2015-07-22 10:02:00

Viongozi jitahidini kuwa ni mifano bora ya kuigwa na jamii!


Kardinali Charles Maung Bo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Yangon, nchini Mynmar, anawataka wazazi na walezi kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli watu wema na mifano bora ya kuigwa na jamii. Hii pia ni changamoto kwa viongozi katika medani mbali mbali za kijamii kuonesha mfano bora wa kuigwa na kamwe wasiabudiwe kama miungu wadogo, bali watu wanaosimama kidete kutafuta na kuendeleza mchakato wa maendeleo na mafao ya wengi.

Kardinali Maung Bo anasema, katika kipindi cha miaka 50 nchi yao ilijikuta ikiogelea katika giza la utawala wa mabavu, watu wakakosa msingi bora wa familia. Ni matumaini yake kwamba, wakati huu wa demokrasia, tunu msingi za maisha ya kifamilia zitakuzwa na kuendelezwa zaidi, ili kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa unaopata chimbuko lake katika misingi na maisha ya kifamilia.

Kardinali Maung Bo anakaza kusema, myumbo wa uchumi kimataifa unaendelea kuwa ni kati ya vikwazo vinavyokwamisha mfungamano wa maisha ya kifamilia. Kuna maelfu ya vijana ambao wametoka kwenye familia zao kwenda nje ya nchi ili kutafuta fursa za ajira na maisha bora zaidi. Umaskini wa hali na kipato ni janga la familia nyingi kiasi hata zinashindwa kutekeleza dhamana na majukumu yake barabara.

Umoja na mshikamano wa familia nchini Myanmar bado ni dhaifu, hapa kuna haja kwa waamini pamoja na wananchi wenye mapenzi mema kusimama kidete kuhakikisha kwamba, tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 40% ya wananchi wa Myanmar wanaishi katika umaskini mkubwa wa hali na kipato.

Familia zimegawanyika kutokana na athari za biashara ya binadamu inayoendelea kunyanyasa utu na heshima ya binadamu. Kuna maelfu ya watoto ambao wanakosa fursa ya kupata elimu bora, biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na kinzani na migogoro ya kijamii ni mambo ambayo yanaendelea kusambaratisha misingi ya familia nchini Myanmar.

Sera za maendeleo zijikite katika utu na heshima ya binadamu na wala si kwa ajili ya kutafuta faida kubwa. Kardinali Charles Maung Bo anasema, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wana dhamana na wajibu wa kuwakumbuka na kuwaombea viongozi wao, ili waweze kutenda kazi na wajibu wao barabara, daima wakitafuta kulinda, kutetea na kukuza utu na heshima ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.