2015-07-22 07:03:00

Katika sera na mikakati ya uchumi, mwanadamu apewe kipaumbele cha kwanza


Wajumbe wa vyama vya kiraia waliokuwa wanakutanika Santa Cruz de la Sierra nchini Bolivia kuanzia tarehe 7 hadi hadi 9 Julai 2015, pamoja na mambo mengine walikazia kuhusu; mazingira, kazi na makazi. Wanakubaliana kimsingi na changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira kwani hii ni nyumba ya wote. Katika sera na mikakati ya uchumi na maendeleo, binadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na wala si rasilimali fedha na vitu.

Wajumbe wa vyama vya kiraia wanasema, kilio chao ni kwa watu ambao wanatengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, changamoto kwa wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kwamba, mwelekeo huu ni batili katika ustawi na maendeleo ya wengi. Kundi hili haliwezi kuendelea kukubali kunyonywa na kudhalilishwa, bali linataka kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maisha, unaoheshimu utu wa binadamu, mafao na ustawi wa wengi.

Kwa kutambua dhamana hii kubwa mbele yao, wajumbe hawa katika tamko ambalo wamemkabidhi Baba Mtakatifu Francisko  wamekazia mambo makuu kumi ambayo wanataka kuyavalia njuga kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu wengi. Kusaidia mchakato wa mabadiliko, kuwa na mahusiano mema na mazingira; kutetea kazi bora sanjari na uboreshaji wa mazingira na makazi ya watu; kulinda mazingira na kukuza sekta ya kilimo; kujenga na kudumisha amani pamoja na utamaduni wa watu kukutana.

Wajumbe wa vyama vya kiraia wanasema kwamba, wanataka kupambana fika na vitendo vya ubaguzi, ili kudumisha uhuru wa watu kujieleza pamoja na kuhakikisha kwamba, maendeleo ya sayansi na teknolojia yanatumika kwa ajili ya huduma ya ustawi na maendeleo ya binadamu na mwishoni, wanakataa katu katu kutumbukizwa katika sera ya ulaji na badala yake wanapenda kujenga na kudumisha mshikamano na maendeleo ya maisha.

Wajumbe wa vyama vya kiraia wanasema kwamba, wanapenda kushiriki kikamilifu katika mchakato unaopania kuleta mabadiliko katika maisha ya mwanadamu kwa kukataa miundo mbinu iliyopelekea watu kutawaliwa, kunyonywa na kudhalilishwa utu na heshima yao kama binadamu.

Wataendeleza mapambano ili kuhakikisha kwamba, watu wanajitahidi kuiishi falsafa ya amani na maridhiano kati yao pamoja na mazingira wanamoishi. Pawepo na matumizi bora ya ardhi kwa ajili ya mafao ya wengi pamoja na kuhakikisha kwamba, nchi zinatunga sheria na kanuni za kulinda na kuendeleza mazingira bora. Harakati hizi hazina budi kwenda sanjari na utetezi wa haki msingi za watu mahalia katika ngazi ya kitaifa na kimataifa, ili kuendeleza majadiliano yatakayosaidia kupata suluhu ya kudumu kuhusiana na migogoro na kinzani iliyojitokeza kati ya watu mahalia, wakulima na wahamiaji.

Wajumbe hawa wanakaza kusema, kazi ni kielelezo cha utu na heshima ya binadamu na kwamba, hii ni haki msingi kwa wote. Wanapenda kuona kwamba, watu wanafanya kazi katika mazingira bora, wakiwa na uhakika wa usalama wa maisha yao kadiri ya mifumo ya hifadhi za kijamii pamoja na kuwa na uwakilishi unaotetea masilahi ya wafanyakazi. Wanapenda kuona watu wengi wanahusishwa katika masuala ya kazi.

Kutokana na ongezeko la wahamiaji, wakimbizi na wageni, wanaiomba Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, watu hawa wanaheshimiwa na kuthaminiwa utu wao na kamwe wasibaguliwe wala kutumbukizwa kwenye kazi za suluba, biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; mambo ambayo yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu. Sera na mikakati ya kiuchumi itoe kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu, umoja na mshikamano kati ya watu.

Wajumbe katika tamko lao, wanalaani vitendo vya ukwapuaji wa maeneo makubwa ya ardhi kwa matumizi ya watu binafsi; watu kuhamishwa kwa nguvu katika makazi yao pamoja na ongezeko la makazi duni mijini. Wanapinga nyanyaso zinazofanywa dhidi ya watu wanaotetea sera za makazi bora ya watu, kwani makazi ni haki msingi ya binadamu, changamoto kwa Serikali na wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, haki hii inatekelezwa, kwa kujenga makazi ya watu yanayozingatia usalama na utu wa watu.

Wajumbe wanataka kuwepo na sera pamoja na mikakati ya kilimo endelevu kitakachosaidia kupambana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha duniani; kwa kulinda mazao asilia ili kukuza na kudumisha zawadi ya maisha na afya ya binadamu; utunzaji bora wa mazingira pamoja na mchango unaotolewa na watu mahalia katika sekta ya kilimo na utunzaji bora wa mazingira.

Kuna haja ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kwa kukazia mchakato wa ujenzi wa madaraja ya watu kutoka katika dini, tamaduni na makabila mbali mbali kukutana na kuishi kwa amani na utulivu. Urithi wa tamaduni mahalia unapaswa kulindwa na kuendelezwa. Wajumbe wanakataa katu katu: ukoloni na ukoloni mamboleo unaojitokeza katika mfumo wa msaada wa kijeshi, fedha au mawasiliano. Viongozi wanaopatikana na hatia wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria ili kujibu tuhuma zinazowasibu.

Wajumbe wanasema kuna haja ya kujifunga kibwebwe ili kupambana na mifumo ya ubaguzi, kwa kutambua kwamba, wote ni sawa na wana haki sawa. Wajumbe wanalaani vitendo vya: mauaji, nyanyaso na dhuluma dhidi ya wanawake. Hapa kuna haja ya kuhakikisha kwamba, Jamii inajenga na kudumisha uhuru wa watu kujieleza, ili kukuza demokrasia, utawala na uhuru wa mtu. Wananchi wawe na uhuru na haki ya kuandamana.

Wajumbe hawa wanasema, maendeleo ya sayansi na teknolojia hayana budi kuwa ni kwa ajili ya huduma na ustawi wa binadamu wengi na kamwe yaistumike kwa ajili ya kujitafutia faida kubwa wala utajiri. Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu visaidie maboresho ya maisha ya wengi katika sekta ya afya, elimu na ustawi wa jamii. Wajumbe wanataka kujenga na kudumisha mshikamano kwa kujifunga kibwebwe kupambana na ubinafsi, uchu wa mali na madaraka; wivu usiokuwa na mvuto wala mashiko pamoja na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengi. Kwa pamoja wanataka kujenga madaraja kati ya watu, ili kubomoa kuta za utengano na unyonyaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.