2015-07-20 13:02:00

Njia ya asili ya mpango wa uzazi inajikita katika utakatifu wa maisha!


Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani kuanzia Jumapili tarehe 19 hadi tarehe 25 Julai 2015 linaadhimisha, juma la “Njia ya asili ya mpango wa uzazi, “BOM” muhimu sana kwa ustawi wa maisha ya mwamini kiroho na kimwili. Lengo la kampeni hii, ni kuwawezesha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusherehekea Injili ya Familia kwa kuambata Injili ya Uhai, inayoheshimu na kuthamini mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Kanisa linataka kuwasaidia waamini kutambua na kuthamini njia ya asili ya mpango wa uzazi kadiri ya Mafundisho Kanisa, ili kusimama kidete kushuhudia Injili ya Uhai, dhidi ya utamaduni wa kifo unaoendelea kusambaa duniani kama moto wa kipindi cha kiangazi.

Tarehe 25 Julai 1968, Mwenyeheri Paulo VI alichapisha Waraka wa Kitume “Humanae vitae” yaani “Maisha ya mwanadamu”; Waraka ambao unachambua kwa kina na mapana utakatifu wa tendo ndoa katika maisha ya ndoa na familia; upendo wa dhati kati ya wanandoa na dhamana katika kulea na kuwatunza watoto ambao kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Tarehe 25 Julai, 2015 inatangulia pia Kumbu kumbu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Julai.

Katika kipindi cha juma zima, Parokia zote nchini Marekani, zinaendelea kuhamasisha njia ya asili ya mpango wa uzazi, ili kuwasaidia waamini kufahamu na hatimaye, kushuhudia Injili ya Familia inayoambata Injili ya Uhai, dhidi ya utamaduni wa kifo. Huu ni wakati kwa Familia ya Mungu nchini Marekani kujitaabisha kufahamu Sakramenti ya Ndoa, kielelezo cha upendo wa dhati kati ya Bwana na Bibi na uaminifu unaopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo kwa ajili ya mchumba wake Kanisa.

Huu ni mwaliko kwa wanandoa kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana, wajibu na wito wao katika kuzaa, kulea na kuwatunza watoto ambao kwa hakika ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Njia ya asili ya mpango wa uzazi inawasaidia wanandoa kushirikiana kikamilifu katika mchakato wa utakatifu wa maisha, kwani njia hii inawawajibisha bwana na bibi katika maisha ya unyumba. Wanandoa wanapata nafasi ya kufahamiana zaidi na kutambua karama na vipaji ambavyo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu wanaposhiriki katika kazi ya uumbaji na malezi kwa ajili ya watoto wao.

Kumbe, Familia ya Mungu nchini Marekani inachangamotishwa na Mama Kanisa kutambua na kuthamini utakatifu wa tendo la ndoa, umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa na thamani ya Injili ya Familia, wanayotakiwa kuishuhudia kwa kuambata Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.