2015-07-26 08:52:00

Mchungaji mwema kwa wanaoteseka huko Mashariki ya Kati!


Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia ujumbe wa heri na matashi mema Patriaki Gregoire Pierre XX Ghabroyan wa Kanisa la Cilicia la Waarmeni, baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa hili na kumwomba Papa kuridhia uchaguzi huu kama kielelezo cha umoja wa Kanisa. Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuchaguliwa kwake na kumtakia mafanikio yatakayo zaa matunda ajaa katika maisha na utume.

Anasema, uchaguzi wa Patriaki Gregoire umekuja katika kipindi kigumu na chenye changamoto kubwa kwa Kanisa kwani linakabiliwa na hali ngumu ya maisha ya Wakristo wa Armeni huko Mashariki ya kati. Pamoja na magumu yote haya, lakini Kanisa bado linaendelea kuonesha imani na matumaini yake kwa Kristo Mfufuka na kwamba, bado ulimwengu umesheheni kwa matumaini na huruma, kwa kutambua kwamba, Msalaba wa Kristo ni mti unaomkirimia mwanadamu zawadi ya maisha.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Patriaki Gregoire akiwa ameungana na Mababa wa Sinodi, akiwa anasindikizwa na nguvu ya Roho Mtakatifu na hekima ya Kiinjili, ataweza kuwa ni Baba,  kiongozi mkuu na mchungaji mwema kwa Kondoo ambao amekabidhiwa kwake na Mwenyezi Mungu. Mashuhuda wa imani kutoka Armenia pamoja na Mtakatifu Gregori wa Narek, Mwalimu wa Kanisa, watakuwa ni waombezi wake wakuu.

Baba Mtakatifu anasema, anaridhia umoja wa Kikanisa ambao amemwomba mintarafu Sheria, Kanuni na Mapokeo ya Kanisa yanayotekelezwa kwa sasa. Anamtakia kheri na baraka katika maisha na utume wake pamoja na kumwombea tunza na ulinzi wa Bikira Maria, Mama wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.