2015-08-02 15:09:00

Jiandaeni kukabiliana na changamoto za Uinjilishaji kwa nyakati hizi!


Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye pia ni Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari katika mahojiano maalum na Radio Vatican kuhusiana na maadhimisho ya Jubilei ya miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Wamissionari wa damu Azizi ya Yesu anakaza kusema, kuna changamoto mbali mbali ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi, ili Injili ya Furaha iweze kuwafikia watu wengi zaidi.

Kuna mabadiliko makubwa ya watu, mazingira, tamadunia, vipaumbele; mambo ambayo yanahitaji mbinu na mikakati mipya ili kweli watu waweze kuguswa na Habari Njema ya Wokovu, ndiyo maana Kanisa kwa sasa linajikita katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, ili kuweza kuwatangazia watu wa nyakati hizi, Habari Njema ya Wokovu.

Kuna uhaba mkubwa wa miito ya Kipadre na Kitawa katika baadhi ya maeneo. Hapa Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu hawana budi kuhakikisha kwamba, wanawekeza katika malezi na majiundo ya wanashirika wapya watakaokuwa tayari kujitosa kimasomaso kuwatangazia watu huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.  Wamissionari wawe ni wajumbe na vyombo vya upatanisho kwa kujikita katika Mwaka wa Upatanisho uliozinduliwa kwa Kanisa Barani Afrika, unaoadhimishwa sanjari na Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu.

Fumbo la Pasaka liwasaidie watu kuonja huruma ya Mungu na liwahamasishe Wamissionari wenyewe kutoka kifua mbele kwa ajili ya kuwatangazia watu Injili ya Upatanisho, ili kuponya na kuganga madonda yanayoendelea kumsibu mwanadamu kwa nyakati hizi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.