2015-08-02 09:24:00

Huruma inayoambata haki ni chemchemi ya toba na wongofu wa ndani!


Mpendwa Msikilizaji wa kipindi chetu hekimishi cha Hazina yetu, tunakusalimu kutoka Studio za Radio Vatican. Karibu tuendelee kuisikia sauti ya mama Kanisa, anayetuandaa wakati huu ili kuupokea Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya Huruma ya Mungu. Kukumbusha tu mpendwa msikilizaji, kwa wakati huu tunaendelea kuuchambua waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, ujulikanao kama Misericordiae vultus, yaani uso wa huruma, ambao ndanimwe umesheheni, mafundisho, maelekezo na malengo mintarafu mwaka mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu.

Lengo letu: tuelewe vema maana na malengo ya mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, ili utakapozinduliwa hapo tarehe ya 8.12.2015, sote kwa moyo mmoja na nia mmoja tuuishi vema huku tukiwa tayari kuguswa na huruma ya Mungu na sisi wenyewe kutoka kwenda kuitangaza na kuipeleka huruma hiyo ya Mungu kwa watu, huruma inayomwilishika katika matendo ya huruma ya kiroho na kimwili.

Tutakumbuka kwamba, katika mafundisho yake, ndani ya Misericordiae vultus, Baba Mtakatifu anatualika sote kujibidisha sana kuyaishi matendo ya saba ya huruma ya kimwili na yale saba ya kiroho. Kuiishi huruma ya Mungu, siyo tu jambo la kulitamkatamka au kulitungia nyimbo, bali ni jambo la kulitekeleza kwa matendo halisia. Na utekelezaji wa matendo ya huruma hayo, ni vema yakafanywa kwa unyenyekevu na uadilifu, bila kujitafutia sifa binafsi au faida fulani.

Mara nyingi, tumesaliti upendo wetu kwa watu, pale ambapo tunawatendea mambo mema kwa mfumo wa matendo ya huruma, na kisha tunawatangaza, ili tujulikane kuwa ni sisi ndiyo tuliowasaidia. Wakati mwingine, tunapenda kutenda matendo ya huruma mbele za watu wengi, huku tukishuhudiwa na vyombo vya habari na kushangiliwa na magazeti, na kuchambuliwa na mitandao ya kijamii ya kuwa sisi ndiyo watu wema tunaosaidia watu!! Kufanya hivyo, ni kuhaini unadhifu wa matendo ya huruma na upendo. Kristo Bwana alitufundisha, mwenye huyaona hayo yote ni Mungu peke yake, naye ndiye mwenue kutoa thawabu; kwa sababu yeye ni Mungu wa haki, huruma na mapendo.

Katika kipindi kilichopita, kwa njia ya kinywa cha Nabii Hosea, Mungu wetu amejidhihirisha kama Mungu wa haki na huruma; Mungu mwenye uwezo wa kuizuia hasira yake, lakini hawezi kujizuia kuhurumia. Na Baba Mtakatifu Fransisko anasema, kama Mungu angekosa kuwa na huruma, basi angekuwa sawa tu na wanadamu ambao wanashinikiza haki yenye msingi katika utii kwa sheria zaidi kuliko huruma.

Ni kwa njia ya huruma yake, Mungu hutusamehe makosa yetu, na ndiyo maana Yeye huvuka ngambo ya haki kwa njia ya msamaha wake. Lakini hapo Baba Mtakatifu anafafanua akisema, huruma ya Mungu haimaanishi kwamba haki inapunguzwa thamani yake au inafanywa kuwa ni kitu cha ziada. Kinyume chake, kila afanyaye makosa lazima alipe fidia. Maana yake, wote wanaoadhibiwa kwa sababu ya makosa yao, hupewa nafasi ya huruma ili kuweza kuanza safari ya uongofu.

Anakaza kusema, adhabu ni mwanzo tu wa uongofu na sio mwisho wake, kwa sababu hapo ndipo mtu huanza kuonja wema na huruma ya Mungu. Mungu haikani haki; bali huifunga vizuri na kuiendeleza kwa tendo kubwa zaidi ambamo tunaonja upendo kama msingi wa haki ya kweli. Kama tunataka kujizuia kurudia kufanya makosa yaleyale, lazima tuwe makini sana na maneno anayoyasema Mtume Paulo  alipowarudi Wayahudi wa nyakati zake akisema “kwa kuwa wajinga kuhusu haki itokayo kwa Mungu, na  kutafuta kujijenga wao wenyewe, hawakujiweka chini ya haki ya Mungu. Kwa maana Kristo ni utimilifu wa sheria, ambayo kwayo kila mwenye kusadiki aweze kuhesabiwa haki” (Rum 10:3-4).

Haki ya Mungu ni huruma yake anayoitoa kwa kila mmoja kama neema zinazobubujika kutokana na kifo na ufufuko wa Kristo. Hivyo Msalaba wa Kristo ni hukumu ya Mungu kwetu sisi sote  na kwa ulimwengu mzima, kwa sababu kwa njia yake anatupatia uhakina wa upendo na maisha mapya.

Mpendwa msikilizaji, mwaliko hapa ni kujitahidi zaidi kuikuza huruma kuliko kuzingatia haki peke yake. Si mara chache, watu wameteswa sana kwa kulazimishwa tu kufuata sheria zisizokuwa na huruma. Kwa njia hiyo kuna watu wamedhalilishwa utu wao, wamepokwa matumaini yao. Huruma inamjali mtu katika uhalisia wake. Lakini kama asemavyo Baba Mtakatifu, kuwa na huruma haimaanishi kwamba haki iwekwe kando, hasha.

Neno hili linasisitizwa ili kukwepa kishawishi cha kubweteka na kutenda kila aina ya vitimbwi na kudai kuhurumiwa. Huruma haiondoi kuwajibishwa pale ambapo tunakengeuka katika jamii. Ndiyo maana Baba Mtakatifu anasema, kuwajibishwa huko ndiyo haswa mwanzo wa kuongoka. Kumbe, haki yenye huruma, ndiyo njia ya uongofu wetu.

Kwa leo sina la ziada, tusikilizane tena kipindi kijacho. Kutoka katika studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB








All the contents on this site are copyrighted ©.