2015-08-02 11:48:00

Wanasema "Mang'ana Gasarikiri" Hali ya hewa imechafuka!


Tafakari ya Neno la Mungu, Injili ya Jumapili ya 20 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa inaongozwa na Injili kama ilivyoandikwa na Yoh. 6: 51-58. Katika nchi yenye vyama vingi vya siasa, wagombea kiti cha urais wanatoka ndani ya chama kimojawapo. Yawezekana pia mgombea urais akawa mgombe binafsi asiye na chama. Mgombea binafsi anakuwa na kazi nzito sana ya kuhakikisha na kuwadhihirishia watu kuwa sera zake zinakidhi mahitaji ya wananchi wote. Kadhalika wananchi yabidi wamwamini sana waweze kumchagua.

Katika Injili tunamkuta Yesu kama mgombea binafsi anayejinadi mwenyewe kama sera na anataka kuchaguliwa yeye mwenyewe kama alivyo na kumwiga maisha yake. Hebu tufuatilie kampeni zake. Wiki iliyopita Wayahudi “Walimnung’unika Yesu” kwa sababu alisema “Mimi ni chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni” yaani Wayahudi walitafuta mashabiki wenzao wajiunge nao ili kuzikataa sera za Yesu kuhusu mkate. Leo tunasikia kuwa Wayahudi hao, wamegawanyika: “Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, ‘Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule?” Wayahudi wanatofuatiana wenyewe kwa wenyewe juu ya kumla Yesu.

Ndugu zangu hata sisi tunaweza kushindana au kujadiliana na wale wanaotupendekezea vyakula vyenye kiwango kitakiwacho na vile vilivyo feki (visivyokidhi kiwango). Yaani, tunafahamu kwamba mkate wa hekima ya ulimwengu huu hauyeyuki na hivi hautufai kwa afya zetu ni tofauti na Hekima ya Kristo iliyo mkate unaoyeyuka na kujenga mwili kwa kuupatia sia bora na yenye nguvu!

Kula maana yake kutafuna, kumeza, kuyeyusha hekima ya Mungu na kuiacha itugeuze tuwe na utu wa Mwana wa Mungu. “Mimi ni chakula chenye uzima kilichosuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa aili ya uzima wa ulimwengu.” (Yoh. 6:51). Hapa tendo la “kuamini” linafifia, na linapisha nafasi yake tendo la kula linalotokea mara kumi na moja, na linaingia neno “kutafuna” kwa nguvu zaidi halafu mara tatu tunaliona neno “kunywa.” 

Wayahudi walidadisi: “Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule?” Kwa sababu “mtu akishakula chakula, anabadilika afya yake anageuka na kuwa kile alichokula,” hivi anayekula ujumbe wa maisha ya Yesu atageuka kuwa kama Yesu. Hapa Wayahudi wameelewa kwamba mkate anaosema Yesu unamaanisha Neno na Hekima ya Mungu iliyojimwilisha katika Nafsi ya Yesu.

Mbaya zaidi anaposema: “Msipotafuna nyama ya Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu.” Kwa Wayahudi damu ilitumika kwa ajili ya kufanya maagano na Mungu, ilikuwa ni kielelezo cha uhai na kifo. Mathalani chini ya mlima Sinai Musa alinyunyiza damu ya wanyama altareni na nyingine aliwanyunyizia Waisraeli. Damu ni alama ya muungano wa  Mungu na mtu kuwa kitu kimoja. Kwa hiyo kula mkate na kunywa damu maana yake kuwa na maisha na Kristo “kuchanjiana damu na Kristo.”Kabla yake Yesu alisema: “Anayeamini ana uzima wa milele,” akimaanisha kugeuza mapendekezo na ujume wa Yesu kuwa wako, yaani mmoja akiamini Neno lake (Injili) atakuwa na uzima wa milele.

Lakini leo Yesu anaongeza kusema: “yabidi kutafuna nyama na kuinywa damu yake, yaani kupokea Ekaristi Takatifu. Ekaristi haina maana ya kummiliki au kumtamalaki Yesu, bali ni kumla na kumtafuna. Kutafuna vizuri chakula ili kipate kuyeyuka mwilini. Kwa hiyo madhehebu ya Ekaristi ni sawa na ndoa takatifu inayofanyika baada ya wachumba kuelewana na kuamua kuoa. Kama madhehebu ya karamu ya mwisho ambapo “Yesu alitwaa mkate, akashukuru, akaumega akawapa wafuasi akisema: Twaeni mle huu ni mwili wangu. Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi.” Yesu anataka kutuambia kuwa baada ya kuelewa ujumbe wa maisha ya ubinadamu wangu, katika umbo (alama) hili la mkate wa Ekaristi ambako ni nafsi ya maisha yangu yote ya upendo myapokee myatafune na myayeyushe. Tendo la kumla na kumnywa linaonesha muunganiko kama wa kindoa na nafsi ya Kristu na kuwa kitu kimoja naye aliye uzima kamili. Tukiungana naye tutakuwa zawadi kamili ya upendo.

Kisha anaendelea kusema: “anayeutafuna mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake,” yaani kutakuwa na mahusiano ya undani yanayodumu. “Mimi nitakuwa Mungu wenu” tena “Mimi ni wake mpendwa wangu.” (Wim. 7:10).

Tamko gumu zaidi ni hili: “Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunitafutana atakuwa hai kwa mimi.” Kwamba Yesu ametokana na Mungu, ni picha ya Mungu kamili. Yesu hapa anaingia katika maungano na mahusiano na binadamu kwa njia ya sisi. Mapato ya kumtafuna ni kukaa ndani yake naye ndani yetu. Huo siyo uchawi bali ni umoja wa upendo. Kama Paulo anavyowaandikia Wagalatia “Siyo mimi bali Yesu anayeishi katika mimi.”

Yesu anarudia mara nane kutoa hoja kwamba tule nyama yake ili tuweze kuishi: “Anayekula nyama yangu anaishi milele.” Msisitizo upo wakati wa sasa na siyo uzima ujao. “Anayetafuna nyama yangu na kunywa damu yangu anao uzima wa milele.” Uzima huo wa milele au unaodumu siyo kama pesa za kiinua mgongo, unazoziwekeza mwenyewe kwa ajili ya uzeeni, au matendo mema yatakayokulipa uzeeni, la hasha, bali maisha ya kweli, ya hakika, yaliyoko sasa.

Yesu anasema: chukueni ubinadamu wangu, utu wangu na uwepo wangu kuwa chachu yenu. Binadamu ni kiumbe pekee aliye na Mungu ndani ya damu na ya pumzi yake. Kwa hiyo Yesu siyo suala gumu lisilowezekanika kujilinganisha nalo, bali lipo ndani mwangu mimi mwenyewe kabisa, ni chemchemu, ni msukumo wa kuelekea kwenye mwanga mwangavu wa maisha.

Kumla na kumnywa Kristu siyo tu kumpokea katika komunio ya misa takatifu, bali ni kuungana na siri ya uwepo wake wa fumbo, yaani, upendo wake unaoenda hadi Msalabani ambako mwili wake unapigiliwa misumali, hadi kutoka damu. Wakati wa Misa Takatifu Altareni kuna hostia ndogo tu nyeupe isiyotiwa chachu, tena haina radha, imetulia kimya kabisa. Hostia hiyo ndogo haina zaidi isipokuwa inaniunganisha mimi na Mwenyezi Mungu.

Tunaweza kuelewa vizuri zaidi muuganiko huo tukiyatafakari maneno ya wimbo wa majitoleo wanayoimba watawa wabenediktini wakati wanafunga nadhiri zao: “Unipokee ee Bwana kama ulivyoahidi nami nitaishi!” Kuishi na Mungu ndilo jambo la msingi, na siyo kuishi baada ya maisha haya, bali kuanzia sasa. Hii ndiyo tamati ya historia. Mungu amejimwilisha, amekuwa mtu ili mtu awe Mungu. “Anayekula nyama yangu na kunywa damu yangu, anaishi ndani yangu.” Hili ni jambo zuri. Wanaopendana wanaalikana nyumbani: “Ujisikie nyumbani.” Ndivyo anavyotuambia Mungu. Mioyo yetu ikiwa ndani yake itajisikia nyumbani. Ninammeza Kristo, ninapumua Injili ninabadilika na nimejikristisha na Kristo.

Na padre Alcuin Nyirenda. OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.