu na
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Timor ya Mashariki. Mkataba, wa kisheria utakao tumika
kama chombo cha kuongoza uhusiano kati ya Kanisa Katoliki na Serikali ya Timor ya
Mashariki, katika masuala msingi kwa ajili ya watu wapendwa wa Timor- Mashariki.
Aliitaja hati hiyo kwamba ina lengo moja tu kuu nalo ni kuwa na namna bora ya kusaidia
watu kufanikisha maendeleo endelevu kwa jumla, kimwili na kiroho.
Kardinali Parolin, alikumbusha kwamba, wote Kanisa na Serikali, uwepo wake ni ajili
ya kutumikia watu , na hivyo kwa Mkataba huu waliotia saini, unakuwa uthibitisho
unaodai uwajibikaji katika kuwatumikia watu kwa mujibu wa yaliyoandikwa katika mkataba
huo, maandishi yanayodai kushirikiana na kuheshimiana kwa ajili ya maendeleo kamili
ya watu katika haki, amani na manufaa ya wote.
Na alirejea uzoefu wa siku za nyuma , akisema daima umeonyesha, binadamu hupata huduma
iliyo bora zaidi pale kunapokuwa na ushirikiano na mazungumzo kati ya sehemu zote
za jamii na pale panapojengeka utamaduni imara wa kukutana kwa amani na kuheshimiana,
na hasa miongoni mwa viongozi.
All the contents on this site are copyrighted ©. |