2015-07-21 11:35:00

Kifo laini si bure! Kuna mkono wa mtu!


Wakristo nchini Ujerumani wanaungana kwa pamoja, ili kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sheria iliyopitishwa na Bunge la Ujerumani hivi karibuni, ili kuwasaidia watu kupata matibabu ya kifo laini. Viongozi wa Makanisa nchini Ujerumani wanasema, wasingependa kuona kifo laini linakuwa ni jambo la kawaida kabisa machoni mwa wananchi wa Ujerumani.

Maisha ya binadamu ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, yanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa, tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Hii ni changamoto inayotolewa na Kardinali Reinhart Marx, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani kwa kushirikiana na Mchungaji Heinrich Bedford-Strohm, Rais wa Baraza la Makanisa ya Kiluteri ya Kiinjili nchini Ujerumani.

Wagonjwa walioko kufani wanapaswa kupatiwa matibabu hadi pale Mwenyezi Mungu atakapowaita na kwamba, ni dhamana na jukumu la Serikali kuhakikisha kwamba, linaboresha huduma ya afya kwa watu wake, ili kulinda na kutetea zawadi ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba, hadi mauti ya kawaida yanapomfika. Maisha ya binadamu yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa jamii inayoheshimu utu na ustawi wa watu wake, badala ya kuwachimbia kaburi kwa kuwapatia huduma za kifo laini.

Majadiliano ya sheria ya kifo laini nchini Ujerumani yamevuta hisia za wengi kiasi cha kuwagawanya wananchi wenyewe kwa baadhi yao kuunga mkono na wengine kubeza sheria ambayo inakiuka haki msingi za binadamu. Ni nani mwenye dhamana ya kuamua mauti au maisha ya mtu? Madaktari au wahudumu wa familia majumbani? Wananchi wengi nchini Ujerumani wanaitaka Serikali kuu kuboresha huduma za afya sanjari na kuheshimu zawadi ya maisha.

Kanisa Katoliki nchini Ujerumani limekuwa mstari wa mbele kupinga utamaduni wa kifo unaokumbatiwa wakati mwingine na sheria za nchi. Kifo laini ni mradi unaowaingizia watu waliofilisika kimaadili kwa kutoguswa na mateso ya jirani zao kiasi kikubwa cha fedha. Kumbe, kifo laini si bure! Kuna mkono wa mtu! Kuna haja kwa Jamii kutambua, kuheshimu na kuthamini maisha ya wagonjwa, walemavu na wazee kuwa ni kito cha thamani kubwa, kinachopaswa kulindwa kwa nguvu zote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.