2015-08-02 08:45:00

Haki na huruma huzaa mapendo ya dhati!


Mpendwa msikilizaji wa Kipindi cha hazina yetu tunakusalimu kutoka katika Studio za Radio Vatican. Baraka ya Kristo aliye Tumaini letu ikufikie wewe mpendwa msikilizaji hapo ulipo pamoja na watu wote ulimwenguni. Kukukumbusha tu, kwa wakati huu tunaupitia Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Fransisko ujulikanao kwa jina la Misericordiae vultus, yaani uso wa huruma. Waraka huu ni maalumu kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, itakayozinduliwa rasmi hapo tarehe 8 Desemba 2015, katika sherehe ya Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili.

Baba Mtakatifu Francisko anaamini kwa dhati kwamba kwa nyakati zetu hizi, Familia ya mwanadamu inahitaji zaidi na zaidi huruma ya Mungu. Fujo zote, na vilio tulivyonavyo ulimwenguni humu kwa ngazi na viwango vyote; vitazimishwa kwa huruma ya Mungu peke yake. Ndiyo maana analialika Kanisa kuhubiri na kuishi huruma ya Mungu na sisi waamini na watu wote wenye mapenzi mema tunaalikwa kuichuchumilia huruma ya Mungu. Tuguswe na huruma ya Mungu, na huruma hiyo hiyo ya Mungu itusaidie tutoke kifua mbele, macho mbele tuwaendee na tuwafikie wenzetu tukawaonjeshe huruma ya Mungu inayomwilika katika matendo ya huruma na upendo ya kiroho na kimwili.

Hakika, yeye mwenyewe alisema “Kanisa litarajie kufanya mambo makubwa huku likijibidisha kurudi katika misingi”. Tufungue mioyo yetu, akili zetu na nafsi zetu nzima, tuupokee mwaka huo Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu ambao unatuletea changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuiishi vema imani yetu.

Pamoja nayo, Baba Mtakatifu anaendelea kututafakarisha, tujaribu kuweka ulinganifu kati ya haki na huruma. Haya si mambo mawili yanayopingana, bali ni kama pande mbili za shilingi, ambazo zinajipambanua polepole hadi zinafikia utimilifu wa upendo. Haki na huruma huzaa upendo. Haki ni dhana msingi kabisa katika jamii ya watu ambayo inaongozwa kwa utawala wa sheria. Haki inaeleweka pia kama kile anachostahili mtu kihalali. Katika Biblia, kuna nukuu nyingi sana zinazohusu haki ya kimungu na kwa Mungu kama Hakimu. Katika nukuu hizo, haki inaeleweka kama uzingatiaji mkamilifu wa Sheria ya Mungu na tabia ya kila Mwisraeli kwa kufuatana na Amri za Mungu.

Hata hivyo, mtazamo huo  mara nyingi umetupeleka katika mfumo-sheria kwa kuharibu maana asilia ya haki na kufunika thamani yake msingi. Ili kukwepa mtizamo huo wa mfumo-sheria, tunahitaji kukumbuka kwamba, katika maandiko matakatifu, haki inaeleweka kimsingi kama kujiweka  katika mapenzi ya Mungu.

Kwa upande wake, Kristo anaongea mara nyingi juu ya umuhimu wa imani zaidi ya ufuataji tu wa sheria. Ni katika mtazamo huu tunapaswa kuelewa maneno yake wakati alipokuwa mezani pamoja na Matayo na watoza ushuru wengine pamoja na wadhambi, anawaambia Wafarisayo waliokuwa wakimpinga, akiwaambia “Nendeni mkajifunze maana ya maneno haya, nataka rehema na wala si sadaka. Sikuja kuwaita watu wema bali wenye dhambi” (Mt.  9:13).

Kwa kuwa na mtazamo wa haki kama tu mtindo wa kufuata sheria ambapo watu huhukumiwa kwa kugawanywa katika makunndi mawili yaani ya wenye haki na wadhambi; Kristo ameelekea kuipambanua dhana pana zaidi ya haki ambapo mdhambi wadhambi hutafutwa na kujaaliwa msamaha na wokovu.

Hapo tunaweza kuona jinsi ambavyo mtazamo huu wa kiukombozi wa huruma kama chanzo cha maisha mapya, ulimfanya Yesu akataliwe na Mafarisayo na waalimu wengine wa sheria. Kwa kujaribu kubaki waaminifu kwa sheria walikuwa wakiweka mizigo mizito mno mabegani mwa wengine na huku wakiipuuza huruma ya Mungu.

Mwaliko wa kufuata sheria usiwafanye watu kusahau mambo yanayogusa utu na heshima ya binadamu.

Mwaliko anaouleta Kristo katika andiko tulilolinukuu hapo juu, ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Hosea asemapo “nataka upendo na sio sadaka” (Hos 6:6).  Yesu anathibitisha kwamba, kutoka wakati ule na kuendelea, utaratibu wa maisha kwa wafuasi wake lazima uweke huruma kama nguzo msingi, kama Kristo mwenyewe alivyoonesha kwa kula chakula pamoja na wadhambi. Huruma hapa kwa mara nyingine tena inadhihirishwa kama dhana msingi ya utume wa Yesu.

Hali hiyo ilikuwa changamoto kubwa sana kwa wasikilizaji wake ambao walitenganisha kati ya huruma na haki kwa kigezo cha sheria. Yesu kwa upande mwingine anakwenda ng’ambo zaidi ya sheria. Kwa kuambatana na wale ambao sheria iliwahukumu kuwa ni wadhambi kunatufanya sisi tung’amue undani wa huruma yake. Ni huruma hiyo ndiyo inayotuinua na kututegemeza sisi katika unyonge wetu, ndiyo maana tunaalikwa sana, kuikimbilia huruma ya Mungu daima, huku tukijibidisha kuiishi vema na kuwapelekea wenzetu ujumbe wa huruma ya Mungu.

Tunahitimisha kipindi chetu kwa leo kwa kusema ‘huruma ya Mungu ndiyo wimbo haswa wa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei’. Tusikilizane tena wakati mwingine. Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.