2015-08-02 10:28:00

Rehema kamili kutolewa wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu


Mpendwa Msikilizaji wa Kipindi cha Hazina yetu, tunakusalimu kwa mara nyingine tena na kukukaribisha katika kipindi chetu tuendelee kuandaliwa vema katika kuupokea na kuuishi Mwaka mtakatifu wa Jubilei kuu ya Huruma ya Mungu utakaozinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko hivi Karibuni mjini Vatican. Katika kipindi kilichopita tuliangazia kwa uchache kuhusu hija katika Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, na leo kama tulivyokuahidi mpendwa msikilizaji, tuhekimishane kwa ufupi juu ya rehema kamili.

Kanisa kwa mamlaka halali iliyowekwa, huweza kutoa nafasi za rehema kamili, kwa waamini wake.  Hili ni moja kati ya mambo yanayofumbatwa katika mpango mzima wa Ukombozi wa Mwanadamu, na Kanisa lenyewe kama Sakramenti ya Jumla ya Ukombozi, linazo nyenzo mbalimbali, kama vile Nno, Sakramenti na Visakramenti, Rehema Kamili ikiwa ni mmoja ya nyezo za kumfikishia mwanadamu ukombozi.

Katekisimu ya Kanisa Katoliki (n.1471), mintarafu rehema kamili inatuelewesha kwamba: Rehema ni msamaha mbele ya Mungu ambao kosa lake lilikwishwafutwa, msamaha ambao Mkristo mwamini aliyejiweka vizuri huupata  kutoka katika hazina ya malipizi ya Kristo na ya Watakatifu.

Rehema inaweza kuwa ya muda au Kamili. Rehema ya muda huondoa sehemu ya adhabu ya adhabu za dhambi na rehema kamili huondoa adhabu zote (Rej. KKK, n1472). Mkristo huweza kupata rehema kamili kwa ajili yake yeye mwenyewe au kwa ajili ya marehemu kama atatimiza yafuatayo. Mosi, awe na nia thabiti ya kupata rehema katika kipindi kilichopangwa, pili akokee sakramenti ya Upatanisho (Kitubio), tatu, Apokee Ekaristi Takatifu siku hiyo ya kutolewa rehema kamili, nne; asali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu na tano atembelee Kanisa au Kituo maalumu kilichotengwa kwa ajili ya kupatiwa rehema Kamili.

Mpendwa Msikilizaji hayo matajwa hapo juu ndiyo mapaswa kwa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, tutakumbuka kwamba Baba Mtakatifu katika mafundisho yake amekanyaga humo humo, akituhimiza kufanya toba, kujipatanisha na Mungu na jirani zetu ili tujichotee neema tele. Katika Mwaka wetu huo wa Jubilei, tutajaaliwa pia Rehema kamili. Anasema Baba Mtakatifu, desturi hii itatwaa maana nzito zaidi katika  mwaka huo Mtakatifu wa huruma ya Mungu.

Msamaha wa Mungu hauna mipaka. Katika kifo na ufufuko wa Yesu Kristo, Mungu anadhihirisha wazi zaidi upendo wake na uwezo wake wa kuangamiza dhambi zote za mwanadamu. Upatanisho na Mungu umewezekanishwa  kwa njia ya fumbo la Pasaka na kwa njia ya Kanisa. Hivyo Mungu daima yupo tayari kusamehe, na hachoki kutusamehe katika njia ambazo ni mpya na za kutushangaza. Hata hivyo, sote twajua hali halisi kuhusu dhambi. Tunajua kwamba tumeitwa kuwa watakatifu (rej. Mt 5:48), lakini bado tunaonja uzito wa mzigo wa dhambi.

Pamoja na kwamba tuonaonja nguvu ya neema inayotugeuza rohoni, tunaonja pia madhara ya dhambi zetu. Pamoja na kuwa tumesamehewa, madhara ya dhambi zetu hubaki. Katika Sakramenti ya Upatanisho, Mungu hutusamehe dhambi zetu, ambazo kwa kweli huzifuta kabisa; lakini dhambi bado huacha madhara hasi katika namna yetu ya kufikiri na kutenda. Lakini huruma ya Mungu ina nguvu kuliko madhara hayo.

Kwa njia ya Mchumba wa Kristo yaani Kanisa, rehema ya Mungu  humfikia mdhambi aliyesamehewa, na inamlegezea vifungo vyote vilivyobakia kutokana na madhara ya dhambi, na hivyo kumwezesha kutenda kwa upendo, kukua katika upendo kuliko kudondoka tena dhambini.

Kanisa linaishi ndani ya Jumuiya ya watakatifu. Katika Ekaristi, ushirika huu ambao ni zawadi kutoka kwa Mungu, hugeuka kuwa ni muungano wa kiroho unaotuunganisha na watakatifu na wenye heri wote, ambao namba yao haihesabiki (rej Uf. 7:4). Utakatifu wao unatusaidia sisi katika udhaifu wetu,. Na pia unalisaidia Kanisa kwa njia ya sala zake za kimama na kwa njia ya maisha yake, liweze kuwaimarisha wadhaifu kwa njia ya nguvu yaw engine.

Hivyo, anasema Baba Mtakatifu, kuishi rehema kamili katika Mwaka Mtakatifu ina maana kukaribia huruma ya Mungu kwa uhakika kwamba msamaha wake unaelekezwa kwa maisha mazima ya mwamini. Kupata rehema kamili ni kuonja utakatifu wa kanisa, unaowajaalia wote matunda ya ukombozi ya Kristo., ili Upendo wa Mungu na msamaha upelekwe kila mahali.  Anamalizia Baba Mtakatifu kwa kusema “na tuuishi mwaka huo wa Jubilei kwa ukamilifu wote, huku tukimwomba Mungu atusamehe dhambi zetu, na atuogeshe katika kisima chake cha rehema”.

Mpendwa msikilizaji, mwaka mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, unatuletea mambo mazito mazito. Zaidi ni kwamba, huruma ya Mungu inavuka kabisa mipaka ya Kanisa. Inaelekezwa pia hata kwa Dini nyinginezo. Mintarafu hili, usipitwe, tusikilizane kipindi kijacho wakati kama huu.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.