2015-08-02 15:18:00

Wito: Washirikisheni zaidi waamini walei tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu!


Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S linaadhimisha Jubilei ya miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Shirika hili. Katika mchakato wa maadhimisho haya, Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania hapo tarehe 8 Agosti 2015 litapandishwa hadhi na kuwa ni Kanda inayojitegemea kwa: uongozi, rasilimali watu na fedha. Wakati wa maadhimisho haya, mahujaji 54 kutoka Tanzania walishiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Shirika katika ngazi ya kimataifa, mjini Roma.

Katika mhojiano maalum na Radio Vatican Mama Magret Ikongo, mwamini mlei kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam anasema ameguswa kwa namna ya pekee na jinsi ambavyo tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu ilivyoenea sehemu mbali mbali za dunia, kazi kubwa iliyofanywa na Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu. Hili ni Shirika ambalo limejipambanua kwa kwenda pembezoni mwa jamii, ili kuwatangazia watu Njema ya Wokovu sanjari na kujikita katika Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Mama Ikongo anasema, huduma mbali mbali zinazotolewa na Shirika katika kuwahudumia wagonjwa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama inavyojionesha kwenye Hospitali ya Mtakatifu Gaspar ni jambo la kumshukuru Mungu. Hospitali hii ni kubwa na inatoa huduma makini kwa wagonjwa ndani na nje ya mkoa wa Singida. Wamissionari wamekuwa pia mstari wa mbele katika kuwahudumia watoto walioathirika kwa ugonjwa wa Ukimwi, kama ilivyo katika Kijiji cha Matumaini, ambacho kweli kimekuwa ni kielelezo cha upendo unaoponya kutoka familia.

C.PP.S wamekuwa ni wadau wakubwa katika utoaji wa huduma ya maji na kwamba, kwa miaka mingi watoa huduma hii eneo la Kanda ya Kati. Wanaendelea pia kutoa elimu makini kwa watoto wa maskini pamoja na kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri wenyewe kwa njia ya shule za ufundi huko Mtongani, Dar es Salaam na Manyoni, Singida. Shughuli zote hizi ni sehemu ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Wamissionari wa damu Azizi ya Yesu wanatekeleza dhamana na utume wao Jimbo kuu la Dar es Salaam, Morogoro, Jimbo kuu la Dodoma, Ifakara na Singida.

Mama Ikongo kwa namna ya pekee, anawataka Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu kuhakikisha kwamba, wanakuza na kuiendeleza tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu kwa kuwawezesha waamini walei, ili iwasaidie katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Shirika linapopandishwa hadhi na kuwa Kanda kamili, ni mwaliko wa kujifunga kibwebwe katika masuala ya rasilimali watu, fedha na vitu, ili kuhakikisha kwamba, huduma inaendelea na kuboreshwa zaidi. Kujitegemea kuna dhamana na changamoto zake.

Mama magret Ikongo anaialika Familia ya Mungu nchini Tanzania kushikamana na Wamissionari hawa katika maisha na utume wao kwa ajili ya Kanisa nchini Tanzania, ili siku moja, watanzania waweze kuadhimisha Jubilei ya miaka 200 ya Uwepo wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.