2015-07-28 15:07:00

JK apongezwa kwa kuachia ngazi kwa amani nchini Tanzania


Waziri Mkuu wa Australia, Bwana Tony Abbot amempongeza Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuamua kukabidhi madaraka kwa kiongozi mwingine kwa mujibu wa Katiba nchini Tanzania. "Nakupongeza sana kwa uamuzi wako wa kukabidhi madaraka kwa amani nchini kwako , ni jambo la nadra sana Barani Afrika, kuwa na utaratibu mzuri na wa Amani namna hii" Bw. Abbot amemwambia Rais Kikwete na kumweleza awe na uhakika kuwa " Australia itaendelea kuisaidia Tanzania katika juhudi zake za kuleta maendeleo na kukuza uchumi" ameongeza.

Rais Kikwete na Waziri Mkuu Abbot pia wamezungumzia jinsi nchi zao zinaweza kuendelea kushirikiana katika kulinda usalama baharini, kukuza zaidi ushirikiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kijamii. Rais Kikwete yuko nchini Australia kwa mwaliko rasmi wa Kiserikali kutoka kwa Gavana Mkuu wa Australia Mheshimiwa Peter Cosgrove. Rais Kikwete amepokelewa asubuhi tarehe 28 katika makao Makuu ya kiongozi wa Australia kwa heshima zote kwa kupigiwa mizinga 21 na kuandaliwa chakula rasmi cha mchana na baadae kupanda mti kuashiria kuimarisha mashirikiano baina ya nchi hizi mbili kwa kipindi kirefu kijacho.

Tanzania na Australia zimedumu katika ushirikiano baina ya nchi zao tangu miaka ya sitini na sasa nchi mbili hizi zimeazimia kuimarisha mahusiano haya zaidi katika sekta mbalimbali zikiwemo za uwekezaji na biashara kati yao. Baadaye Jumanne jioni, Rais Kikwete atakutana na wawekezaji wakubwa wa Australia ambao tayari wanawekeza nchini Tanzania kwa ajili ya mazungumzo ya namna ya kuendeleza sekta mpya ya gesi nchini na jinsi Tanzania inaweza kunufaika kutokana na kupata gesi.

Tayari Serikali ya Australia na makampuni binafsi ya gesi na mafuta, yanaisaidia Tanzania hasa katika vyuo vya ufundi stadi VETA na tafiti mbalimbali katika Kilimo. Tarehe 29 Julai, 2015 Rais Kikwete anatarajia kutunukiwa digrii ya udaktari wa heshima ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Newcastle, kwa mchango wake mkubwa alioutoa katika uongozi kwa kipindi cha miaka 10 aliyokaa madarakani nchini Tanzania na Dunia kwa ujumla.

Na mwandishi maalum.








All the contents on this site are copyrighted ©.