2015-07-22 11:58:00

"First Ladies" Barani Afrika katika mapambano dhidi ya Saratani!


Jukwaa la wake wa marais kutoka Barani Afrika, Jumatatu tarehe 20 Julai 2015 limekutanika Jijini Nairobi, Kenya katika mkutano wake wa tisa ili kujadili jinsi ya kupambana na Saratani ya matiti na tezi dume miongoni mwa wananchi Barani Afrika. Hadi sasa jukwaa la wanawake wa marais limefaulu kuhamasisha umma kuhusu ugonjwa wa Saratani na sasa kuna haja ya kuendeleza wajibu huu kwa kuhakikisha kwamba, watu wanapata nafasi ya kupimwa, kuzuia na hatimaye kupata tiba kwa wale watakaogundulika kwamba, wana Saratani.

Haya yamesemwa na Mama Margaret Kenyatta, mke wa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ambaye alikuwa ni mwenyeji wa mkutano huu. Amewataka wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya Saratani, ili kusaidia mchakato wa maboresho ya watu wengi Barani Afrika ili hatimaye, waweze kuchangia katika ustawi na maendeleo yao.

Wananchi Barani Afrika wanapaswa pia kuwa na maisha ambayo yatawasaidia kufanya mazoezi ya viungo ili kuupatia mwili kinga inayohitaji pamoja na kupata lishe bora na salama. Vijana wa kizazi kipya wametahadharishwa kuhusu ulaji ovyo wa vyakula vinavyoweza kuwasababishia magonjwa na hitilafu mwilini. Mama Kenyatta ameitaka Serikali ya Kenya kuunga mkono mapambano dhidi ya ugonjwa wa Saratani unaoendelea kupoteza maisha ya watu millioni 8 kila mwaka kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Nafasi ya Uenyekiti wa Jukwaa la Wanawake wa Marais Barani Afrika kwa sasa imechukuliwa na Mama Monica Geingo, mke wa Rais wa Namibia. Mkutano huu umehudhuriwa na Mama Nana Lordina Mahama kutoka Ghana, Salma Jakaya Kikwete, Tanzania, Tobeka Madima Zuma, Afrika ya Kusini na Lalla Malika Issouffou Mahamadou, Nigeria, kwa kutaja baadhi ya wanawake hawa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CISA. 








All the contents on this site are copyrighted ©.