2015-07-31 07:47:00

Mwimbieni Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kutunza vyema mazingira!


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume kuhusu utunzaji bora wa mazingira, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji bora wa nyumba ya wote” anabainisha mambo msingi yanayojikita katika maisha ya kawaida, lakini yakipewa kipaumbele cha kwanza ni msaada mkubwa katika utunzaji bora wa mazingira. Wananchi wajifunze kutunza mazingira kwa kukusanya taka katika mazingira yao; kwa kudhibiti matumizi ya maji, gesi na umeme wa majumbani pamoja na kulinda kile kidogo ambacho mtu amekipata kwa jasho kubwa.

Haya ni maneno ya Kardinali Francesco Coccopalmerio, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Nyaraka za Sheria anapofanya tafakari kuhusu Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Binadamu atambue kwamba, amekabidhiwa dunia ili aweze kuilinda, kuitunza na kuindeleza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya kizazi cha sasa na kile kijacho. Kumbe, hapa kuna haja ya kuwa waangalifu na wakarimu kwa nyumba inayotoa hifadhi ya maisha ya binadamu, yaani mazingira. Mwanadamu anapochafua na kuharibu mazingira, athari zake ni kubwa kwa viumbe vyote vinavyohifadhiwa katika nyumba hii, yaani mazingira.

Kardinali Coccopalmerio anasikitika kusema kwamba, mwanadamu kutokana na kuelemewa na ubinafsi, uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka amejikuta akichangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira na matokeo yake ni athari kubwa zinazoendelea kujionesha katika mabadiliko ya tabianchi. Hapa kuna haja ya kuwa na sera na mikakati itakayosaidia mchakato wa maboresho ya mazingira, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pakuishi.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujifunga mkanda ili kutoa sadaka kwa kuondokana na uchoyo na badala yake, watu wajenge na kudumisha moyo wa upendo na mshikamano; badala ya kutupa na kuharibu chakula, watu wajenge utamaduni wa kushirikishana na kugawana rasilimali ya dunia.

Dunia inahitaji kujikita katika mshikamano wa kimataifa, ili kukabiliana kikamilifu na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika maisha ya mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Hii ni changamoto kubwa ya utunzaji wa mazingira pamoja na mshikamano na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kumwilisha haki jamii. Maskini ni wale ambao wanateseka sana kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kuna baadhi ya viumbe vinatoweka na wala havitaonekana tena katika historia ya binadamu na kwamba, kuna baadhi ya maeneo ambayo watu wanavuna rasilimali ya dunia hii kwa uchoyo kiasi kwamba, baada ya miaka michache kutakuwa ni mashimo ya machimbo ya madini na maeneo ya jangwa, kwani watu wamevuna misitu kwa fujo na ubinafsi. Mbaya zaidi kutokana na majanga asilia, watu wanalazimika kuyakimbia makazi na nchi zao, wakiwa njiani wanakumbana uso kwa uso na kifo! Kumbe, utekelezaji wa mambo madogo madogo unaweza kusaidia sana katika kuboresha mchakato wa utunzaji bora wa mazingira na wala si kusubiri mambo makubwa!

Kila mtu atende kadiri ya uwezo na nafasi yake. Ni dhamana ambayo inawahusisha viongozi wa Serikali, wanasiasa na watunga sera, ili kwa pamoja  jamii iweze kujielekeza katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Kardinali Francesco Coccopalmerio amekazia dhana ya utekelezaji wa changamoto zinazotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hapa kuna haja ya kuona, kutambua, kuwajibika na kutenda kwa kumwilisha mambo haya katika uhalisia wa maisha.

Wakati huu ambapo kuna watu wengi hususan kwenye Nchi za Ulaya wako kwenye kipindi cha likizo ya kiangazi, ni nafasi ya kugusa kwa karibu zaidi uzuri na utakatifu wa mazingira, iwe ni fursa ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani na sifa, inayomkumbusha mwanadamu kwamba, ana dhamana ya kulinda na kuendeleza mazingira kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Hapa kuna haja ya kujikita katika toba na wongofu wa kiekolojia, ili kuwa makini na kujikita katika utunzaji bora wa mazingira.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.