2015-07-20 10:01:00

Kanisa nchini Angola lasikitishwa na vipigo na mkong'oto unaotembezwa majumbani


Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Angola katika mkutano wake uliohitimishwa hivi karibuni, inasema, imepata fursa ya kutafakari kwa kina na mapana umuhimu wa kuanza maandalizi kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu uliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko na unatarajiwa kuzinduliwa rasmi hapo tarehe 8 Desemba 2015.

Wajumbe wa tume ya haki na amani wanasema kuna haja kwa Familia ya Mungu nchini Angola kujikita katika mchakato wa upatanisho wa kitaifa ili kuganga na kutibu madonda na mipasuko ya kijamii iliyosababishwa wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Baada ya mkutano huu, wajumbe wametoa waraka kwa ajili ya Familia ya Mungu nchini Angola.

Kwa namna ya pekee, Majimbo Katoliki nchini Angola yanahamasishwa kuwa na Tume za haki na amani pamoja na kuhakikisha kwamba, tume za majimbo zinashirikiana kwa karibu kwa ajili ya huduma kwa Familia ya Mungu nchini Angola. Tume hizi ziwe makini kuangalia haki msingi za binadamu, utunzaji bora wa mazingira pamoja na changamoto mbali mbali zinazojitokeza nchini humo kuhusiana na utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi. Lengo ni kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha ya Familia ya Mungu nchini Angola.

Wajumbe wanasikitishwa sana na nyanyaso pamoja vipigo vya majumbani wanavyotendewa wanawake na baadhi ya wanaume, ambao, kutokana na “uzalendo na aibu” pengine wanakosa ujasiri wa kusema mambo haya hadharani, kwani kilio cha mwanaume eti ni macho makendu! Lakini wajumbe wa tume ya haki na amani nchini Angola wanasema yapo na wala si utani, kuona mwanamke akitembeza mkong’oto kwa mwanaume wake! Kuna haja ya kuendesha kampeni itakatosaidia kudhibiti vitendo vya ukatili wa majumbani na nyanyaso dhidi ya wanawake na watoto.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu, iwe ni fursa ya kuanzisha mchakato wa upatanisho wa kitaifa, kwa kuangalia kwa namna ya pekee: haki msingi za wafungwa magerezani; kwa kushikamana na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ili kuondokana na umaskini; kuonesha upendo kwa wahamiaji, wakimbizi na wageni kwa kutambua kwamba, upendo na ukarimu ni vinasaba na utambulisho wa Wakristo.

Wanasheria Wakatoliki wawe tayari kutoa msaada wa kisheria kwa watu wasiokuwa na uwezo, ili waweze kupata haki zao msingi, sanjari na kukazia umuhimu wa kudumisha uwazi na ukweli katika masuala ya biashara na mikataba ya kimataifa, ili iweze kuleta mafao, ustawi na maendeleo kwa wananchi wa Angola badala ya mikataba hii kuwanufaisha wajanja wachache ndani ya jamii. Wajumbe wa Tume ya haki na amani, Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, panapo majaliwa, watakutana tena mwezi Julai, 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.