2015-08-03 09:22:00

Papa : Usiogope kwenda kuungama


 Baba Mtakatifu Francisco Jumapili wakati wa sala ya Malaika wa Bwana pamoja na kutoa tafakari juu ya somo la Injili , linalomwonyesha Yesu kuwa ndiye Mkate wa Uzima , Papa  pia alikumbuka Sikukuu ya kila mwaka ya Agosti 2 ya mjini Assisi. Ni Sikukuu ya Msamaha, inayoadhimishwa  kwa lengo la kuhimiza  waamini  kuomba msamaha kwa dhambi zao kupitia njia ya Sakramenti ya Upatanisho na kupokea Komunio.

Sikukuu hii ya Msamaha yenye kuvutia Maelfu ya waamini kwenda  Assisi kila Agosti 2, ina asili kimiujiza, kwamba Yesu, Maria na malaika wengi waliomtokea  Mtakatifu Francis kwa mara nyingi ,  na Yesu aliitika ombi la Mtakatifu Francis la kupata rehema kamili, lakini  akimtaka kwanza, apate idhini ya  Papa  Honorius. Na ndivyo ilivyofanyika.  Mtakatifu Francis  wa Assisi, aliposhawishi  Papa Honorius III, kutoa rehema kamili kwa wale wote wanao tembelea kanisa kidogo linachojulikana kwa jina "Portiuncula" kila mwaka tarehe  Agosti 2 na kukiri dhambi zao.

Baba Mtakatifu Francisco amelitafakari tukio hili na kutoa maelezo kwamba, Sikukuu  hii ni wito wa nguvu unaodai  kumkaribia Bwana kupitia  sakramenti ya upatanisho ambayo pia tunaweza ita sakramenti ya kupokea Ushirika," Papa alisema.


Baba Mtakatifu aliendelea kusema kwamba, kuna baadhi ya watu wenye kuhofu kumkaribia Kristo na kukiri dhambi zao. Watu hao wanasahau kwamba, Yesu si hakimu dhalimu lakini  badala ya Baba mwenye huruma kubwa.  Na ni kweli kwamba , wakati tunapokwenda kuungama tunashikwa na mfadhaiko wa aibu kidogo na hili humtokea kila mmoja . Lakini aibu tunayoisikia ndani mwetu inaweza kuwa sehemu neema za maandalizi ya  kutubu dhambi tulizo nazo . Hutuandaa kwenda kukumbatiwa na Baba, ambaye mara zote husamehe  na daima husamehe  kila kitu.

Baba Mtakatifu Francisko wakati huo wa sala ya Malaika wa Bwana, akirejea somo la Injili ya Jumapili, alisistiza pia kuwa na utambuzi kwamba ,licha ya juhudi za kutafuta mahitaji ya mwili, pia tunapaswa kuweka jitihada zaidi katika kutafuta yanayokidhi mahitaji ya kiroho, kwa kuwa   tunahitaji uwepo wa Mungu katika maisha yetu ya kila siku. Papa alieleza hivyo akirejea jinsi watu  walivyomfuata Yesu , baada ya  tukio la kuzindisha mikate na samaki. Yesu alitoweka  na watu walianza kumtafuta na hatimaye kukutana naye huko Kapernaumu.  Yesu alielewa sababu ya shauku ya  watu hao kumtafuta kwa bidii, kwamba ilikuwa ni kwa mahitaji yao ya kimwili, na si kwa mahitaji ya kiroho. Aliwaambia wazi kuwa wanamtafuta si  kwa kuwa waliona ishara, ila kwa kuwa walikula ile mikate na kushiba" (Yohana 6: 26). 

Papa alitoa wito kwa watu wote kwamba tunahitaji uwepo wa Mungu katika maisha yetu ya kila siku. Kila siku tunahitaji kumkaribia Mungu na kumweka ndani mwetu kupitia Sakramenti ya Ekaristi ambamo tunakutana na Yesu, aliye Mkate wa uzima. 








All the contents on this site are copyrighted ©.