2015-07-30 14:51:00

Mawasiliano yenye mashiko na mvuto!


Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwashangaza wengi kwa mtindo wake wa mawasiliano ya kijamii unaojikita zaidi katika fasihi simulizi, yenye mvuto na mashiko katika maisha ya watu. Baba Mtakatifu anajisikia kuwa ni kati ya “Vijana wa zamani” ambao wanaendelea kuchechemea katika matumizi ya mitandao ya kijamii inayochangamkiwa na vijana wa kizazi kipya.

Baba Mtakatifu anatambua uwezo na mapungufu yake katika matumizi ya mitandao ya kijamii kama alivyokiri mwenyewe hivi karibuni wakati akizungumza na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake wakati akirejea kutoka kwenye hija ya kitume huko Amerika ya Kusini, hija ambayo, itaendelea kubakiza chapa ya kudumu katika maisha na utume wake, kwani ameguswa kwa ukarimu na upendo ulioneshwa na Familia ya Mungu huko Amerika ya Kusini.

Haya yamesemwa na Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya mawasiliano mjini Vatican. Utamaduni na ulimwengu wa digitali ni mambo ambayo yanaanza kuingia taratibu katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko, kwani ni kiongozi ambaye anapenda kuzungumza na watu kutoka katika undani wa mioyo yao; kwa maneno machache yanayoacha chapa ya kudumu, kama alivyofanya tangu siku ile ya kwanza alipojitokeza hadharani baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki.

Nguvu ya mawasiliano inayooneshwa na Baba Mtakatifu inawagusa hata wale wanaoliangalia Kanisa kwa jicho la “kengeza”. Baba Mtakatifu alipokuwa nchini Paraguay, kabla ya kuondoka na kurejea tena mjini Vatican alibahatika kukutana na kuzungumza na vijana kutoka Paraguay. Alisikiliza kwa makini shuhuda zilizokuwa zinatolewa na vijana, akaandika pembeni yale yaliyomgusa katika shuhuda hizi. Vijana walipomaliza shuhuda zao, Baba Mtakatifu akawashukuru na kuwaambia kwamba, alikuwa ameandika hotuba ambayo angewasomea, lakini, akaiweka pembeni na kuanza kuwashirikisha yale yaliyomgusa kutokana na shuhuda zilizotolewa na vijana.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, kwake kuwasomea watu hotuba iliyoandikwa inampatia taabu sana ndiyo maana mara kadhaa ameweka pembeni hotuba iliyoandikwa na kuanza kuwashirikisha watu yale yanayomgusa. Fasihi andishi ina sheria na kanuni zake, lakini fasihi simulizi ina uwezo wa kutoa muhtasari, kunyambulisha na kufafanua mambo; kuyapatia mwelekeo na vionjo kadiri ya mazingira na hadhira inayokusudiwa.

Monsinyo Dario Edoardo Viganò anasema kwamba, Baba Mtakatifu anapenda kukazia mazingira ya watu anaozungumza nao kama ilivyojitokeza wakati alipokuwa anazungumza na bahari ya vijana kutoka Paruaguay. Dhana hii ameikazia pia wakati akizungumza na waandishi wa habari, kutambua umuhimu wa kuweka kila jambo mahali pake, ili kupata maana inayokusudiwa. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, Injili ya Furaha, “Evangelii gaudium” anakaza kusema ni hatari kubwa kuishi katika ulimwengu unaotawalia zaidi na maneno, picha na mambo yanayoelea katika ombwe na kusahau hali halisi inayomsibu mwanadamu.

Fasihi simulizi inajikita katika uwelewa, mang’amuzi na hali halisi ya maisha ya mwanadamu na kamwe si jambo la kufikirika tu. Baba Mtakatifu ni kati ya wale ambao wamezaliwa na kukulia kwenye utamaduni wa vitabu, lakini ni bingwa katika matumizi ya fasihi simulizi, ili kuwasaidia wasikilizaji wake kupata ujumbe anaokusudia. Mara kwa mara anapenda kukazia maarifa kwa kurudia maneno msingi katika hotuba yake, mambo ambayo anataka wasikilizaji wake waweze kuyazingatia katika safari ya maisha yao.

Baba Mtakatifu anatambua kasoro zinazoweza kujitokeza katika mawasiliano, kiasi kwamba, hata wakati mwingine watu wakapitiwa na baadhi ya maneno, kumbe anaporudia maneno makuu analenga kukazia zaidi ujumbe wake. Baba Mtakatifu Francisko anapozungumza na vijana, anajiweka katika mazingira ambayo yatamwezesha kuweza kufahamika, ili kujenga na kuimarisha mawasiliano ambayo leo hii yameboreshwa sana na kuufanya ulimwengu kuwa kama kijiji kama anavyokaza kusema McLuhan.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutumia mtindo wa mawasiliano ya majadiliano na wasikilizaji wake, ili kwenda pamoja; anataka kuwavuta vijana wa kizazi kipya wanaoogelea katika ulimwengu wa digitali kutambua na kuthamini pia Fasihi simulizi na andishi, ili kuimarisha mawasiliano na wasikilizaji wake; ni kiongozi anayependa kuwamegea watu Injili ya Furaha inayojikita katika tunu msingi za maisha ya mwanadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.